Social Icons

Monday, April 25, 2011

PASAKA: MAASKOFU WASISITIZA VITA DHIDI YA UFISADI

VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini wamesisitiza umuhimu wa kulinda amani, kupambana na ufisadi na umakini katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.Walisema hayo jana wakati wa Sikukuu ya Pasaka ikiwa ni kuadhimisha kufufuka kwa Yesu Kristo yaoata miaka 2,000 iliyopita.

Askofu Mtenji: Tubadili mwelekeo wa rushwa, ufisadi
Akihubiri katika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi Mjini, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Ulanga Kilombero, Renard Mtenji aliwataka waumini kusimama kidete kubadili mwelekeo wa rushwa, ufisadi na maovu mengine katika jamii.

“Mambo ya rushwa na ufisadi sasa yanasikika kila kona nchini... wenye pesa wakati wote ndiyo wenye haki na wenye uhakika wa kuishi. Kundi hili lina uwezo mkubwa wa kununua haki…haya si maisha yanayompendeza Mungu,” alisema.

Askofu Mtenji alisema jamii ya Watanzania sasa inashuhudia mambo mengi ya ajabu ukiwamo ukatili wa kutisha akitolea mfano mauaji ya vikongwe na albino.

“Ukatili wa aina mbalimbali unaendelea kutendeka katika jamii yetu… watoto wadogo wanabakwa kwa sababu ya ushirikina… hivi sasa inakuwa ni jambo la kawaida kabisa mama kumnyonga mtoto wake wa kumzaa,” alisema.

Askofu Libena: Tuna matatizo ya tamaa, wizi, kujilimbikizia mali...
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Saltarius Libena aliwataka Wakristo na jamii nchini kujihoji kama wao sehemu ya matatizo ya taifa na kuchukua hatua kubadili maisha yao na ya nchi kwa kuacha kuwa sehemu ya matatizo hayo. Aliyataja matatizo hayo kuwa ni tamaa, wizi, ubinafsi wa kujilimbikizia mali, kujikweza, ulevi na ukorofi.

Askofu Libena alisema hayo alipokuwa akihubiri katika Ibada ya Misa Takatifu ya mkesha wa Pasaka katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jimboni humo.

"...Katika nchi yetu kuna matatizo mengi yanasemwa hata kuandikwa na magazeti na redioni, wewe nami si sehemu ya matatizo hayo? Wizi, ukorofi, hali ya kutaka sifa za ajabu ajabu, utajiri sana kujisifia na kujikweza?" alihoji Askofu Libena na kuongeza:

"Watu siku hizi wanatafuta vitu vya kujinufaisha binafsi. Tunaandamana na mambo makubwa makubwa yasiyompendeza Mungu. Wewe nami hatumo humo?."

Askofu Adam: Katiba si mali ya vyama vya siasa
Askofu Marko Adam wa KKKT, mkoani Mara amewataka wananchi kutambua kuwa Katiba si ya vyama vya siasa, bali ni ya Watanzania wenyewe hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuijadili kwa maslahi ya taifa na vizazi vijavyo.

Akihubiri katika Kanisa la Karanga, Soweto, Moshi, Askofu Adam alisema kila Mtanzania analo jukumu la kujadili katiba na siyo kusubiri ijadiliwe na wengine na baadaye kuanza kulalamika kutoshirikishwa.

“Tumepungukiwa kitu kimoja. Tunaposhirikishwa jambo tunapuuza na kila mmoja kuona yuko 'bize' na mambo yake lakini tuko mstari wa mbele kulalamika kuwa hatukushirikishwa. Hebu tubadilike na tuone hili kama jambo linalotuhusu kuliko mambo yote,” alisema.

Askofu Mokiwa: Amani haiko mbali kuvurugwa
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana, Dk Valentino Mokiwa alisema amani ya nchi haiko mbali kuvurugwa kutokana na kuporomoka kwa maadili, ugumu wa maisha na malumbano yanayoendelea kwa viongozi wa nchi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Dk Mokiwa alisema kuchafuana kunakozidi kuongezeka ni ashirio baya kama Watanzania hawataendelea kuzungumza ukweli.

"...Tunazungumzia wakati mwingine kwamba kichwa cha binadamu kinaweza kikasongwa na kitu kinachoitwa msongo wa mawazo. Sasa hivi tunaona ongezeko la kiwango cha msongo wa mawazo kwa kiwango cha kitaifa. Hakuna kusemana vizuri kila mmoja ni mtu anayejua kusema na anasema vibaya dhidi ya mwenzake," alisema.

Alisema neno demokrasia nchini limeendelea kuchukua sura tofauti na maana yake asilia inaanza kutoweka: "Sasa demokrasia si demokrasia baadhi yetu tunaamini kuwa ni domokrasia."

"Hivi karibuni tumeliona bunge letu kwa masikitiko makubwa sana. Wabunge kwa mara ya kwanza tumeshuhudia wakizomeana, wakisemana vibaya, uvunjivu wa maadili kutokuheshimiana katika kiwango kinachoanzia bungeni! Nje ya Bunge yatatokea mabaya zaidi," alisema na kuongeza:

"Tunaposherehekea Pasaka mwaka huu, tunaposherehekea ufufuko, kila mtu atazingatia umuhimu wa amani kupenda amani kukwepa mambo yaletayo vurugu na tuzingatie. Viongozi waongoze, wanaoongozwa watulie ili kusudi nchi yetu iweze kwenda mbele," alisema.

Askofu Mhogolo: CCM kiache ubabe
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati, Godfrey Mhogolo alisema vurugu na vita zilizotawala katika baadhi ya nchi za Afrika zikiwamo, Libya na Ivory Coast ni dalili tosha na fundisho la kung'ang'ania amani iliyopo nchini.

Akihubiri katika Kanisa Kuu la Kianglikana Mjini Dodoma, Askofu Mhogolo alisema misuguano ya vurugu hizo ni dalili ya wananchi kutaka haki na uhuru wao kujitawala upya, hivyo yapaswa wasikilizwe.

Alisema mfano wa Libya umedhihirisha kuacha kuchezea kisiwa cha amani na upendo kilichopo hapa nchini na kusema mabadiliko ya kujivua gamba kwa chama tawala CCM kulenge kutibu majeraha ya migogoro iliyojitokeza ili kutoiingiza nchi kwenye machafuko.

Alisema muda umefika kwa CCM kuacha ubabe na badala yake kitambue uwepo wa vyama vingi vinavyoleta demokrasia ya kweli ya watu kufanya uamuzi wanaoona kuwa ni sahihi.

Aliwataka viongozi walioko madarakani kufanya maridhiano yanayopigania amani na haki na kuacha hofu au woga wa kusikiliza, kutatua au kujibu vilio na madai ya wananchi kama Katiba na uhuru wa mahakama.

Askofu Mkude: Serikali isitafute umaarufu kwa Babu
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphory Mkude aliitaka Serikali isitumie kikombe cha Babu (Mchungaji Ambilikile Mwasapila wa KKKT anayetoa tiba ya magonjwa sugu huko Samunge, Loliondo) kama mtaji wa kisiasa.

Askofu Mkude alisema dawa inayotumiwa na Mchugaji huyo aina ya mrigariga imekuwepo kwa miaka mingi ikitumiwa na jamii mbalimbali ikiwa ni pamoja na jamii ya Wasonjo na baadhi ya jamii huko Kenya na hata kufikia kuwapatia Shahada ya Uzamivu (PhD) kwa baadhi ya watafiti.

“Wakristo na wote wenye mapenzi mema tunaisihi Serikali na wadau wote wa afya kudhamiria kuboresha huduma za afya, bila shaka wanaokimbilia kikombe ni kutokana usumbufu katika hospitali zetu. Kwa mfano, msururu wa wagonjwa na maswali mengi, uduni wa huduma za x-ray, tiba ya sindano za vipindi, kuambiwa warudi kesho na hatimaye hakuna dawa,” alisema.

Askofu Kakobe apunguza idadi ya ibada
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF, Zachary Kakobe amepunguza idadi ya ibada katika kanisa lake huku akiwataka waumini wake kutokunywa dawa kutafuta tiba ya mwili na badala yake watafute tiba ya roho.

Alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia mbinguni kwa jina la uchungaji ikiwa hana tiba ya roho huku akisema kuwa kwa sasa kanisani kwake kutakuwa na ibada moja tu badala ya mbili kama ilivyokuwa awali.

Alisema muda wa ibada ya kwanza waumini wake watakuwa wanasoma mafundisho tu badala ya kusali kama ilivyokuwa kawaida.

Akiendelea kuzungumzia dawa, Askofu Kakobe alisema hakuna mtu yeyote aliyeokolewa kwa kunywa dawa na kuwataka watafute tiba ya kiroho ambayo itawafikisha mbinguni.

“Hata ukitafuta tiba ya mwili ukapona bado utakufa tu, lakini kama ukitafuta tiba ya roho utakuwa umejiwekea hazina mbinguni na ukifa utaona ufalme wa Mungu, damu yake Yesu ndiyo itasafisha moyo wako leo na kuacha dhambi,” alisema.

Alisema wapo watu mashuhuri, wanasiasa na waliokuwa na vyeo ambao wamekufa na makaburi yao yanaonekana hadi leo lakini hawajafufuka kama Yesu.

“Utaingiaje mbinguni wakati unapougua unatafuta msaada kwa mashetani? Hayo mashetani ndiyo yalishindwa kumzuia Yesu asifufuke na wewe unataka uponyaji kwao?”

Askofu Msonganzira:Malumbano ndani ya CCM yanachefua


Askofu wa Jimbo la Katoliki Musoma, Mhashamu Michael Msonganzira amesema malumbano yanayoendelea ndani ya CCM yanachefua na kuonyesha kuwa vijana hawawaheshimu wazee.

Akihubiri katika Parokia ya Mugumu, Serengeti alisema vijana wamefikia hatua ya kukimbia kasi na kuwaacha wazee wakisahau kuwa nafasi ya wazee iko palepale akisema mtoto ni mtoto kwa wazazi wake, hivyo wanatakiwa kutambua na kuwaheshimu wazee.

“Ninyi ni mashahidi, malumbano yaliyodumu kwa muda kwenye vyombo vya habari vijana wanawashambulia wazee hadharani bila kutambua kuwa wao bado ni watoto tu kwa wazazi wao,” alisema na kuongeza:

“Tunatambua vijana wana nguvu na kasi ya kukimbia lakini hatuna utamaduni wa kuwadharau na kuwatukana wazee, yakianza kutokea hayo lazima kutakuwa na matatizo, hata kama wamekosea hatuna utamaduni wa kuwatukana hadharani.”


Askofu Mdegella azungumzia hatua ya CCM kujivua gamba

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Owdenberg Mdegella ametafsiri neno ‘kujivua gamba’ ambalo limekuwa likitumiwa na CCM kwamba kisayansi linamaanisha hatua ya nyoka kupata madhara ya kiafya baada ya kupita katika vumbi na kuziba masikio yake.

Akihubiri katika Kanisa Kuu la Mjini Iringa, Mdegella alisema nyoka hutegemea ngozi yake kama masikio katika ulinzi wake na mapito yake ndiyo maana anapopata madhara hutafuta njia ya kujiokoa huku nia kuu ikiwa kujivua gamba.

Alisema kisayansi nyoka husikia kwa kutumia ngozi yake na mara anapopita katika vumbi, masikio yake huziba ndiyo maana hukimbilia kuvua gamba lake ili aweze kupata kusikia kwa usikivu.

“Siku hizi kuna huu msemo wa kujivua gamba, niwaambie tafsiri yake, kisayansi ni kwamba asili yake ni nyoka. Kiumbe huyu hujivua gamba baada ya kupita katika vumbi na masikio yake kuziba ndiyo maana hufikia uamuzi wa kujivua ili apate kusikia.”

0 comments: