Wiki hii namleta kwenu msanii anayefanya vizuri kupitia kiwanda cha filamu Bongo, Mohammed Mwikongi ‘Frank’. Kabla ya kwenda kwenye maswali niliyombana nayo kwanza tupate historia yake kwa ufupi.
Mshikaji alizaliwa miaka 31 iliyopita katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam na mwaka 1987 alijiunga katika shule ya msingi Mapambano na kuhitimu mwaka 1993. Frank alikuwa ‘kichwa’ flani kwani alifaulu na kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya Highlands Secondary School iliyopo mkoani Iringa na kuhitimu mwaka 1997. Mwaka 1998 alijiunga katika Sekondari ya Jitegemee jijini Dar es Salaam na kumaliza kidato cha sita kisha kujiunga na chuo cha habari cha DSJ ambapo alichukua Diploma ya Habari.
TQ: Dah! Kumbe wewe ni msomi? Enhee baada ya kuhitimu masomo yako ya uandishi wa habari, ilikuwaje sasa ukajikita katika masuala ya uigizaji wa filamu badala ya kuitumia taaluma yako?
Frank: Uigizaji ulikuwa katika damu yangu, niliipenda fani hii tangu nilipokuwa mdogo ndiyo maana hata nilipohitimu DSJ haikuwa kitu cha ajabu mimi kujiingiza kwenye uigizaji.
TQ:Unavyo vyeti vya uandishi wa habari, ulishwahi kufanya kazi sehemu yoyote kama mwandishi, mtangazaji au afisa uhusiano?
Frank: Nilishawahi kufanya kazi katika kituo cha Star TV kama ripota baada ya kuhitimu masomo yangu na baada ya hapo nilipata shavu Benchmark Production katika kipindi cha Wimbo.
TQ: Hivi unadhani filamu inalipa zaidi kuliko uandishi kiasi cha kuamua kuipa kisogo taaluma yako?
Frank: Awali nilibaini kwamba, nina ‘wake’ wawili yaani huku ni muandishi lakini pia ni muigizaji, hivyo nikaona siwezi kutumikia wake wawili kwa wakati mmoja,nikaona kwa kuwa naiweza vizuri sanaa bora niitumie hiyo katika kuyaendesha maisha yangu.
TQ:Unaweza kuimbuka filamu yako ya kwanza kuicheza na ikaingia mtaani? Ilipotoka ulijisikiaje?
Frank: Filamu yagu ya kwanza naikumbuka vizuri, ilikuwa inaitwa Chumba Namba 77. Filamu hii iliandaliwa na Christian Mhenga. Kusema kweli ilipotoka nilisikia furaha ya aina yake ambayo siwezi kuielezea kwa maneno.
TQ:Turudi kwenye maisha yako ya kimapenzi, umeoa wewe au bado uko singo?
Frank: Nimeoa ila kwa sasa siwezi kumzungumzia mke wangu kwa undani.
TQ:Vipi watoto, umejaaliwa kuwa nao?
Frank: Ninao watoto wawili ambao ni Tariq na Sharline, nawapenda sana wanangu.
TQ:Huko nyuma ulikuwa na urafiki wa karibu sana na viraka wa filamu nchini, Steven Kanumba na Vincent Kigosi ‘Ray’ lakini sasa hivi inadaiwa hampikwi chungu kimoja, habari hizi zina ukweli ndani yake?
Frank: In short, Ray na Kanumba ni wadogo zangu, nilibaini pia umri walionao huenda ulikua ukichangia katika yale waliyokuwa wanayafanya hivyo nikaamua kujiepusha nao, hata hivyo tulikaa tukasuluhishwa ingawa mapungufu huwa hayakosekani lakini kwasasa hamna shari.TQ: Imekuwa ikitokea sana kwamba, wasanii wenye rika kama lako kutafunwa na skendo za ngono zembe huku wakihusishwa na wasanii wao wa kike, kwako hili limekaaje?
Frank:Kwa upande wangu suala zima la ngono zembe huwa silipi nafasi na wala sijawahi kutumia jina langu kuchukulia mademu. Pamoja na hilo sikatai kama hakuna wenye tabia hiyo ila mara nyingi wenye tabia hiyo huwa hawadumu katika fani.
TQ: Ni akina nani hasa ndani ya sanaa ya uigizaji ambao hawaitendei haki fani?
Frank:Kaazi kweli kweli! Ok wasanii wa aina hiyo wapo tena wanafahamika na wengi wao ni maproducer. Mara nyingi huwa naona bora waachane na sanaa wachukue majembe wakalime kwani wanakoipeleka sanaa siko kabisa.
TQ:Ni mafanikio gani ambayo umeyapata tangu umeamua kujiingiza katika fani hii ya uigizaji?
Frank: Kwanza kuendelea kuwepo katika ‘game’ hadi leo ni mafanikio. Lakini pia ujue sanaa ndiyo inayoniweka hapa mjini. Hata hivyo natarajia mafanikio makubwa zaidi kwani miongoni mwa malengo yangu ni pamoja na kuwa Director wa Kimataifa na kwa hili nitarudi shule ili niweze kuendesha sanaa kisomi zaidi.
Ten question nitakuwa nawaletea kila siku ya Ijumaa, Endelea kucheki na mateja20 kila kukicha mambo mbalimbali yanapatika humu.