Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Adolphina Chialo, akizungumzia tukio hilo.
MWANAFUNZI wa darasa la sita wa shule ya msingi ya Ipopoo, kijiji cha Miembeni, Tarafa ya Mlimba, Wilayani Kilombero, aliyetambulika kwa jina la Hapa Kasenga (12) amefariki dunia na watu wengine wanane wamelazwa katika kituo cha afya cha Mlimba baada ya kula mzoga wa kondoo unaosadikiwa kuwa na sumu.
Akizungumzia tukio hilo lililotokea Februari 4 majira ya jioni, Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro, Adolphina Chialo,alisema waliolazwa kituo cha afya cha Mlimba kwa ajili ya matibabu wakiwemo watu wazima ni: Kikwete Kitewi (6) Boly Balabit (50), Emmanuel (11).
Wengine ni Maria Kimasai, (20), John Girigida (42), Veronica Zakayo (6), Godfrey Kapital na Lesso John (10) wote wakiwa ni wafugaji wa jamii ya Kimang’ati na wakazi wa Ipopoo.
Chialo alisema uchunguzi wa polisi kuhusu suala hilo unaendelea wakati waathirika wakipatiwa matibabu.
Pia alitoa rai hasa kwa jamii za wafugaji kuacha tabia ya kula mizoga ili kuepuka hatari ya vifo ama madhara ya kiafya.
Aliwataka pia wananchi kuacha tabia ya kununua nyama kutoka kwa wafugaji kabla ya kupimwa au kuchinjwa kitaalam.
0 comments:
Post a Comment