Catherine akikabidhi msaada wa kompyuta kwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Arusha, Nembris Kimberly.
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Arusha, Catherine Valentine Magige, amefanya kufuru ‘baabkubwa’ kwa kumwaga misaada na kujitolea shughuli za kijamii.
Catherine aliyeingia mjengoni kupitia ‘mlango’ wa vijana (UVCCM), aliitumia wikiendi iliyopita kufanya mambo makubwa sita, ikiwemo kuwasaidia wagonjwa na kushiriki kufanya usafi kwenye Hospitali ya Mt. Meru.
Mbunge huyo kijana, pia aliumwagia misaada Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Arusha kisha alikwenda kumhani Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Arusha, Thomas Laizer ambaye alifiwa na mama yake mzazi mwezi uliopita.
RATIBA ILIKUWA HIVI
Jumamosi alikwenda kumtembelea Askofu Laizer nyumbani kwake na kumpa pole.
Jumapili, alikwenda Hospitali ya Mt. Meru ambako alishiriki kufanya usafi wa mazingira kama vile kufyeka nyasi na kufagia.
Akiwa hospitalini hapo, Catherine aliwatembelea wazazi na watoto wao kisha akamsaidia kila mama pea ya khanga, mche wa sabuni na mafuta. Jumla ya wagonjwa 125 walinufaika.
Siku hiyo hiyo, aliikabidhi ofisi ya UWT Arusha msaada wa kompyuta, skana, printa na USB.
Leo (Jumatatu), Catherine ana ziara ya kuwatembelea wafungwa waliopo gerezani Arusha na kuwapa misaada mbalimbali.
Catherine, anaitumia siku ya leo kuwatembelea watoto waliobakwa pamoja na mwanamke aliyezaa watoto wengi kimiujiza bila kukutana na mwanaume mkoani Arusha na kutoa misaada kwa wote.
Mwenyekiti wa UWT Arusha, Nembris Kimberly alisema kuwa Catherine ni mfano wa kuigwa kwa sababu tangu awe mbunge amekuwa akionesha namna ambavyo kiongozi anaweza kuwa karibu na jamii kwa vitendo.
Catherine alisema, ataendelea kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii yenye kuhitaji msaada kwa sababu ni wito aliokuwanao hata kabla ya kuwa mbunge.
Catherine (mwenye fyekeo) akishiriki kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Mt. Meru.
...akiwa amembeba mtoto hospitalini hapo.
....akitoa msaada wa khanga kwa wagonjwa.
....akina mama waliolazwa hospitalini hapo wakimsubiri mbunge huyo.
...akiwa na Askofu Laizer nyumbani kwake alipokwenda kumpa pole.
0 comments:
Post a Comment