Na Walusanga Ndaki
NI dhahiri Watanzania wengi wanakumbuka jinsi suala la wabunge kulipwa posho lilivyopingwa na watu wengi, wakiwemo wabunge wenyewe, husuani kutoka vyama vya upinzani.
Hili lilotokea katika kikao cha bunge cha mwezi Septemba mwaka huu.
Sauti nyingi zilielezea kwamba haikuwa haki kwa wabunge kulipwa posho kwa kushiriki kazi ambazo ni sehemu ya majukumu yao wanayopaswa kuyafanya.
Kwa kifupi, wabunge waliokuwa wanaunga mkono hoja hiyo walitaka zifutwe kabisa badala yake zikatumike kwa miradi ya maendeleo wananchi.
Zaidi ya hapo, kiwango chenyewe cha posho ya sh. 70,000 kwa siku kilipigiwa kelele sana na wananchi kwamba ni kikubwa mno kwa mtu kujikimu kwa siku moja, na kwamba kiwango hicho kinapita mishahara ya mamilioni ya watu nchini ambao hufanya kazi za suluba.
Hata hivyo, suala hilo lilipita kimyakimya bila kupewa nadhari iliyotakiwa, kwani wabunge wengi hawakuliunga mkono.
Hivi majuzi, kiasi cha kama wiki mbili, gazeti moja la kila siku nchini liliandika habari kwamba serikali ilikuwa imepandisha kiwango cha posho za wabunge kwa asilimia 154 kutoka sh. 70,000 hadi 330,000 kwa siku.
Habari hizo zilipokelewa na wananchi kwa mshituko na wabunge kadhaa waliokuwa wakipinga ongezeko hilo. Hata hivyo, hilo likapita kimyakimya.
Baada ya kupita kama wiki nzima, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah akalikanusha hilo na akautangazia umma kwamba posho za wabunge zilikuwa hazikupanda!
Watanzania wakaendelea kushangaa, wasijue kwa nini habari hizo zilichukua muda mrefu kukanushwa.
Katika kuendelea kwa kioja hicho, siku chache baadaye, bosi wa Kashililah, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Makinda, jana (Jumanne) akatangaza kwamba posho za wabunge zimeongezwa kwa asilimia 185.7 ikiwa ni kutoka sh. 70,000 hadi 200,000 kwa siku.
Kituko kikubwa hapa ni kwamba watu waliotoa taarifa hizo za kupingana ni watu wa ofisi moja ambao ni mtu na bosi wake. Ilikuwaje kila mtu akatoa taarifa tofauti na ya mwenzake wakati suala hilo lilihusu ofisi yao, na walibidi walifahamu vyema?
Kioja hicho ni moja ya mambo lukuki ambayo hufanywa na watendaji wa ofisi za umma – tangu ngazi za chini hadi za juu – ambapo husababisha usumbufu mkubwa kwa umma, hususani pale uamuzi unapotakiwa kutolewa katika mambo muhimu.
Hali hiyo ambayo msingi wake ni uzembe na kutokuwa makini katika kutekeleza kazi za umma kila mara huleta madhara makubwa katika taasisi za umma kama vile katika hospitali mbalimbali, mahakamani, majeshi ya usalama hususan polisi, ofisi za umma, na kadhalika.
Tukio hilo la posho za wabunge ambalo wahusika walikuwa wanachukua muda mrefu kulikubali au kulikanusha haliwezi kuelezwa katika maneno mengine isipokuwa ni UZEMBE WA HALI YA JUU NA UKOSEFU WA NIDHAMU HATA KWA RAIS!
0 comments:
Post a Comment