Social Icons

Wednesday, February 2, 2011

' KAMSEMO KA' LEO BAANA!'

Ndugu Zangu,
”UNAPOTAKA kusema, tumia yako hekima. Neno liwe la heshima. ”- Remmy Ongala.
Naam. ’Chumvi ’. Nataka kusema kuhusu chumvi. Chumvi ni maisha, chumvi ni siasa. Kwa wengine wataona ni kitu kigogo sana. Hapana, chumvi ni kitu kikubwa. Sukari na utamu wake hauzidi utamu wa chumvi. Kwanini? Maisha yaso chumvi si maisha. Ndio, maana, Serikali zote Afrika huheshimu bei za chumvi. Ukimwona raia wa nchi anaanza kulalamikia bei ya chumvi, basi, hizo si ishara njema.
Mwanadamu waweza kuwa na kila kitu nyumbani. Lakini, ukikosa chumvi nyumbani , basi, huna kitu! Chumvi ni mwandani pia, au?
Haya, umenunua nyama, vitunguu, nyanya na vingine. Jikoni unakaangiza. Kumbe! Unakumbuka, kuwa umesahau. Nyumbani huna chumvi. La haula! Giza limeshaingia, utakitafuta hata kibanda cha masikini, ukaombe chum… Shii! Usiku kuna mwiko wa chumvi. Usiku usiseme chumvi, sema ’ dawa ya mboga’. Na unajua maana yake? Wazee wetu walikuwa na busara sana. Aliyesahau kuwa na chumvi nyumbani alikumbushwa kwa kupewa ’ tabu kidogo’ katika kuipata. Maana, chumvi ni muhimu nyumbani.
Ndio, chumvi ndio dawa ya mboga. Nyama ulokaangiza haiwezi lika bila chumvi ati! Kama kuna ’ nyama ya ulimi’, basi , chumvi ndio ’ asali ya ulimi’. Na chumvi ina kawaida yake. Ikiharibika ndo basi tena, ni ya kutupwa hiyo. Chumvi haioshwi.
Na mwanadamu chunga ulimi wako. Neno lako ni chumvi. Fikiri kwanza kisha ulitamke, usitamke kisha ukafikiri. Neno baya ni sawa na chumvi iliyoharibika. Haiosheki, ikasafishika, na ikabaki kuwa chumvi.
Na mwanadamu akisemwa amekula chumvi nyingi ina maana ameishi miaka mingi. Amefaidi maisha. Binadamu aweza kupitisha siku bila kula chenye sukari. Lakini, hakuna siku ipitayo kwa mwanadamu bila mdomoni mwake kumeza kitu chenye chumvi. Na kama si chakula, basi mate, yana chumvi! Na nikisema chumvi ni tamu kuliko sukari nani abishaye?
Mh! Chumvi! Na hilo ni Neno La Leo.

0 comments: