Mkurugenzi wa Nyota na Mkuki Publishers na Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Vitabu nchini, Bw. Walter Bgoya (Kulia) akisisitiza jambo wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mafunzo kuhusu Utunzi na Usomaji wa vitabu kwenye Jukwaa la Sanaa
Na Mwandishi Wetu
Wasanii na waandishi wa habari wameaswa kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu ili kupanua uelewa wao na baadaye kuwaelimisha kwa ufasaha wasomaji na watazamaji wa kazi zao.
Wito huo umetolewa wiki hii na Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Vitabu nchini na Mkurugenzi wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya wakati akiwasilisha mada kuhusu Hali ya Uandishi na Uchapishaji wa Vitabu vya kiada na ziada vya sanaa nchini kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
“Kama wasanii na waandishi wa habari hawajengi utamaduni wa kujisomea kamwe hawawezi kuwa wasanii au waandishi wa habari wazuri. Hii ni sawa na ziro kabisa. Hakuna njia ya mkato katika kuwa msanii au mwandishi mzuri ni lazima kusoma na kujua mambo mengi.
Wewe utawezaje kumuelimisha mtu kama hujajua masuala mbalimbali yanayomuhusu? Lazima tufanye utafiti na kujisomea mambo mengi ili tujue nini tunawahabarisha na kuwaelimisha wasomaji na wasikilizaji wetu. Ndiyo maana tunasema kama hujafanya utafiti huna haki ya kuongea” Alisisitiza Bgoya ambaye alikiri kwamba watanzania wengi hawapendi kujisomea vitabu.
Alitoa ushauri kwa wasanii na waandishi wa habari kwamba, watenge muda wa kusoma vitabu na machapisho mbalimbali hasa wakihakikisha kila siku wanasoma kurasa kadhaa bila kukosa. Katika hili alisema kwamba, wataweza kujenga utamaduni wa kujisomea na kupata ufahamu wa mambo mbalimbali wanayoyawasilisha kwa jamii
“Mimi pamoja na kazi zangu huwa nasoma kwa wiki kitabu chenye kurasa mia ishirini hadi hamsini. Kwa mwaka naweza kusoma vitabu zaidi ya hamsini. Kazi zote za sanaa hata uchongaji huanza kwa maandishi kwa hiyo huwezi kuwa mwandishi au mwana sanaa mzuri kama husomi” Alizidi kuweka msisitizo.
Akifunga Jukwaa hilo la Sanaa, Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema kwamba, ni lazima waandishi wa habari na wasanii wajenge utamaduni wa kujisomea kwani huko ndiko kunakopatikana elimu na ufahamu wa mambo mbalimbali.
“Leo hii tumejionea hali ilivyo mbaya, kwamba watu hawasomi kabisa vitabu. Ni vema wasanii na waandishi wa habari tukajenga utamaduni wa kujisomea. Tumeambiwa pia tuonyeshe michezo ya majukwaani ili iweze kuandikwa sasa tuna wajibu wa kurudi kwenye sanaa za maonyesho” alimalizia Materego.
0 comments:
Post a Comment