Social Icons

Wednesday, February 9, 2011

POLISI IRINGA WADAIWA KUMPIGA RISASI RAIA

Majeruhi akiwa katika kochi nyumbani kwake.
Waandishi wa habari wakimhoji mwanamke huyo majeruhi
Hapa akiwa na watoto wake wawili ambao wanamuunguza mwenye nguo ya jano ndiye aliyeshuhudia mpango mzima.


POLISI Iringa watuhumiwa kutenda unyama baada ya askari kanzu wa kike wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, kudaiwa kumtwanga risasi mguuni katika mazingira ya kutatanisha,mfanyabiashara ndogo ndogo Frida Mgima (33) akiwa anateremka katika gari dogo la kukodi (taksi) nje ya baa moja maarufu mjini hapa.


Tukio hilo la kinyama lilitokea Februari 4 mwaka huu mjini hapa majira ya saa 11 za jioni baada ya mfanyabiashara huyo kushuka katika gari hilo aina ya Ballon lenye namba T 450 AEA akiwa na lengo la kwenda kununua chips katika baa hiyo na kurejea nyumbani.


Akizungumzia tukio hilo nyumbani kwake maeneo ya Don Bosco mjini Iringa, alisema amekuwa akiuguza jeraha hilo baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Frida alisema kuwa hakujua alipigwa risasi hiyo na askari huyo kwa lengo gani.

Alisema muda mfupi baada ya tukio hilo alifuatwa na kusindikizwa na askari waliokuwa doria karibu na baa hiyo na kwenda kituo kikuu cha Polisi Wilaya ya Iringa kupewa kibali cha kupata matibabu (PF3).

Alisema baada ya kufika kituoni na kupewa PF3 alikwenda kutibiwa katika Hospitali ya mkoa wa Iringa ingawa wakati wa tukio hilo hakuelezwa na mtuhumiwa huyo (askari kanzu wa kike) alipigwa risasi hiyo kwa kosa gani.

Katika tukio hilo, mfanyabiashara huyo akiwa na mwanae wa miaka tisa (9) anayeitwa Miki, anadai kwamba alipoteza fedha za makusanyo ya biashara zake kiasi cha sh. 500,000 pamoja na simu ya mkononi.

“Nikitwa katika gwaride la utambulisho nitawaonyesha, yule askari ni wa upelelezi mimi namjua,alikuwa amevaa koti na amebeba redio call ya Polisi, alinitwanga shaba mguu wa kushoto lakini namshukuru Mungu hakuniua nimepona…sijui nimefanyiwa hivi kwa kosa gani”,alihoji mwanamke huyo huku akiangua kilio.

Hata hivyo,Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa Evarist Mangala alipotafutwa na mtandao huu
kuzungumzia sakata zima, alisema kuwa hana taarifa na tukio hilo na kwamba askari wa kike hawaruhusiwi kubeba silaha.

“Nimewasiliana na OCD wangu tukio kama hilo halipo na halina ukweli wowote…askari wa kike hawaruhusiwi kubeba silaha,huyo aliyemuona alipata wapi hiyo silaha anayosema…ndugu yangu hakuna ukweli katika tukio hilo”,alisema Kamanda Mangala.


Huku uongozi wa Hospitali ya mkoa wa Iringa kupitia mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Oscar Gabone ukikanusha kumruhusu mgonjwa huyo kabla ya kupo japo umekiri kumpokea mgonjwa huyo.

Picha: Francis Godwin Iringa.

0 comments: