Social Icons

Friday, August 12, 2011

EWURA YAIFUTIA LESENI KAMPUNI YA BP




TAARIFA KWA UMMA JUU YA KUSITISHA KWA LESENI YA BIASHARA YA JUMLA KWA KAMPUNI YA BP (T) LTD KWA MATUFA YA PETROLI, DIZELI NA TAA NA KUTOA ONYO KALI KWA KAMPUNI ZA ENGEN PETROLEUM (T) LTD, OILCOM (T) LTD NA CAMEL OIL (T) LTD

UTANGULIZI


ITAKUMBUKWA kwamba mnamo tarehe 22 Juni 2011 Serikali, kupitia kwa Waziri wa Fedha na Uchumi wakati akihitimisha Hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12, ilitoa maagizo kwa EWURA kuchukua hatua mbalimbali zitakazochangia kupunguza bei za mafuta kwa utaja maeneo mengi kama ifuatavyo (tunanukuu):



(a) Ukokotoaji wa thamani ya shilingi kwa kuioanisha na Dola ya Marekani (yaani Exchange rate);

(b) Kuondoa au kupunguza wigo wa asilimia 7.5 ambayo makampuni yaliruhusiwa kuwekwa ili kufidia baadhi ya gharama;

(c) kupitia upya misingi ya ukokotoaji wa viwango vya tozo mbalimbali za taasisi za Umma kwa lengo la kubakia na tozo stahili na kwa viwango stahili bila kuathiri majukumu ya udhibiti ma usimamizi yanayofanywa na Taasisi hizo;

(d) kupunguza tozo za kampuni za mafuta ikiwa ni pamoja na gharama za kibenki (yaani Financing Charges); na

(e) Upotevu wa mafuta yanayosafirishwa kwenye meli na gharama ya ukaguzi (yaani inspection fee).

(mwisho wa kunukuu).

Aidha, mnamo tarehe 4 Julai 2011, EWURA ilianza mchakato kwa kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuhusu mchakato wa kupunguza bei za mafuta. Pia EWURA iliandaa dokezo (discussuon paper) lililokuwa na vipengele mbalimbali ambavyo vitapunguzwa na kusambazwa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wauzaji wa mafuta hapa nchini.

Wadau mbalimbali walichangia dokezo hilo na kuwasilisha EWURA kwa maandishi na hatimaye mchakato wa utengenezaji wa Kanuni mpya ambayo imepunguza bei za mafuta ulihitimishwa kwa kuitisha Mkutano wa TAFTISHI uliofanyika Julai 22, 2011 katika Ukumbi wa Karimjee

USHIRIKISHAJI WADAU

Mchakato wa kupata maoni ya wadau (taftishi) ulianza tarehe 04 Julai 2011 na kukamilika tarehe 26 Julai 2011. Kwa kawaida, mchakato huu ungechukua siku 81 lakini kutokana na unyeti wa suala hili, Mamlaka ililazimika kuufupisha hadi siku 23. Wadau walioshirikishwa katika taftishi hiyo ni pamoja na kampuni za mafuta, Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na EWURA (Consumer Consultative Council), Baraza la Ushauri la Serikali, Taasisi za Umma kama vile TRA, TBS, WMA, TPDC, TPA, SUMATRA, na TIPER.



MATOKEO BAADA Maoni mbalimbali ya wadau yalipokelewa na kuchambuliwa na timu ya wataalam kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Uchumi, Shirika la Maendeleo ya Mfuta Tanzania (TPDC), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na EWURA na katika mfumo mzima wa kufanikisha utayarishaji wa kanuni hii mpya, wadau wote walifahamishwa katika mchakato huu kuwa bei mpya zitatolewa tarehe 1 Agosti 2011.

YA KUTANGAZ BEI MPYA

Baada ya kutangaza bei mpya zilizoanza Agosti 3, 2011 kampuni zilianza mgomo baridi wa kutouza mafuta kutoka kwenye magahala yake. Hata hivyo mgomo huo haukufahamika sana kutokana na kutokea wakati kukiwa na siku za mapumziko ya muda mrefu yaani taari 6 hadi tarehe 8 Agosti 2011.

Baada ya kugundua hilo, Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA ilikaa Agosti 9, 2011 na kutoa AGIZO LA KISHERIA (ORDER) kwa kampuni nne ambazo zilionekana ndizo kinara wa mgomo husika. Kampuni hizo ni BP (T) Ltd, Oilcom (T) Ltd, Camel Oit (T) Ltd na Engen Petroleum (T) ltd.

Agizo hilo la kisheria lilizitaka kampuni hizotajwa kutekeleza yafuatayo;

(a) Waanze kuuza mafuta mara moja baada ya kupata agizo la kisheria kutoka EWURA

(b) Waache mara moja vitendo vyovyote vinavyozuia uuzwaji wa mafuta

(c) Watoe maelezo kwa maandishi katika muda wa saa 24 kwa kuvunja Sheria ya Petroli ya mwaka 2008 kifungu 24 (1).

Baada ya agizo kutolewa tarehe 9 Agosti 2011, kesho yake kampuni zote zilianza kuuza mafuta kwenye maghala ambapo siku ya kwanza tarehe 10, Agosti 2011 ziliuzwa lita 8,535,700 kutoka kwenye maghala .

Hata hivyo, pamoja na kuuzwa kwa mafuta kwa wingi, bado BP (T) Ltd alionekana kukahidi amri halali ya EWURA kwa kuzingatia Sheria ya Petroli ya mwaka 2008, kifungu 24 (1) kwa kutouzaa mafuta kwenye vituo vyake vyote.

HATUA ZINAZOCHUKULIWA

Baada ya kuchambua kwa undani kuhusu suala hili, Bodi ya Wakurugenzi imekutana leo na kuamua yafuatayo:

a) Kuziandikia ONYO KALI kampuni za Oilcom (T) Ltd, Camel Oit (T) Ltd na Engen Petroleum (T) ltd kuwaonya kutorudia tabia walioionesha ambayo ni kinyume na Sheria za Tanzania na kuwaagiza wauze mafuta kwa watu wote bila ubaguzi. Amri hii itafuatiliwa kwa ujirani na ikibainika wamekiuka hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao mara moja

b) Kusitisha leseni ya biashara kwa BP (T) Ltd kwa MIEZI MITATU KUANZIA LEO kuuza mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa.

c) BP (T) Ltd ataruhusiwa kuendelea kuuza mafuta ya ndege kutokana na ukweli kwamba EWURA haidhibiti bei za mafuta ya ndege ambao ndio msingi wa mgomo kwa wafanyabiashara ya mafuta.

d) Pia BP (T) Ltd ataruhusiwa kuuza mafuta yake yote ya petroli, dizeli na taa yaliyopo kwenye maghala yake kwa wafanyabiashara wengine wa jumla kama wanataka kwa usimamizi wa EWURA ili kuzuia kutoharibika kwa mafuta hayo katika kipindi hicho cha miezi mitatu ambapo hataruhusiwa kufanya biashara ya mafuta ya jumla.

e) Hata hivyo, vituo vyote vya rejareja (Petrol Stations) vya vyenye nembo ya BP vitaruhusiwa kuuza mafuta kwa kununua mafuta kwa wafanyabiashara wengine wa jumla na si kwa BP.

f) Pia Bodi ya Wakurugenzi imeeagiza Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa BP (T) Ltd kufikishwa Mahakamani kwa kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Jinai (DPP).

USIMAMIZI WA MAFUTA

a) Kuanzia sasa EWURA itaendelea kuangalia mfumo mzima wa mafuta yanayoingia bandarini.

b) Pia EWURA itaendelea kufuatilia bei zinazouzwa kwenye vituo kama zinafanana na zile zilizotangazwa.

IMESAINIWA

Haruna Masebu

MKURUGENZI MKUU

MAMLAKA YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA MAJI NA NISHATI (EWURA)


0 comments: