Social Icons

Wednesday, March 23, 2011

SUGU AKABIDHI RAMBIRAMBI


Mh. Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akikabidhi rambirambi zake kwa Mkurugenzi wa Kundi la Five Stars Modern Taarab, Ferouz Juma huku Katibu wa Kamati ya Mazishi, Asha Baraka akishuhudia.
MBUNGE wa jimbo la Mbeya Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ‘Chadema’ Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ leo Jumatano ametoa mchango wa shilingi laki tatu (300,000) kwa kamati ya mazishi ya wanamuziki 13 wa Five Stars Modern Taarab waliofariki dunia juzi kwa ajali ya gari iliyotokea Mikumi mkoani Morogoro.

Akikabidhi mchango huo kwa katibu wa kamati hiyo Asha Baraka, Sugu alisema akiwa kama waziri kivuli wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, ameguswa sana na msiba huo.

“Kwa niaba yangu mwenyewe na chama changu tumepokea kwa uchungu na majonzi makubwa msiba huu. Taifa limepoteza wasanii wa kikundi cha Five Stars Modern Taarab, ni huzuni kubwa kwangu binafsi kama mmoja wa wasanii hapa nchini. Nawaomba ndugu, marafiki pamoja na mashabiki wa muziki huu wa taarabu wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki cha huzuni kubwa,” alisema Sugu.

Naye katibu wa kamati hiyo ya mazishi amemshukuru Sugu kwa moyo wake huo na kumsihi aendelee hivyo hivyo kwani ingawa ni Mbunge lakini bado ni msanii katika tasnia ya muziki nchini.

Wakati huo huo, Asha Baraka alisema tayari kamati yake imeshapokea michango kutoka kwa Ofisi ya Meya wa Manispaa ya Temeke ambayo imetoa shilingi milioni moja na laki tatu (1,300,000), Redio ya Clouds Fm ambayo imetoa milioni moja (1,000,000) na Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi ‘UWT’ shilingi laki tano.

Michango mingine imetoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Idd Azzan shilingi laki nne na hamsini elfu (450,000), Mh. Juma Kapuya shilingi laki moja (100,000), Bendi ya Fm Academia laki mbili (200,000), Akudo Sound shilingi elfu hamsini (50,000), Bendi ya African Stars International ‘Twanga Pepeta’ laki mbili (200,000) na watu waliochangia kupitia M-pesa hadi mwandishi wetu anaondoka eneo la tukio, walikuwa wametoa shilingi laki tatu na tisini na tatu elfu (393,000).

Asha alisema kamati inatarajiwa kukabidhi michango hiyo kwa wahusika kesho Alhamisi saa 2 asubuhi.



Katibu wa Kamati ya Mazishi akipokea mchango kutoka kwa Meya wa Manispaa ya Temeke, Mabadi Hoja.

0 comments: