Rais Jakaya Kikwete.
RAIS Jakaya Kikwete jana alilihutubia taifa, huku akitumia muda mwingi kujibu mapigo ya kauli za Chadema dhidi yake na kutahadharisha kuwa chama hicho, kina lengo la kuleta machafuko nchini. "Kauli na vitendo vya wenzetu hao vyenye dhamira ya kutaka kuleta machafuko makubwa na uvunjifu wa amani nchini." alisema Rais Kikwete ambaye amekuwa kimya bila kulihutubia taifa kwa muda wa miezi miwili.
Onyo la Rais Kikwete limekuja siku chache baada ya Chadema kumpa siku tisa ikitaka mkuu huyo wa nchi atekeleze baadhi ya mambo ikiwamo kutoilipa fidia ya Sh 94 bilioni kampuni ya Dowans.
Lakini, jana katika hotuba yake, Rais Kikwete pamoja na kufafanua hoja kadhaa, alisisitiza "Hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa."
Rais Kikwete alifafanua kwamba, hivi karibuni wananchi wengi wameingiwa na hofu kubwa kuhusu usalama wa nchi yao hali ambayo ni ngeni kwa Watanzania.
"Hofu hiyo inatokana na kauli na vitendo vya wenzetu wa Chadema vyenye dhamira ya kutaka kuleta machafuko makubwa na uvunjifu wa amani nchini," alieleza Rais Kikwete.
Mkuu huyo wa nchi ambaye tayari amemaliza siku 100 za ngwe yake ya pili akiwa Ikulu, aliweka bayana kuwa kufanya maandamano na mikutano ni haki ya msingi ya vyama vya siasa na raia, lakini, akaonya kuigeuza fursa hiyo kuwa jukwaa la kuchochea ghasia kwa nia ya kuindoa Serikali iliyoko madarakani kwa mabavu.
Kikwete alisisitiza kuwa hatua hiyo ni matumizi mabaya ya fursa ya kufanya maandamano na isiyostahili kuungwa mkono na Watanzania wazalendo, wapenda amani na nchi yao.
Rais alisema Tanzani ni nchi ya kidemokrasia na kila miaka mitano hufanyika uchaguzi wa kuchagua viongozi na kuweka bayana.
"Uchaguzi wa mwisho tumefanya tarehe 31 Oktoba, 2010. Kabla ya hapo tulikuwa na kampeni zilizochukua karibu miezi mwili na nusu. "
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, katika kampeni hizo, kila chama kilielezea jinsi kitakavyokabiliana na matatizo yanayowakabili wananchi ikiwa ni pamoja na hayo yanayoyazungumzwa sasa na Chadema.
"Hatimaye siku ya uchaguzi wananchi walifanya uamuzi wa kuchagua chama walichokiamini, nacho ni Chama cha Mapinduzi.,"alieleza
"Iweje leo, miezi mitatu baadaye kwa mtu au chama cha siasa kufanya maandamano kwa masuala yale yale waliyoyasema kwenye kampeni. Siyo sawa hata kidogo," alisema Rais Kikwete.
"Kuchochea ghasia ati kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima. Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi,"alionya Rais Kikwete.
Kikwete alisema katika nchi ya kidemokrasia na kwa wanademokrasia wa kweli, wanapomaliza uchaguzi mmoja, hujiandaa kwa uchaguzi mwingine kwa kujenga upya chama , kuongeza wanachama, kuboresha sera na hoja pamoja na namna ya kuziwasilisha ili watu wawakubali na kuwachagua.
Rais Kikwete aliitaka Chadema kutumia Bunge kuwasilisha hoja zao badala ya mikutano ya hadhara inayotoa kauli za chuki kwa Serikali.
"Na, uwanja muhimu wa kufanya sehemu kubwa ya hayo ni katika Bunge na Halmashauri za Wilaya kupitia wabunge na madiwani wenu,"alieleza Rais Kikwete
Kikwete ambaye mara ya mwisho alitoa hotuba ya mwezi wakati wa mwaka mpya wa 2011, alisema kuacha kufanya hivyo na badala yake kuamua kuzunguka nchi nzima na kuchochea ghasia kwa lengo la kuwaondoa walioshinda ni kinyume na misingi ya demokrasia na kusisitiza
Alisisitiza "Tutajenga misingi ya hovyo na nchi yetu itakosa amani na utulivu daima."
Aliwataka Chadema kukaa chini na kujiuliza wanachokifanya na athari zake kwa wananchi akisema, "kama kila atakayeshindwa uchaguzi anafanya hivyo tutakuwa nchi ya namna gani?"
"Tanzania yetu hii yenye sifa na heshima ya kuwa nchi ya amani na utulivu itapoteza kabisa sifa hiyo na badala yake umwagaji wa damu na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia vitageuka kuwa maisha ya kawaida." alisema.
Rais alisema kitendo hicho haikiitendei haki nchi na hata wananchi ambao viongozi wa siasa wamekuwa wakidai kuwapenda na kuwatetea.
"Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu; ndugu zetu wa Chadema wanayajua yote haya, lakini wanalo lao jambo. Wanataka kuipeleka nchi yetu pabaya kwa kukidhi uchu wao wa madaraka. Kwao sasa demokrasia haina maana, inaweza kusubiri," alifafanua Rais.
Aliwataka Watanzania kuwa makini na Chadema akisema "naomba tuyakatae mambo yao. Tusiwafuate. Waambieni mchezo wao ni hatari na ni mauti yetu. Sisi katika Serikali tutajitahidi kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa nchi yetu, watu wake na mali zao."
Hali ngumu ya maisha
Rais alikiri, "Ni kweli kuna hali ngumu ya maisha, na kukabiliana nayo ndiyo kazi tunayoendelea nayo kufanya kila siku."
"Tumeelekeza nguvu zetu na rasilimali zetu huko na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali, lakini akisisitiza, "hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa."
Alifafanua kwamba, kikwazo siyo upungufu wa sera wala dhamira, bali ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wa nchi na hivyo uwezo siyo mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo ingepaswa iwe.
Kikwete akirejea zama mbali za viongozi mbalimbali tangu uhuru, alisema hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii.
"Na wale wa umri wangu au kunizidi wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang’atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri. Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, Mzee Mkapa nae kakaa miaka 10 hakuyamaliza. Mie nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano hayataisha yote." alisema
Alisema jambo la muhimu ni kuwa katika kila awamu nchi iweke malengo ya kupiga hatua ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo na kuongeza, hali iliyokuwa wakati ule sivyo ilivyokuwa mwaka 1985, wala 1995 au 2005 na ilivyo sasa.
Kuhusu mafanikio yake alisema, "Katika miaka mitano hii kuna maendeleo yanayoonekana wazi, pamoja na changamoto nyingi tumefanya juhudi kubwa na mafanikio yanaonekana katika nyanja zote za maisha ya Watanzania. Mwenye macho haambiwi tazama.''
Rais alirejea matukio mbalimbali yanayoitikisa dunia, akisema ni muhimu watu kutambua ukweli kwamba uchumi kama wetu ambao haujajenga uwezo wake wa ndani wa kujitosheleza kwa mahitaji yake, huathirika sana na yanayotokea katika uchumi wa dunia.
"Unapoyumba na sisi tunayumba. Bei za mafuta katika soko la dunia zikipanda na kwetu kupitia gharama za uchukuzi na uzalishaji huongezeka na kusababisha bei za bidhaa kupanda," alifafanua Rais akitaka wananchi wafahamu jinsi athari za dunia zinavyoweza kugusa uchumi wa nchi.
Mfumuko wa bei ukipanda China, nguo na bidhaa tunazonunua kutoka China hupanda bei. Hivi sasa mataifa yote makubwa tunakonunua bidhaa mfumuko wa bei umepanda na sisi tunaathirika.
Alihoji, "mvua ikikosekana kunakuwa na uhaba wa chakula, bei za vyakula hupanda na watu wengine hukosa chakula. Lawama kwa Serikali au Rais Kikwete inaanzia wapi?
Hali ya Umeme
Rais alikiri pia hali ya upatikanaji wa umeme nchini kwamba ni mbaya na kuweka bayana, "chanzo cha matatizo ni kupungua sana kwa maji katika bwawa kubwa la Mtera.
"Hadi jana kina cha bwawa hilo kimeshuka hadi kufikia mita 691.25 ambacho ni pungufu kwa mita 7. Kwa sasa zimebaki mita 1.25 tu juu ya kiwango cha chini kinachoruhusiwa kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme,"alisema.
Hata hivyo, alisema 15 Februari, 2011, Baraza la Mawaziri lilijadili na kuidhinisha mpango wa dharura wa Tanesco wa kukodi mitambo ya kuzalisha MW 260 za umeme na kuongeza, baraza limeitaka bodi na menejimenti ya shirika hilo kuhakikisha mchakato huo unakamilika mapema iwezekanavyo ili kupunguza makali na athari za ukosefu mkubwa wa umeme kwa jamii na uchumi wa nchi.
Akionekana kukwepa jinamizi la Richmond aliyowahi kuita kuwa ni 'Phantom,' Rais alisema, ilisisitizwa pamoja na udharura uliokuwepo sheria na taratibu za manunuzi ya umma vizingatiwe kwa kuhakikisha mkataba utakaoingiwa uwe ni wenye maslahi kwa taifa na watoa huduma wawe ni makampuni yanayofahamika na yenye sifa stahiki na kuaminika.
Milipuko ya Gongo la Mboto
Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, alitangaza kwamba Serikali itawalipa fidia waathirika wa mambomu yao na kwamba Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA -JKT) limepewa wajibu wa kujenga upya nyumba zilizobomolewa na mabomu hayo.
Rais alifafanua, "Nimeagiza Jeshi la Kujenga Taifa lifanye kazi hiyo kupitia Shirika lake la Uchumi. Nimeamua hivyo ili kuhakikisha kuwa maisha ya ndugu zetu waliokumbwa na maafa haya yanarejea kuwa ya kawaida mapema iwezekanavyo."
Aliongeza kwamba, ameagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ishirikiane na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Kitengo cha Taifa cha Maafa kuhakikisha kuwa utekelezaji unaanza mapema iwezekanavyo.
Hali ya chakula
Akizungumzia tatizo hilo Rais alisema, katika baadhi ya maeneo nchini kumeanza kujitokeza matatizo ya upungufu wa chakula kuanzia mwezi Januari 2011 na kuongeza, mengi ya maeneo hayo ni yale yanayopata mvua za vuli ambazo bahati mbaya hazikuwa nzuri.
"Imetambuliwa katika Halmashauri 36 za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Mara, Tabora, Singida, Dodoma, Lindi, Mtwara na Iringa ndiko kwenye maeneo mengi yenye upungufu mkubwa, " alisema Rais.
Hata hivyo, alisema tayari serikali imeidhinisha kutolewa kwa jumla ya tani 13,760 za chakula kutoka Akiba ya Taifa ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kuhudumia watu 423,530 walioathiriwa na upungufu wa chakula katika maeneo hayo huku kazi ya usambazaji ikiendelea.
" Hadi sasa jumla ya tani 4,822 za chakula cha msaada kimekwishatolewa katika mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Lindi. Napenda kuwathibitishia kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa. Tutawahudumia ipasavyo hawa waliokwishatambulika na wengineo watakaojitokeza siku za usoni," alifafanua.
Mbowe amjibu
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake hakitaacha maandamano licha ya kushutumiwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wanachochea vurugu katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi.
Mbowe ambaye alikuwa akihutubia katika Uwanja wa Josho Mjini Shinyanga, alisema kuwa ameamua kuijibu mapema ili kueleza msimamo wa chama chake kuwa hawataacha maandamano hata wakikamatwa na kuwekwa ndani.
“Kikwete leo atahutubia taifa na kusema maandamano yetu yanachochea vurugu, namjibu kuwa tutaandamana na tutaendelea kuandamana. Tunaandamana kwa sababu hatutaki Dowans ailipe kama ambavyo yeye na Kamati Kuu ya chama chake wameamua kuilipa kwa fedha za walipa kodi,” alieleza.
Alisema Rais Kikwete anazungumzia bei ya sukari wakati akijua fika kuwa tatizo ambalo limesababisha kupanda kwa bei ya sukari na kuyafanya maisha ya Watanzania kuwa magumu ni sera mbovu za chama chake na kushindwa kwa utawala wake.
“Kikwete anazungumzia mgao wa umeme, taifa gani limekaa na mgao wa umeme kwa miaka saba na halitatuliwi. Halafu anataka tuheshimu Serikali, tusiandamane, tutaendelea kuandamana na tutaandamana,” alisema Mbowe.
Alisema katika hotuba yake ya mwezi amezungumzia juu ya Serikali yake kununua mitambo mingine ya kufua umeme kwa kutumia kiasi cha Sh 400 milioni fedha za walipa kodi wakati la Dowans halijaisha.
“Haki ya Mungu tutaendela kuandamana na kama anatuona sisi ni wachochezi basi anikamate Mbowe na wengine anaowaona wachochezi na akatushitaki,leo tunaandamana Shinyanga na kurudi makwetu kwa amani,lakini kuna siku tutaandamana na hatutarudi ila sijui tutakwenda wapi kama hapa Shinyanga tutaenda kwa mkuu wa mkoa sijui…” alieleza Mbowe.
CHANZO: MWANANCHI MACHI 1, 2011
0 comments:
Post a Comment