Social Icons

Tuesday, January 4, 2011

WIKILEAKS: MTANDAO KIBOKO CHA WAFANYA MAOVU DUNIANI


Kauli mbiu yake: Tunazifungua serikali zionekane kwa walimwengu
KISHINDO halisi cha mtandao wa WikiLeaks ambacho ni chombo cha kufichua maovu na siri zinazohusu matukio mbalimbali duniani, kilisikika hapa nchini kiasi cha wiki kadhaa zilizopita baada ya kufichuka kwa mazungumzo yaliyomhusisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hoseah, na ofisa mmoja wa kidiplomasia wa Marekani, Purnell Delly, jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Julai 2007, mkuu huyo wa kupambana na rushwa nchini alidai kwamba alikuwa na uwezo wa kuwashitaki watu wote waliohusika na manunuzi “mabaya” ya radar kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza.

Hata hivyo, kwa mujibu wa WikiLeaks, jambo hilo Hosea alishindwa kulifanya kwa madai kwamba wahusika hao walikuwa wanakingiwa kifua na nguvu “fulani” kubwa nchini.

Wakati ishu hiyo haijapoa, Wikileaks wametoa taarifa nyingine tena ikidai kuwepo kwa mazingira ya rushwa katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika mpango wake wa kununua ndege mpya. Magazeti ya The Guardian na Daily News ya leo nchini Tanzania yameripoti ishu hiyo.

Hivi ndivyo Watanzania wengi walivyokuja kuifahamu au kuitilia maanani WikiLeaks, licha ya kuanza kuisikia “kwa mbali” kwa muda kadhaa na hata kuipuuza kwa kubeba masuala ambayo wengi walihisi yalikuwa hayawahusu.

Hata hivyo, ni dhahiri watu wengi wangependa kufahamu WikiLeaks ni nini na ni nani kwa jumla?

WikiLeaks ni taasisi ya kimataifa ambayo haina lengo lolote la kujipatia faida yoyote kwa njia ya biashara, ni taasisi ambayo huchapisha hati na kauli mbalimbali za watu na siri mbalimbali kutoka kwa watu, serikali na vyanzo mbalimbali.

Mtandao wake ulizinduliwa mwaka 2006 ukiwa unamilikiwa na The Sunshine Press, ukidaiwa kuwa na hati milioni 1.2 kwa ajili ya kazi zake wakati huo.

Inadai waaasisi wake ni raia wa China wasiokubaliana na sera za nchi yao (waasi), wakiwemo pia waandishi wa habari, wanahisabati, na wataalam wa teknolojia mbalimbali kutoka Marekani, Taiwan, Australia na Afrika Kusini.

Julian Assange, raia wa Australia, mtaalam na mwanaharakati wa masuala ya Internet, huelezewa kuwa ndiye mkurugenzi wa taasisi hiyo.

Mnamo Aprili 2010, WikiLeaks ilitoa video kuhusu tukio la mwaka 2007 ambalo raia na waandishi wa Iraq waliuawa na majeshi ya Marekani. Video hiyo imepewa jina la Collateral Murder na inaendedelea kuoneshwa katika mtandao wa CollateralMurder.Com (bonyeza link kujionea)

Mwaka huohuo mwezi Julai, WikiLeaks ilitoa mfululizo wa matukio ya Vita vya Afghanistan ambao ulijumuisha hati 76,900 kuhusu “Vita vya Afghanistan”, yakiwemo mambo ambayo yalikuwa hayajaonekana wala kufahamika.

Vilevile, Oktoba mwaka jana, ilitoa hati 400,000 kuhusiana na vita vinavyoendelea huko Iraq ambapo vyombo vikuu vya habari vilihusika katika kufichua matukio hayo. Na Novemba mwaka jana, WikiLeaks ilianza kufichua hati na habari mbalimbali za kibalozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

KWA NINI WIKILEAKS 'HAIKAMATIKI'?

Uwepo wa mtandao 'hatar'i kama huu, mtu unaweza kujiuliza kwa nini usifutwe tu au kufungiwa kama ilivyokuwa kwa ZEUTAMU hapa nchini? Jibu la swali hilo ni kwamba mtandao huu haufungiki na wala haukamatiki kutokana na utaalamu wa hali ya juu uliotumika katika kuunda na kuuendesha.

Katika hali ya kawaida, ungetegemea Wikileaks ipatikane katika web site rasmi na moja ambayo ni WWW.WIKILEAKS.COM. Lakini ukifungua mtandao huo kwa anuania hiyo, utakutana na ujumbe usemao: SORRY! THIS SITE IS CURRENTLY NOT AVAILABLE. Kwa ujumbe huo bila shaka utaamini wikileaks haipo tena hewani.

WAKO MATAWI YA JUU, HAWASHIKIKI

Ili kuthibitisha kuwa mtandao huu umetengenezwa katika mfumo wa kitaalamu zaidi, Wikileaks inaendelea kupatikana hewani na itaendelea kuwepo siku zote kwa sababu uko 'matawi ya juu'. Mtandao huu umetengenezwa kwa staili ya MIRRORS na CABLEGATES kibao. Hadi kufikia Desemba 21 mwaka jana, kulikuwa na anauani (Mirrors & CableGates)) 1,426 ambazo zinawasilisha Wikileaks. Hii ina maana kwamba ukifungua anuani yoyote kati ya hizo, itakupeleka kwenye mtandao uleule wa Wikileaks.

Baadhi ya anuani hizo ni kama vile wikileaks.l0cal.com, wl.kallix.net, wikileaks.jbfavre.im, 213.165.84.77, 3u.ro, wiki.nlgshopping.nl, na nyingine nyingi, pia wapo FaceBook, Twitter, .....NIAMBIE UTAANZIA WAPI KUIFUTA?

PONGEZI NA TUZO

WikiLeaks imepata pongezi na tuzo kibao, pia imepata lawama kibao kwa ufichuo huo. Hata hivyo, taasisi hiyo imepata tuzo kadhaa, ikiwemo ile ya jarida la The Economist katika tuzo yake ya Chombo Kipya cha Habari ya mwaka 2008 na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (Amnesty International) tawi la Uingereza katika tuzo yake ya Chombo cha Habari Bora mwaka 2009.

Mwaka 2010 gazeti la Daily News la New York City liliiorodhesha WikiLeaks kuwa tovuti ya kwanza miongoni mwa zile ambazo “zitabadili kabisa mwelekeo wa utoaji wa habari duniani”, na Julian Assange alitajwa na jarida la Readers’ Choice kuwa Mtu wa Mwaka wa jarida la TIME kwa mwaka 2010.

Vilevile Kamishna wa Habari wa Uingereza, aliitaja WikiLeaks kuwa ni nguvu kubwa katika kusambaza habari muhimu kwa walimwengu.

Katika mlolongo wake wa kutoa habari mbalimbali kwa walimwengu, watu wengi wameiunga mkono taasisi hiyo na kupinga njama zozote ambazo zina lengo la “kuiminya”.

Watetezi wengi wa WikiLeaks wameisifu kwa kufichua siri za serikali na mashirika mbalimbali zenye mwelekeo wa uovu, na kwamba imeongeza uwazi katika utoaji wa habari na kuyaweka bayana mambo mengi ambayo yalikuwa yamefichwa kwa sababu za hila.

Wanasema pia kwamba wameona imeongeza uhuru katika utoaji wa habari, imeongeza demokrasia na kutoa changamoto kubwa kwa taasisi ambazo zilikuwa zinajiona zina nguvu zisizopingika.

Wakati huohuo, maofisa kadhaa wa Marekani wameilaumu WikiLeaks kwa kufichua habari za siri za serikali, kuvuruga usalama wa taifa, na kuharibu taratibu za kidiplomasia.

Mashirika kadhaa ya haki za binadamu yameomba WikiLeaks iwe inayahariri (yaani kuyaficha) majina ya watu wanaofanya kazi na mashirika ya kimataifa, ili kukwepesha hatua za ulipizaji kisasi zinazoweza kufanywa dhidi yao kazini kwao.

Waandishi wa habari, vilevile, wamelaumu kutokuwepo kwa uhariri wa kutosha kabla ya “kuzimwaga” habari husika hadharani na bila ya kuzifanyia uchunguzi wa kutosha.

Vilevile, Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu imeelezea wasiwasi wake kuhusu mashambulizi dhidi ya WikiLeaks, na katika taarifa yake ya pamoja na Umoja wa Nchi za Amerika (Organization of American States) imezitaka nchi na watu husika kutia maanani kanuni husika katika utoaji wa habari.

Mtandao huu ambao kauli-mbiu yake ni: Tunazifungua serikali kwa walimwengu (We open governments), waasisi wake hawafahamiki rasmi.


Julian Assange
Lakini, kama ilivyoelezwa, mtandao huo umekuwa ukiwakilishwa na Julian Assange na watu wengine tangu Januari 2007. Assange amekuwa akijelezea kama mmoja wa wajumbe wa bodi ya ushauri ya WikiLeaks.

Kwa mujibu wa jarida la Wired, mtu aliyejitolea kusema chochote kuhusiana na mtandao huo, alielezea kwamba Assange mwenyewe hujitambulisha faraghani kama “moyo na roho ya taasisi hii, mwasisi, mwanafalsafa, na msemaji wa taasisi hiyo, pamoja na kuwa mratibu, mwezeshaji kifedha, na mwongozaji wa shughuli zote za mtandao huo.

Hadi kufikia Januari 2009, mtandao huo ulikuwa na watu 1,200 wa kujitolea, ambapo kulikuwa na bodi ya ushauri, akiwemo Assange, na watu wengine wanane.

Mzee wa Wikileaks, Julian Assange

Nia kuu ya WikiLeaks: “Ni kufichua udhalimu wa tawala za barani Asia, Urusi ya Kisoviet, nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara na Mashariki ya Kati, lakini pia tunategemea kuwasaidia watu wa maeneo yote ambao wanataka kufichua ufisadi katika serikali na mashirika ya nchini mwao.”

Mahojiano ya Assange na televisheni ya Marekani
Imetayarishwa na Walusanga Ndaki kwa msaada wa mitandao

0 comments: