Social Icons

Saturday, April 23, 2011

SHELA NUKSI



Baadhi ya mastaa wa kike Bongo (majina tunayo) wameibuka na kudai kuwa, watakuwa wanagoma kuigiza nafasi ya kuvaa shela na kufunga ndoa baada ya kubaini kuwa, wenzao wengi waliovaa vazi hilo wamepatwa na nuksi kwani hawajaolewa mpaka sasa.

Wakiongea kwa nyakati tofauti mastaa hao, kila mmoja alizungumzia jinsi anavyolichukulia vazi hilo, na wengine wakakiri kuwa, hata wale waliokwishavaa zamani wanalikimbia kwa kuwa linawasotesha tu.

Mastaa hao waliwatolea mfano wenzao, Jennifer Raymond Mau ‘Penina’, Lucy Francis Komba ‘Lona’, Blandina William Chagula ‘Johari’, Riyama Ali, Ummy Wenslaus ‘Dokii’ kwamba, walivaa shela kwenye filamu ndiyo maana hakuna aliyeolewa.

Aidha, walidai kuwa, umri wa mastaa hao umegota miaka 30 au kukaribia, wakisema; Johari ana 29, Lucy Komba 30, Penina 28, Dokii 31, Riyama 28.

Wakasema kuwa, kwa msichana akifikisha miaka 25 hajaolewa ni tatizo.
Risasi liliwasaka mastaa hao waliodaiwa kuingiwa na nuski na wengine, ili kusikia ya mioyoni mwao.
Staa wa kwanza kufunguka kuhusu nuksi ya kuigiza na shela ni Johari ambaye alikiri.

“Mimi naona ni kweli haya mashela yanatia nuksi, nimecheza filamu nyingi za kuolewa, ikiwemo ya Johari nikayavaa. Lakini nahisi nitaishia kuyavaa haya ya kuigizia tu, yale yenyewe hakuna,” alisema Johari.

Kwa upande wake, Riyama aliyevaa shela kwenye filamu ya Best Wife alisema kuwa, anaona hakuna shida kuvaa vazi hilo. Akasema haamini kwamba, anapochelewa kuolewa ni kwa sababu ya nuksi ya kuvaa shela wakati wa kuigiza filamu.

“Siku zote kuolewa ni majaliwa na pia inawezekana kabisa mtu hajaamua kwa sababu bado anachagua na unajua mchagua, huchaguliwa. Tuwe wavumilivu tu,” alisemaRiyama.


Msanii mwingine ambaye hakukumbwa na tuhuma lakini aliongea na Risasi ni Shamsa Ford ambaye alivaa kwenye filamu ya Saturday Night, ana haya ya kusema:
“Mimi nafikiri ni bahati ya mtu tu, kwa sababu nimeigiza nimevaa shela, lakini tayari nina mchumba ambaye yuko tayari kwa ndoa, ila mimi sijaamua.”

Akafuatia Rose Ndauka ambaye alivaa kwenye filamu ya More Than Pain: “Kwa kweli imani hiyo mimi sina, ninachojua ipo siku itafika, Mwenyezi Mungu atapanga, nitaolewa na kuvaa kabisa lile lenyewe.”


Dokii kwenye filamu ya Scandalm anasema: “Ninachojua mimi ni kwamba, muda ukifika nitapata mume, hiyo dhana wanayosema wenzangu sikubaliani nayo hata kidogo.”
Aunt Ezekiel kwenye Young Billioners, anafunguka: “Mimi sijalitilia maanani sana, mwenyewe nimecheza filamu nyingi nikiwa nimevaa shela la harusi, lakini sina mpango wa kuolewa, ndiyo maana sina uhakika kama shela zinatia nuksi au lah.”

Penina kwenye filamu ya Penina, ana haya: “Kwani kuolewa si uamuzi wa mtu? Kwanza mnajuaje kama nina mume au sina? Shela ni shela tu, liwe la harusi ya kweli au la kwenye filamu.”



Lucy Komba yeye alivaa kwenye filamu ya My Love, akajitetea: “Mh! Hao waliosema hivyo ni washirikina. Wana imani za kishirikina ndiyo maana wanaamini ukivaa shela la filamu hutakuja kuolewa, si kweli bwana.”

0 comments: