
Lile bifu la ‘mayanki’ wawili wa muziki wa Kizazi Kipya, Naseeb Abdul ‘Diamond’ na Rahim Rummy Nanji ‘Bob Junior’, linazidi kuumuka ambapo wameponea chupuchupu kutwangana.
Tukio la wawili hao kutaka kutoana manundu lilijiri ndani ya Ukumbi wa New Maisha Masaki, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii.
Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na mapaparazi wetu, Bob Junior, Top C wa Sharobaro kwa kolabo na msanii wa Kundi la Dar Stamina, Nurdin Bilal ‘Sheta’, walikuwa wakiangusha bonge la shoo ‘kiwanjani’ hapo.
Katika hali ya kushangaza, ghafla ukumbini humo hali ilichafuka ambapo walizama ‘masela’ ambao kazi yao ilikuwa ni kumzomea Bob Junior katika kila kitu alichofanya.
Nyuma ya zomea zomea hiyo kuliibuka madai mazito kuwa, watu hao ambao walifika kiwanjani hapo wakiwa wamejaa kwenye gari aina Toyota Coaster walikodiwa na Diamond huko Kariakoo ili kuja kumpotezea Bob Junior.
Baadaye Bob Junior alishuka stejini na kukatiza jirani na Diamond aliyekuwa ameegemea kwenye ukuta ukumbini humo ambapo kwa mujibu wa watu waliokuwa jirani walisikika wakibadilishana lugha ya matusi ya nguoni na vitisho vya kufa mtu.
Achilia mbali matusi waliyokuwa wakiporomosheana mithili ya mvua zinazonyesha nchini kote, Diamond aliamua kumfuata Bob Junior ‘toileti’ ili wakatwangane kumaliza ubishi unaoendelea kati yao.
Kama siyo kaka wa Bob Junior ambaye jina lake halikupatikana, leo kungekuwa na stori nyingine mbaya zaidi kama siyo maombolezo ya vifo kwani alifanya kazi ya ziada kuwazuia kutoana macho.
Habari zinadai kwamba Bifu la Diamond na Bob Junior linazidi kuumuka kila kukicha kwa kujumuisha watu wengine zaidi.

Ukiachia mbali Wema Abraham Sepetu aliyewekwa chini ya ulinzi na ‘wajeda’ wa Oysterbay wiki iliyopita kwa ishu hiyo, naye msanii Sheta anatajwa kwenye bifu hilo kufuatia kuwa kwenye ‘kampani’ ya Wasafi ambayo Diamond ndiye rais wao ikielezwa kuwa ni hasimu wa ile ya Sharobaro iliyo chini ya Bob Junior.
Bifu la Diamond na Bob Junior (wakati huo akiwa prodyuza) lilianza miezi kadhaa iliyopita baada ya rais huyo wa Wasafi kumtuhumu mwenzake kuwa alikataa kumrekodia kibao chake kipya cha Gongo la Mboto akisingizia kuumwa sikio.
0 comments:
Post a Comment