Social Icons

Wednesday, May 18, 2011

SITTA: MIMI NI MTAJI WA URAIS


SIKU moja baada ya kurushiwa kombora la kutaka kukihama CCM na kuanzisha kilichokuwa Chama Cha Jamii (CCJ), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (pichani), amesema yeye ni mtaji wa kisiasa na ndiyo maana amekuwa akifuatwa na vyama mbalimbali vikimhitaji ajiunge navyo kuwania urais.

Akizungumza kwa simu jana, Waziri Sitta alisema si CCJ tu, bali alifuatwa na vyama vingine ambavyo kwa ukomavu wa kisiasa hawezi kuvitaja ambavyo baadhi, vilimtaka agombee nafasi hiyo ya urais mwaka jana.

Sitta alisema ni kawaida kwa mwanasiasa mwenye mvuto kufuatwa na vyama vingine vya siasa kwa ajili ya kujiunga navyo na kusema: "Sasa cha ajabu nini kwa CCJ? Mimi ni mtaji wa kisiasa bwana!"

"Katika demokrasia ya vyama vingi mazungumzo ya kisiasa ni kitu cha kawaida sana na hakuna cha ajabu hapo."

"Sasa kuanza kusema huyu fulani alikuwa hivi na mwingine vile kisiasa haipendezi, haya mazungumzo ya kisiasa yanaendelea kila siku hata sasa hivi unaweza kukuta wapo watu wanaendelea na mazungumzo. Sasa hii ya huyu bwana (Mpendazoe) inashangaza na kusikitisha."

Alifafanua kwamba mtu anapofanya mazungumzo ya kisiasa kama kutaka kujiunga na chama kingine na kisha akaghairi, anakuwa ameangalia mambo mengi ya msingi ikiwamo wakati na kuongeza kwamba mazungumzo ya kisiasa na kuanzisha chama ni vitu viwili tofauti.

"Ndiyo maana siwezi kusema kwamba siwezi kufikiria uamuzi huo au la. Haya ni mambo ya kisiasa unaangalia mambo mengi ya msingi, sitakiwi kujifunga kwamba siwezi kufanya hivi au la," alisema Sitta.

Akizungumzia uamuzi wa Mpendazoe kuamua kuwataja majina kwamba alishiriki katika kuanzisha CCJ, Sita alisema: "Huyu bwana amenishangaza sana. Nadhani amekasirishwa na sisi kukataa ushauri wake... Mwanasiasa makini hawezi kupata umaarufu kwa njia hii. Katika siasa watu hawasemi kama alivyosema."

Sitta alisema yeye ni mtaji wa kisiasa hata ndani ya CCM na anajivunia kwamba mabadiliko wanayotaka ndani ya chama hicho sasa yanawezekana.Aliwataka wanasiasa kujadili mambo ya msingi ya maendeleo kuliko kuanza kuzungumza mambo binafsi... "Kama ikiendelea hivyo, tunaweza kuumbuana sana."Alisema alijiunga na TANU Oktoba 3, 1960 hivyo uamuzi wowote wa kuhama CCM anapaswa kuufanya kwa umakini mkubwa.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCJ anena
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCJ, Renatus Muabhi ameelezea kushangazwa kwake na hatua ya Mpendazoe kuibuka na hoja hiyo sasa wakati chama chenyewe kimeshakufa.
Mbali ya Muabhi, mwanasheria maarufu nchini na kada mwandamizi wa NCCR Mageuzi, Dk Sengondo Mvungi naye ameibeza hoja hiyo ya kada huyo wa zamani wa CCM.

Muabhi alisema jambo la CCJ sasa hivi halipo kwani chama chenyewe kimekufa na kuhoji mantiki ya kuanzisha hoja hiyo katika kipindi hiki huku akisisitiza kamwe hawezi kuanza kuibuka na kuzungumzia kitu kisichokuwapo... "Hicho chama chenyewe hakipo, sasa kuanza kuzungumzia CCJ maana yake nini?

Dk Mvungi na Katiba CCJ
Dk Mvungi ambaye amekuwa akidaiwa kuwa ndiye aliyeandika katiba ya CCJ, alisema kamwe hajawahi kupewa kazi hiyo huku akisisitiza: "Loh! Kama ningepewa kazi hiyo si ningefurahi. Si unajua sisi Watanzania mtu akifanya kitu anaanza kutangaza ni mimi ndiyo nimefanya."

Dk Mvungi alisema kamwe hakuwahi kuandika katiba hiyo ya CCJ huku naye akisisitiza: "Lakini, hivi kweli ni hoja kwa sasa kujadili CCJ ambayo imekufa? Tunapaswa kuangalia mambo ya msingi ya sasa, si yasiyokuwepo," Alisema Watanzania wanapaswa kuangalia jinsi CCM kinavyobomoka sasa hivi na si kuangalia kipindi hicho cha CCJ ambacho chama hicho tawala kiliweza kujipanga na kunusurika na mpasuko huo.

"Sasa hivi CCM ndiyo inabomoka. Hapa ndipo Watanzania walipaswa kupaangalia lakini kuanza kusema huyu alikuwa CCJ, chama chenyewe hakipo, kweli hilo ni jambo la msingi kulizungumzia?" Alihoji Dk Mvungi.

Alisema sasa hivi Rais Jakaya Kikwete, ametangaza chama kujivua gamba kitu ambacho alisema Watanzania wanapaswa kuonyesha mshikamano kwa kuhakikisha kinafanikiwa ili kuona watu wasio na madili wanang'oka.

Nape: Nendeni kwa Msajili
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa CCM, Nape Nnauye amewaambia wale wanaotaka kujua waanzilishi wa CCJ waende Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ana rekodi zote.

Juzi, katika mkutano wake alioufanya Njombe, Mpendazoe aliwataja Sitta, Nnauye na makada wengine wa CCM kwamba walikuwa waanzilishi wa CCJ lakini waliwasaliti Watanzania ili wapate vyeo ndani ya Serikali ya Rais Kikwete.

0 comments: