Social Icons

Wednesday, March 23, 2011

TAMKO LA JUKWAA LA KATIBA KWA UMMA

Wakati Vuguvugu la kuanza mchakato wa kuandaa Katiba mpya Tanzania likiendelea kushika kasi, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tumewasilisha serikalini mapendekezo ya awali ya Mambo yanayotakiwa kuzingatiwa katika muswaada wa kuweka utaratibu utakaofuatwa tangu kuanza hadi mchakato wa kupata Katiba mpya Tanzania.

Mapendekezo hayo ambayo yamewasilishwa kwa katika ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na nakala kwa ofisi zote husika katika mchakato huu, yameweka bayana hatua, vyombo, majukumu, usimamizi na uwezeshaji wa mchakato mzima wa uandaaji wa Katiba Mpya Tanzania, hatua kwa hatua.

Aidha, mapendekezo ya JUKWAA yameweka bayana namna ambavyo Wananchi wataweza kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kuandaa Katiba mpya ili kuepuka dhana kuwa suala la kuandika Katiba ni la Wanasheria, tena wanasheria waliosomea na kubobea katika sheria za masuala ya Katiba pekee.

JUKWAA limependekeza utaratibu utakaowezesha wananchi wote, ikiwa ni pamoja na wale wasiojua kusoma wala kuandika na wanajamii mbalimbali mijini na vijijini watakavyowezeshwa kuweza kushiriki katika kuweka misingi ya uandikaji Katiba, kutoa maoni katika mijadala ya awali na kwa Tume ya kuratibu maoni, pamoja na kuchagua wawakilishi kutoka miongoni mwao kushiriki katika vyombo muhimu vya kujadili mapendekezo na rasimu za Katiba ikiwemo wajumbe wa Mkutano wa Kitaifa wa Katiba (National Constitutional Conference) na Bunge Maalum la Katiba (Constituent Assembly).

Pia, kuna mapendekezo juu ya vyombo muhimu vya kusimamia hatua zote muhimu katika mchakato huu wa kuandika katiba itakayokuwa muafaka halisi waWatanzania wote bila kujali hali, vipato, Jinsia, wala rangi zao.

Katika kufanya mapendekezo ya vyombo, JUKWAA limetambua imani iliyopo katika baadhi ya vyombo muhimu vilivyopo kuweza kusimamia michakato yote ya uandishi wa Katiba. Kwa sababu hiyo, JUKWAA limependekeza majukumu kadhaa kwa Bunge la Tanzania ikiwemo kupitisha muswaada wa Sheria ya Utaratibu utakaofuatwa kuandaa hadi kupata Katiba Mpya ya Tanzania.

Aidha, Bunge la Tanzania limepewa mamlaka ya kidhinisha vyombo na watendaji wake wote watakaopatikana kwa kuteuliwa na Rais kama vile Tume ya Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba na watendaji wake wote.

Pia, Bunge la Tanzania limepewa mamlaka ya kuendelea kufuatilia kwa karibu mchakato wote wa uandikaji wa Katiba kuona kuwa unakwenda kulingana na sheria ya Bunge itakayowekwa mwezi ujao, na kuhakikisha kuwa hakuna kulegalega wala kukwama kwa mchakato huu wa Kuandaa Katiba ya Nchi yetu.

Zaidi, tumependekeza namna ya kuwezesha na kufadhili utendaji wa vyombo katika hatua za Mchakato. Kunapendekezwa kuanzishwe mfuko maalum wa KATIBA Tanzania ambao utatumika kufadhili na kuwezesha utekelezaji wa majukumu yote rasmi ya uandaaji na uandikaji wa Katiba nchini kuanzia ngazi ya kufanya mijadala, utendaji wa Tume ya Katiba, hadi kura ya Maamuzi itakayokuwa hatua ya mwisho kwa wananchi kukubali au kuikataa rasimu ya mwisho ya Katiba ya Katiba ya Tanzania.

Mapendekezo yetu yameonesha jinsi mfuko huu utakavyotunishwa na kwamba hakutakuwa na matumizi yoyote kutoka katika mfuko huu isipokuwa kwa shughuli zinazohusu mchakato wa uandishi wa Katiba.

Katika yote hayo, na kutokana na unyeti wa Mchakato huu unaoanza wa uandika Katiba ya Tanzania, kunapendekezwa pia vyombo vipya vya kusimamia hatua za baadaye za mchakato huu. Hii ni pamoja na Tume Maalum ya Muda ya Uchaguzi (Interim Independent Electoral Commission) itakayopewa Jukumu la kusimamia Kura ya Maamuzi ya Katiba (referendum).

Chombo hiki pia kitashirikiana na Tume ya sasa ya uchaguzi kuhakiki daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo ndio litakalotumika kuongoza kura zozote zitakazohitajika kupigwa wakati wa mchakato huu wa uandikaji na upitishaji wa Katiba.

Mapendekezo ya JUKWAA pia yamezingatia uzoefu wa nchi yetu na zile za Jirani katika kuendesha michakato ya Upatikanaji wa Katiba Mpya. Tumejifunza kutoka katika Michakato yetu wenyewe ya kujaribu kuandaa Katiba Mpya ya Tanzania siku za nyuma.

Ingawa hakuna jaribio lililowahi kufaulu kuandika Katiba Mpya Tanzania, yapo mafunzo mengi tunayoyapata kutoka katika vyombo, ushiriki wa Wananchi, usimamizi na uratibu maoni wa michakato hiyo. Aidha, tumejifunza mengi pia kutoka katika michakato ya miaka ya karibuni ya uandishi wa Katiba katika nchi za South Africa (1996), Uganda (1995), Katiba ya Jamhuri ya Kenya (2010) na Mchakato uliojaribiwa wa Kuandika Katiba Zimbabwe (2001).

Kwa kuzingatia haja ya kuendesha mchakato huu kwa umakini na weledi wa hali ya juu, na kwa kuzingatia kuwa kumekuwa na madai ya haja ya kuwa na Katiba mpya kufikia uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa hali ya sasa si nzuri Kikatiba, JUKWAA limependekeza kuwa muda wa kuandika Katiba uwe ni kuanzia sasa (2011) hadi mwaka 2014 ili kuruhusu muda wa kuweza kuweza kuweka vyombo vya utekelezaji wa Katiba mpya kabla ya 2015.

Kwa jinsi Tanzania ilivyo na mazingira bora zaidi ya kiutendaji na kwa kuwa sisi sote tutakuwa bega kwa bega kusaidia mchakato huu usirudi nyuma wala kusuasua, haya yote yanawezekana ifikapo 2014. Serikali inapewa jukumu la awali la kuhakikisha kuwa rasilimali na fedha zinazohitajika kwa mchakato huu zinapatikana kwa wakati muafaka.

Sisi JUKWAA LA KATIBA TANZANIA ambalo ni jumuiko la wanajamii linaloratibiwa na Asasi za kiraia zipatazo 30 tutaendelea kuwa na majukumu ya kuwezesha uelewa na ushiriki wa wananchi katika mchakato mzima wa kuandaa Katiba hadi nchi ipate Katiba Mpya. Majukumu yetu katika kila hatua yameoneshwa katika kiambatisho cha TAMKO hili.

Tunatoa tamko hili ili kuufahamisha umma wa Tanzania juu ya hatua iliyofikiwa katika kuendelea na Mchakato wa kuanza Kuandaa na Kuandika Katiba Mpya ya Tanzania.

0 comments: