Social Icons

Thursday, February 10, 2011

MKUU WA WILAYA AKATAZA KITI MOTO KUUZWA BAR

Shekh Kairo mwenye kanzu akizungumza.

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Said Mwambungu, ametoa amri kuzuia kuuzwa kwa nyama ya nguruwe (kitimoto) kwa muda katika baa ya mkazi mmoja inayojulikana kama Baa ya Kimario iliyopo mtaa wa Makaburi (B) Kata ya Mji Mpya mjini hapa kufuatia wananchi wa dini zingine wanaoishi katika mtaa huo kulalamika kwa mkuu huyo kwamba moshi mzito wa kitimoto unaotoka katika jiko la baa hiyo iliyopo jirani na makazi yao ni kero.

Mwambungu alitoa amri hiyo leo mchana katika mkutano wa kujadili suala hilo uliofanyika katika mtaa huo ambapo baada ya kusikiliza maelezo kutoka pande zote tatu yaani upande wa walalamikaji, walalamikiwa na upande wa serikali ya mtaa, mkuu huyo wa wilaya alitoa amri hiyo.

Kwa upande wao, Waislamu wanaoishi katika mtaa huo walidai kwamba jiko la baa hiyo liko jirani na makazi yao na kwamba moshi mzito unaotoka katika jiko hilo hupenya hadi kwenye nyumba zao na kwamba wamebaini leseni aliyopewa mmiliki wa baa hiyo, Bw. Kimario, ni ya kuuza vinywaji na si kuuza nyama ya nguruwe.

Akijibu hoja hiyo, Kimario alisema majirani zake wamemzulia uongo kwamba anauza nyama mchanganyiko ikiwemo ya ng'ombe, kuku na nguruwe.

“Hapa nauza nyama ya nguruwe tu na jiko langu nimelitengeneza kitaalam ambapo moshi unaenda juu na hauendi kwenye makazi ya jirani," alisema Kimario.

Vilevile, Afisa Biashara wa Manispaa, Ernest Makundi na Kaimu Afisa Afya wa Manispaa, Martin Mzuwanda, walisema kwamba kabla ya kutoa leseni kwa muombaji, alipewa masharti na manispaa ambayo Kimario aliyatimiza.

Maofisa hao walisema leseni aliyopewa ni ya vinywaji ambayo inamruhusu pia kuuza nyama choma ambayo inaweza kuwa ni nyama ya ng'ombe, mbuzi, kuku na nguruwe.

Diwani wa kata ya Mji Mpya, Wencelaus Kalogeres, alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema limekuzwa bure na kwamba lingeweza kupewa ufumbuzi na wananchi wa mtaani hapo bila ya upendeleo.

Kabla ya kutoa maamuzi hayo, mkuu huyo wilaya alimpa nafasi Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mohamed Kairo, ambaye alisema kitendo cha moshi wa nyama ya nguruwe kuwafikia watu jirani ni sawa na kuwalisha nyama hiyo kwa nguvu, kama vile mvuta sigara anavyovutishwa sigara kwa nguvu kwa kufikwa na moshi wa mvuta sigara.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, mkuu huyo wa wilaya alisema: "Kuanzia sasa nasimamisha kwa muda uuzaji wa nyama ya nguruwe kwenye baa ya Kimario lakini uuzaji wa vinywaji na biashara nyingine viendelee."

Mkuu huyo wa wilaya alifikia uamuzi wa kufanya mkutano baada ya kupokea barua kali kutoka kwa waislamu iliyotishia kuchoma moto nyumba hiyo inayouza kitimoto.

Pia kwa siku tatu sasa swala hilo limekuwa likizungumzwa katika mkutano wa hadhara wa dini hiyo unaoendele katika viwanja wa shule ya Msingi Mwembesongo iliyopo jirani na kata hiyo ya Mji Mpya.

Hata hivyo baada ya mkuu huyo wa wilaya kutoa maamuzi hayo mtaando huu ulishuhudia baadhi ya watu wengine hasa wa dini ya kikristo kutolidhishwa na maamuzi hayo .


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Said Mwambungu akizungumza katika mkutano huo.

Mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Ustadh Juma Mbega, ambaye alitishiwa kuuawa na Waislamu wenzake kwa kile walichodai kwamba ameegemea upande wa Kimario (mwenye barghashia) akizungumza katika mkutano huo kuwaomba radhi Waislamu wenzake.

Kimario (mwenye kipara) akizungumza katika mkutano huo.

Mmoja wa wakazi wa mtaa huo anayeishi jirani na baa hiyo, Mohamed Mzee (mwenye shati jeusi), akitoa malalamiko yake.

0 comments: