Social Icons

Saturday, April 30, 2011

MTOTO WA MFALME, WILLIAM AFANYA KUFURU KWA KUFUNGA NDOA YA KIFAHARI ILIYOGHARIMU MABILIONI YA PESA


Mwana mfalme William akifungishwa ndoa na Aksofu Rowan William katika kanisa la Westminster Abbey jijini London.

MTOTO wa mfalme wa Uingereza, Prince William na Kate Middleton wamefunga ndoa katika kanisa la Westminster Abbey jijini London.

Takriban wageni 1,900 walishuhudia tukio hilo ndani ya kanisa, na mamilioni wakifuatilia majumbani mwao kwa njia ya televisheni.


Maharusi hao walishangiliwa na maelfu ya watu waliojipanga barabarani kuelekea kasri ya Buckingham Palace ambako Malkia amewaandalia karamu wageni 650.


Wana ndoa hao wapya walitumia gari liliovutwa na farasi la muundo wa mwaka 1902 ambalo lilitumiwa na wazazi wake Prince William wakati wa ndoa yao mwaka 1981.


Maharusi hao baadaye walijitokeza kwenye roshani ya kasri ya Buckingham na kuwasalimu maelfu ya watu waliokwenda kuwasherehekea.


Baada ya kulishana viapo vya ndoa Askofu mkuu wa Canterbury, Rowan Williams, aliwanadi rasmi kuwa "mume na mke"

RAIS JAKAYA KIKWETE AWAAPISHA MANAIBU KATIBU WAKUU IKULU DAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, akimwapisha John Thomas Mngodo, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi wakati wa hafla fupi ya kuapishwa Manaibu Katibu Wakuu iliyofanyika kwenye Viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam leo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, akimwapisha Mwamini Juma Malemi, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakati wa hafla fupi ya kuapishwa Manaibu Katibu Wakuu iliyofanyika kwenye Viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja na wanafamili wa naibu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, akifurahia na mtoto, Irene Simba ambaye ni mtoto wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwamini Juma Malemi (kushoto)




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, akimwapisha Anna Maembe. kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Jakaya Kikwete (katikati) Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakipiga picha ya kumbukumbi na Manaibu Makatibu Wakuu, baada ya kuapishwa rasmi.

Rais Jakaya Kikwete, Makamu wake Dkt Mohamed Gharib Bilal, wakipiga picha ya kumbukumbi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na JKT, Eng. Mussa Ibrahim, akiwa na familia yake baada ya kuapishwa rasmi.

Makamuwa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilal, akizungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati wa hafla hiyo.

FARAJA KIHONGOLE WA CHANEL TEN AFUNGA NDO LEO KANISA LA ST. PETER

Mwandishi wa habari mwandamizi wa kituo cha Televisheni cha Chanell Ten, Faraja Kihongole akiwa na akipozi na mumewe, Projestus Rwegarulila, baada ya kufunga pingu za maisha leo jioni katika Kanisa la Mtakatifu Peter Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Faraja Kihongole, akiingia kanisani na mumewe, Projestus Rwegarulila,
kwa ajili ya kufunga ndoa yao leo jioni.
Faraja akiwa na Mumewe Rwegarulila, wakionyesha vyeti vya ndo baada ya kukabidhiwa kanisani hapo.

TIMU YA TAIFA YA TANZANIA CHINI YA MIAKA 23 YATUPWA NJE

Mchezaji wa timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya miaka 23, Thomas Ulimwengu (kushoto) akiambaa na mpira kumtoka beki wa wa timu ya Uganda (U 23) wakati wa mchezo wa marudiano wa kufuzu kucheza michuano ya All African Games inayotarajia kufanyika mwezi Septemba mwaka huu huko Msumbiji. Mchezo huo umechezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam,ambapo Uganda imeibuka na ushindi wa mabao 3-1.


HATA hivyo timu hiyo ya Tanzania imeshindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kulazimishwa kufungwa mabao 3-1 katika mchezo huo wa marudiano baada ya ule wa awali uliochezwa Nchni Uganda ambapo pia Tanzania ‘Manyara’ ililala kwa mabao 2-1.

Kwa hatua hiyo sasa Tanzania U23 imetupwa nje ya mashindano ya All African Games yanayotarajia kufanyika mwezi Septemba mwaka huu huko Msumbiji baad kukubali kufungwa jumla ya mabao 5-2.


Uganda ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika za mwanzo za mchezo huo na baadaye kuandika bao la pili na kufanya timu hizo kwenda mapumziko huku Uganda ikiwa mbele kwa mabao 2-0.


Kipindi cha pili Mbwana Samatta aliwainua mashabiki baada ya kuifungia timu yake bao 1 na la kufutia machozi kabla ya Uganda kufunga bao la 3 na la ushindi lililozima ndoto na matumaini ya watanzania ya kushinda mchezo huo.


Bao hilo ndilo hasa lilizamisha Jahazi la Tanzania na kuwafanya mashabiki lukuki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo kuanza kuinuka vitini na kuanza safari za kurejea makwao.”TANZANIA UNDER 23 OUT MICHUANO YA ALL AFRICAN GAMES 2011”

WAKAZI WA DAR WANAVYOJIACHIA USIKU

Mashabiki wa Bendi ya Akudo Impact wakiserebuka katika onyesho lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mango Garden uliopo Kinondoni jijini.


Wanenguaji wa Bendi ya Akudo wakiwajibika jukwaani.


Mackey Fanta (katikati) akinengua na wanamuziki wake wa Nina La Musica katika onyesho lililofanyika Ukumbi wa Twiga Kitunda.


Wanenguaji wa Bendi ya Extra Bongo wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati bendi yao ilipotumbiza Ukumbi wa Meeda uliopo Sinza


Wanenguaji wa Bendi ya Extra Bongo, wakinengua kwa staili ya Kulamba sakafu.

Thursday, April 28, 2011

JANE MISO KUPANDISHWA KIZIMBANI

MWIMBAJI wa nyimbo za Injili anayetamba na Kibao cha Omoyo, Jane Miso (pichani), anatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuchikichia kiasi cha shilingi milioni kumi alizopewa kama mkopo na promota aliyefahamika kwa jina la Benson Mafuwe.

Akizungumza na mateja 20 pande za Mwananyamala, Dar es Salaam juzi, Mafuwe alisema kuwa kitu kinachomfanya kumfikisha mahakamani Jane ni kitendo chake cha kushindwa kuwa muungwana na kumtolea maneno ya vitisho.

“Nilidhani angekuwa muungwana na kuja tujue tunafanya nini, kumbe si hivyo, ndiyo kwanza alinipigia simu na kuanza kunitolea maneno ya kashfa, sasa mimi nataka mahakama iamue suala zima,” alisema Mafuwe.

CHALZ BABA ANG’ANG’ANIA THE ATRIUMS

Chalz Gabriel Baba ‘Chalz Baba’ akipata msosi na shabiki wake, Isabela Godfrey mkazi wa Kinondoni Moroco jijini Dar ijumaa iliyopita.

MUIMBAJI katika Bendi ya African Stars International ‘Twanga Pepeta’, Chalz Gabriel Baba ‘Chalz Baba’ Ijumaa ya wiki iliyopita alitoa mpya baada ya kugoma kuondoka kwenye Hoteli ya The Atriums iliyopo Sinza Afrikasana jijini Dar.

Kugoma huko kulitokana na kujiachia katika hoteli hiyo ya kifahari huku akiwa na shabiki wake, Isabela Godfrey mkazi wa Kinondoni Moroco jijini Dar.

Chalz Baba ‘alifuta’ wali na kuku mzima ambapo shabiki wake aliagiza Chips na kuku nusu huku kila mmoja akishushia grasi tatu za juisi aina ya pasheni ambapo huduma hiyo nzuri ndiyo iliyomsababishia muimbaji huyo kugoma kuondoka akidai aongezwe tena msosi kama ule alioletewa mara ya kwanza.

‘Siendi kokote yaani chakula kizuri namna hii mnanihudumia mara moja tu mbona nyinyi huwa mnaniandika mara kwa mara... siondoki hapa,’ alisema Chalz Baba.

Juhudi zakumtoa mwanamuziki huyo hotelini hapo zilifanikishwa na meneja mkuu wa hoteli hiyo kwa kumuahidi kumpa mwaliko siku si nyingi ili aje amalizie hamu yake.

Full kujiachia kwa Chalz Baba kulitokana na zoezi zima la Jiachie na staa linaloendeshwa na gazeti hili la kijanja na kudhaminiwa na hoteli hiyo ya kifahari.

Chalz Baba na shabiki wake huyo walifurahia huduma pamoja na mandhari nzuri ya hoteli hiyo ambapo muimbaji huyo aliahidi kwenda kusaka ‘mahela’ ili arudi kujinafasi katika ‘kiota’ hicho bomba kilichopo jijini Dar es Salaam.

CHENGE: SIJUI KAMA MIMI NI GAMBA CCM

MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (pichani) amesema anasubiri taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuona kama atapewa barua ya kumtaka ajivue nafasi zake za uongozi kwani hadi hivi sasa hajui kitu hicho.Kauli hiyo ya kwanza ya Chenge inakuja kipindi ambacho Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amekuwa akitangaza kwa nguvu mpango mkakati wa chama hicho kujivua gamba. Makada wa chama hicho wanaotakiwa kupima nafasi zao na uzito wa tuhuma zinazowakabili ni wale wanaohusishwa na kashfa mbalimbali zikiwamo za Richmond, Kagoda na wizi wa EPA.

Hata hivyo, Chenge jana alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kutajwa kwake kuwa mmoja wa wanachama wanaotakiwa kupima uzito wa tuhuma zinazowakabili na kujiondoa wenyewe ikiwa ni hatua ya chama hicho kujisafisha kwa kujivua gamba, alisema: "Sijui hicho kitu. Naheshimu vikao na taratibu za chama hilo ni jambo la chama si la vyombo vya habari."

Alisema chama kina taratibu zake za kiutendaji na kuongeza: "Siwezi kuanza kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo ambayo yana taratibu zake ndani ya chama."

Alisema kamwe hatakiuka taratibu za chama na kwamba uamuzi wote utakaofanyika au kutolewa huwa unafuata vikao vya chama.Alipoulizwa juu ya kusubiri kwake taratibu za chama wakati tayari jambo hilo linafahamika kwa umma alijibu: "Kwa ‘public’ ipi wewe? Mimi sijui hilo jambo, nasubiri taratibu za chama na siwezi kuzungumza zaidi nje ya chama."

Akizungumzia utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC-CCM), Nnauye alisema taratibu zimekuwa zikiendelea na kuwataka wananchi kuwa na subira.Juzi, Nnauye alikaririwa akisema kwamba taratibu hizo zingefanyika baada ya Sikukuu ya Pasaka na kusisitiza: "Ambacho nimekuwa nikikisema kiko palepale."

Mapema mwezi huu, NEC-CCM ilitoa muda wa siku 90 kwa watuhumiwa wote wa kashfa mbalimbali ndani ya chama hicho kujipima wenyewe na kujiondoa kwenye nafasi hizo vinginevyo, chama kingewang'oa kwa nguvu. Azimio hilo limekuwa likitangazwa kwa nguvu katika mikutano mbalimbali ya hadhara ikiwa ni mkakati wa chama hicho kurejesha imani chama kwa wananchi ambayo imeanza kupotea kutokana na tuhuma za ufisadi.

Juzi, Nnauye akizungumza na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC Taifa), alisema chama hicho hakitishiki na uwezekano wa makada hao kuhamia upinzani.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akihutubia sherehe za kuzaliwa chama hicho Februari 5, mwaka huu alitangaza mkakati huo wa chama kujivua gamba na kurejea katika misingi ya maadili ya uongozi iliyorithi kutoka Tanu na CCM ya nyuma.

Sekretarieti ya CCM kukutana kesho
Katika hatua nyingine Sekretarieti ya CCM inatarajiwa kukutana kesho kujadili pamoja na mambo mengine, utekelezaji wa maazimio ya Nec-CCM.

Kwa mujibu wa duru za kisiasa kutoka CCM, mkutano huo utajadili ajenda hiyo kwa kufanya tathmini ya azimio hilo na namna ya utekelezaji wake.Alipoulizwa jana, Nnauye alithibitisha kufanyika kwa mkutano huo lakini alisema ni kikao cha utendaji cha kawaida.Kwa mujibu wa Nnauye, kikao kama hicho kiliwahi kufanyika Mjini Dodoma baada ya kuundwa kwa sekretarieti hiyo na pia tayari ilikwishakutana Dar es Salaam.

Alisema kikao hicho si maalumu wala cha dharura na kwamba hufanyika mara moja kwa wiki.
"Siyo kikao cha dharura wala kikao maalumu, ni sehemu tu ya utendaji wa sekretarieti. Tunafanya vikao kama hivi mara moja kwa wiki, kwa hiyo hakuna kikao maalumu," alisema.

RAIA 82 WA SOMALIA WAKAMATWA MSITUNI MORO

Kundi la Wasomali likiwa chini ya ulinzi kwenye kituo kikuu cha polisi mkoani Morogoro.
WATU wapatao 82 raia wa Somalia wamekamatwa jana mchana kwenye msitu wa moja ya vijiji vya Wilaya ya Gairo mkoani hapa wakiwa safarini kuelekea jijini Dar es salaam kutafuta maisha.

Akizungumza na mtandao huu kwenye kituo kikuu cha polisi mkoani hapa, askari mmoja wa kikosi cha kutuliza ghasia wilayani Gairo maarufu kwa jina la 'voda fasta'alisema Wasomali hao walikamatwa baada ya polisi kupokea taarifa kutoka kwa raia wema.

"Tumepokea taarifa kutoka kwa raia wema wakitujuza kuwa kuna kundi la wasomali wanakata mbuga katika misitu ya Vijiji vya Gairo hivyo baada ya kuwafuatilia tumewakamata na kuwaleta hapa mkoani," alisema afande huyo aliyekataa kutaja jina lake kwa kuwa sio msemaji mkuu wa jeshi la polisi.

Mwandishi wetu aliwashuhudia Wasomali hao wakishushwa kwenye roli huku wakiwa na matope hali inayoonesha kuwa huenda wana muda mrefu hawajaoga kutokana na kutembea kwa muda mrefu.

Picha zaidi za Wasomali hao wakiwa mikononi mwa polisi:

Wednesday, April 27, 2011

‘BONGO MOVIES’ WAAMBULIA PATUPU TAMASHA LA SOKA PASAKA

'Bongo Movies' wakijiandaa na mchezo.
WACHEZA sinema nchini wanaojulikana kwa jina la utani la ‘Bongo Movies’ hawakuonyesha cheche zozote katika mchezo wa soka wa tamasha la Pasaka uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Tabata jijini Dar es Salaam ambapo uliwakutanisha wasanii hao na timu za Tabata Veteran, Paris Pub na Temeke Marketing.
Katika tukio hilo lililotoa burudani tosha kwa mashabiki wa soka, wasanii hao walikuwa kivutio kikubwa kutokana na umaarufu wao na jinsi soka lilivyoonekana kuzamisha juhudi zao wanazotumia kusimama mbele ya kamera.

Jackob Steven ‘JB’ akiweka misuli yake sawa.


Zuwena Mohammed ‘Shilole’ akiwahamasisha na Vuvuzela.


Steven Nyerere akiwa haamini kwamba timu yake imefungwa.


Sura za kukata tamaa za wasanii walioambulia patupu.

EXTRA BONGO, TWANGA PEPETA KUPIMANA UBAVU MORO MEI MOSI

Matangazo ya burudani itakayotolewa na bendi za Extra Bongo na African Stars.
BENDI mbili zenye upinzani mkali jijini Dar es Salaam, Extra Bongo 'Wazee wa Kisigino' na African Stars 'Twanga Pepeta’ wataonyesha makali yao mjini Morogoro siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo kitaifa itafanyika mkoani humo.

Bendi hizo ambazo zimesheheni wanamuziki nguli zitafanya shoo siku moja katika kumbi tofauti ambapo Etra Bongo watakuwa ukumbi wa Savoy uliopo katikati ya mji ambapo Twanga Pepeta watakuwa maeneo ya Nane Nane ukumbi wa Groness.

Bendi hizo zimekuwa “zikiibiana” wanamuziki kila mara kiasi cha kuzifanya ziimarike zaidi na hivyo kuzua ushabiki mkubwa wa wapenzi wa muziki nchini.




CCM KUJIVUA GAMBA


INAZUNGUMZWA sana mitaani , dhana hii ya CCM kujivua gamba. Najiuliza, je, huku ni ‘ Kuzaliwa kwa Chama ‘kipya’ au kuzaliwa ‘upya’ kwa chama kikongwe? Unaweza kukiona ninachokiona kadri unavyofuatilia mtiririko wa fikra zangu.

Nionavyo, wengi tumebaki tukijadili kilicho juu ya gamba. Hatuzami kuangalia kilichomo ndani ya gamba. Ndio maana, kama kawaida yetu, tumejikita kwenye kujadili zaidi majina ya watu.

Na tujiulize; ni nini hasa maana ya CCM kujivua gamba? Ni bahati mbaya, kuwa neno kujivua gamba linatoa tafsiri nyingi hasi na chanya. Na wakati mwingine, limewahamisha watu kutoka kwenye hoja za msingi juu ya nini kinachotokea . Mimi nitaelezea kujivua gamba kwa kutoa mfano wa nyumba .

Ndio, CCM ni chama kikongwe. Ni kama nyumba kongwe. CCM wanataka kuikarabati upya nyumba yao. Ipate mwonekano mpya. Kuikarabati upya nyumba kongwe huweza pia kupelekea kuibomoa nyumba yenyewe. Kutakuwa na fito na vipande vya matofali vya kurudishia. Kutahitajika fito na matofali mapya pia. Ndio, fito na matofali mengine yatakuwa ni ya kutupa tu, na ni lazima yatupwe, basi. Na hapo utakuwa umeikarabati upya nyumba yako.

Na nyumba kongwe ya CCM kwa sasa imechakaa, haina mvuto. Wengi hawaipendi, na hususan vijana. Hawa ndio hao walio wengi kwenye kupiga kura. Kwa CCM kurudisha imani ya wapiga kura hawa inahitaji kufanya ukarabati mkubwa wa nyumba yake kongwe. Katika Afrika hii kuna kisa cha Chama tawala kilichochukiwa mno na wapiga kura kiasi kikaamua kubadilisha jina na rangi ya bendera yake ya chama!

Turudi kwenye gamba. Hivyo basi, katika kujivua gamba huku, CCM, kama nyumba kongwe inayofanyiwa ukarabati, yumkini inaweza kubomoka. Hayo yatakuwa ni matokeo ya kawaida kabisa. Ndio, kuna watakaondoka na fito na matofali yao, watakwenda kujenga mahali pengine. Na katika mchakato huu wa kujivua gamba kuna mawili nayaona yatatokea; Mosi, CCM Kuzaliwa Upya au pili, Kuzaliwa kwa Chama kipya. Na mawili hayo yakitokea yatadhihirisha ukweli wa alichoandika Mwalimu Nyerere kwenye kitabu chake; ’ Uongozi Wetu Na Hatima Ya Tanzania’. Hapa kuna mawili, ama kuna Wana- CCM waliosoma kitabu hicho cha Mwalimu bila kukielewa au hawakukisoma kabisa.

Na nini maana ya Kuzaliwa kwa Chama Kipya? Naikumbuka vema Jumamosi ya Februari 5, 1977. Siku hiyo nilibaki na mwezi na wiki moja kabla sijatimiza miaka 11. Ni siku ile Chama Cha Mapinduzi kilipozaliwa. Nikiwa na watoto wanzangu tulikwenda pale ofisi za TANU Ilala Boma kushuhudia tukio lile la kihistoria. Nilichoshuhudia pale Ilala Boma ni ’Kuzaliwa Kwa Chama Kipya’. Niliziona nyuso nyingi za watu wazima zilizojaa matumaini ya siku zijazo, nasi kama watoto, ujio wa Chama kipya ulitujengea matumaini ya baadae.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini.

Na imani ya wananchi kwa viongozi wao ni shina la matumaini yao. Inakuwaje basi mwananchi anapokosa imani kwa kiongozi? Jibu; hukosa matumaini. Atakimbilia popote pale anapoona kuna matumaini. Wahenga walinena; mtoto akikosa titi la mama, atanyonya hata la mbwa. Chama Cha Mapinduzi kihistoria kimekuwa ni kimbilio la wanyonge, lakini sivyo ilivyo kwa sasa.

Na tuamini, kuwa Jakaya Kikwete ameingia katika kazi ya kuongoza Mabadiliko Makubwa ndani Ya CCM. Mwingine atauliza; Je, mabadiliko hayo yatakuwa makubwa kwa kiasi gani? Jibu; ni suala la kusubiri na kuona. Na hapo ndipo tutaweza kutoa hukumu stahili.

Ieleweke, kuwa CCM ni Chama tawala. Kinachotokea ndani ya CCM chaweza kuwa na athari chanya au hasi kwa taifa letu. Na ndio maana, kwa kutanguliza maslahi ya nchi, tuna wajibu wa kumuunga mkono Rais wa nchi na Mwenyekiti wa CCM katika kazi yake hii.

Nimepata kuandika, kuwa ya CCM yanatuhusu sote, wanachama na tusio wanachama. Kwa sasa, CCM inapitia moja ya vipindi vigumu sana tangu kuanzishwa kwake, hivyo basi, nchi yetu nayo inapitia moja ya vipindi vigumu sana tangu tupate uhuru. Hiki ni Kipindi Cha Mpito kuekelea kwenye mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Na hakuna atakayeweza kuyauzuia mabadiliko haya makubwa, maana wakati umebadilika. Chama Cha Mapinduzi kina jukumu la kuyaongoza mabadiliko haya. Na nimepata kuandika, kuwa CCM ina mawili ya kuchagua; kuendanda na mawimbi ya mabadiliko haya, au kukubali kusombwa na kutupiliwa kando.

Yumkini Jakaya Kikwete amezisoma alama za nyakati. Na hakika, sikupata kufikiri, kuwa katika mwaka wa kwanza tu wa awamu yake ya mwisho ya uongozi, Jakaya Kikwete angekifikisha chama chake katika hatua ya kujivua gamba kama tunavyoshuhudia.

Tunaona, CCM imeanza kujivua gamba, lakini hiyo haitoshi. Taifa letu nalo linahitaji kujivua gamba. Na sisi , kama taifa, hatutakuwa wa kwanza, imetokea katika nchi za wenzetu. Kuna mifano hai.

Utawala wa Kikomunisti wa Urusi ya zamani ulianguka mara ile Mikhael Gorbachev alipoanzisha mageuzi makubwa ya kimfumo kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Urusi. Mabadiliko haya makubwa ya kimfumo yalipata majina mawili; Perestroika na Glasnot. Perestroika ina maana ya ujenzi mpya na Glasnot ni uwazi .

Kabla ya mageuzi hayo makubwa, Urusi ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kuwepo na fikra za ukale na kukosekana kwa uwazi. Jamii ilijawa hofu, mambo mengi yalikuwa ya kufichaficha. Kulikuwa na usiri mkubwa. Lakini, ndani ya kufichwa huko, kulikuwa na harufu ya uoza mkubwa. Gorbachev, daima atakumbukwa kwa ’ Kuvunja Ukimya’ na kuifanya Urusi kuwa nchi ya kisasa kama inavyoonekana sasa.

CCM ina cha kujifunza kutokana na yaliyotokea Urusi na yanayoendelea sasa katika nchi za Kiarabu na kwingineko. Ni ukweli, kuwa ndani ya CCM na hata Serikalini, kuna watendaji wenye kufanya kazi kama vile tuko kati kati ya miaka ya sabini. Halafu bado ndani ya CCM kuna wanaoshangaa kuona vijana wa leo wakikipa mgongo chama hicho.

Maana , imefika mahali, kuwa moja ya sifa ya kushiriki siasa ndani ya CCM
ni kuwa na uwezo wa ’ kuendekeza fitna na kusema uwongo!’ Na kwa wengine, uongozi ndani ya CCM unapatikana kama vile mtu anayekwenda kununua ng’ombe mnadani.

Na kuna kauli za Wana-CCM zenye kuthibitisha ukweli huu. Mojawapo ilipata kutolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Phillip Mangula aliyepata kutamka; ” Isifike mahala CCM ikatangaza tenda za uongozi!”.
Naam. CCM wanajivua gamba. Kila la kheir Chama Cha Mapinduzi.

‘MASANJA’, WALOKOLE WENZAKE WANUNUA SHANGA, VIDANI MORO

Masanja (wa pili kulia ngazi ya pili) akiwa na wanakwaya wenzake wakinunua shanga na vidani. MOROGORO
MSANII nyota wa kundi la vichekesho la shirika la utangazaji la TBC1 liitwalo Orijino Komedi, Emmanuel Mgaya 'Masanja Mkandamizaji', Jumatatu Pasaka ya Pili alinaswa na matandao huu akinunua shanga na vidani kwenye tamasha la uzinduzi wa albam ya video ya kwaya ya Agape uliofanyika ndani ya uwanja wa soka wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Mbali na kuigiza, Masanja ni mlokole anayesali katika kanisa la kilokole la EATG Mito ya Baraka la jijini Dar es Salaam ambapo msanii huyo ni miongoni mwa wanakwaya wa kanisa hilo inayojulikana kwa jina la Jerusalem.

Kwaya hiyoni miongoni mwa zilizoalikwa katika tamasha hilo. Masanja na wenzake wakiwa wanasubiri zamu yao ya kuimba waliutumia wakati huo kununua mapambo hayo.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliofurika kwenye uwanjani hapo walionekana kushangwazwa na kitendo cha walokole hao kununua vitu hivyo walivyoviita vya kishetani.

...manunuzi yakiendelea.


Masanja akiwa katika suti yake nadhifu uwanja wa Jamhuri.

KIKWETE, MAALIM SEIF WANG'ARA ZANZIBAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akisalimia wananchi wakati akiwasili na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davies Mwamunyange kwenye sherehe za Muungano za 47 zilizofanyika jana visiwani Zanzibar. Picha: Hisani ya Fredy Maro-Ikulu

MAMIA ya watu jana waliupamba Uwanja wa Amani, Zanzibar katika sherehe za maadhimisho ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Watu hao walionekana kuvutiwa zaidi na mgeni rasmi, Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.Umati huo wa watu, wengi wao wakiwa katika sare tofauti tofauti, ulilipuka shangwe za kelele na vifijo wakati viongozi hao wawili walipoingia kwenye uwanja huo kwa nyakati tofauti.

Rais Kikwete aliingia uwanjani hapo majira ya saa nne asubuhi akiwa kwenye gari la wazi na kuwapungia mkono mamia ya wananchi na baadaye kukagua gwaride.Baada ya hapo gwaride lilipita mbele ya Jukwaa Kuu kwa mwendo wa kasi na kisha mwendo wa pole.

Ulipowadia wakati wa halaiki iliyowashirikisha wanafunzi 500, mvua kubwa ilianza kunyesha na kuvuruga kabisa sherehe hizo.Kwa mujibu wa ratiba ya sherehe hizo, kipindi kilichokuwa kikifuatia ni ngoma za asili, lakini mvua ilipozidi washereheshaji walitangaza kukatisha na viongozi wakaanza kuondoka.

Kaulimbiu ya sherehe hiyo ilikuwa ni “Miaka 47 tuwaenzi waasisi wetu, tudumishe Muungano, matunda ya miaka 47 ya Mapinduzi na miaka 50 ya uhuru, amani, utulivu na maendeleo ni matokeo ya Muungano wetu."
Sherehe hizo zimefanyika huku kukiwa na kauli mbalimbali kutoka kwa wananchi na hata baadhi ya viongozi wa Zanzibar wakitaka Muungano huo ufanyiwe tathimini upya.

Viongozi wengine waliokuwapo katika sherehe hizo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Gharib Bilal, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wake wa Pili, Balozi Seif Idd.

Wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda; Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho; Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange; Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita wa SMZ, Dk Salim Amour.

Pia walikuwapo viongozi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Philip Mangula, Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi, James Mbatia na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao nchini.

Viongozi wengine wa kitaifa akiwamo Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim na Frederick Sumaye hawakuwapo katika sherehe hizo.

Jumuiya, taasisi za Kiislamu zatoa tamko
Katika hatua nyingine, Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar zimetoa tamko kuhusu hali ya Muungano zikisema umekosa kukubalika kwa Wazanzibari tangu siku yake ya kwanza hadi leo.

Huku wakitoa ushahidi wa tume kadhaa zilizoundwa ili kutafuta maoni ya wananchi kama vile Tume ya Jaji Nyalali na ile ya Jaji Kissanga, jumuiya hizo zimekilaumu CCM kwa kile walichokiita kuhodhi Muungano. Katika tamko hilo la pamoja, zimesema kuwa nguvu za Zanzibar ikiwa mshirika kamili wa Muungano huo hazipo.

“Kwa karibu miaka yote 47, Muungano huu umekuwa ni miliki ya chama kimoja cha siasa cha CCM, ukitoa miaka michache ya 1964-1977”.Jumuiya hizo zimetaka kuwapo kwa majadiliano ya Muungano zikitaka pia nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Muungano ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, irejeshwe.

“Mjadala wowote wa Muungano ule urudishe nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Muungano na siyo ilivyo hivi sasa... Rais wa Zanzibar hana maana wala amri yoyote ile katika Muungano,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

RAMSEY NOUAH AAGWA SAVANNAH LOUNGE LEO


Baadhi ya uongozi wa Paridise Hotel ukiwa kwenye picha ya pamoja na Ramsey Nouah na Kanumba.

Mameneja wa vitengo mbalimbali wa hoteli hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja na Ramsey Nouah.

Mwanamuziki wa Bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ ambaye kwa sasa anafanya vyema ndani ya tasnia ya filamu Bongo Patcho Mwamba (kulia), akiwa kwenye pozi na Ramsey Nouah.


Ramsey Nouah (kulia), akiteta jambo na Mkurugezi wa Paradise Hoteli.


Msanii wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ akiwa kwenye pozi na Patcho Mwamba.


Ramsey Nouah, akipozi na Lulu.


Msanii anayekuja kwa kasi katika tasnia ya filamu Bongo, Kajala Masanja, akiwa kwenye pozi na Ramsey Nouh.


Steven Kanumba, akipozi na Kajala.