Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akisalimiana na wanachuo wanaochukua fani ya utabibu katika Chuo Kikuu cha Dodoma alipotembelea chuoni hapo kusikiliza matatizo yanayowakabili na kuyapatia ufumbuzi.
*Wahadhiri wakubali kuanza masomo leo
*Madai yao kulipwa mishahara ya Februari, 2011
*CAG kukagua mahesabu ya chuo ili kupata ukweli
WAZIRI MKUU Mh. Mizengo Pinda ameweza kusuluhisha mgogoro uliokuwepo baina ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)na wahadhiri wa chuo hicho kuhusu maslahi yao na kwamba wamekubali kuingia madarasani kuanzia leo.
Akizungumza na wanajumuiya ya wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) jana mchana kwenye ukumbi wa Chimwaga, Waziri Mkuu alisema matatizo yaliyojitokeza katika chuo hicho ni mlundikano wa mambo ambayo yamekuwepo siku nyingi lakini mengi ni ya kiutendaji tu na yanaweza kuisha bila kupoteza muda mwingi.
“Nimeongea na viongozi wa UDOMASA na kuwaahidi kuwa madai yenu ya posho yanaweza kukamilika mwezi Februari, nilitaka yaishe mwezi huu lakini kwa taratibu za HAZINA sasa hivi wameshaanza kushughulikia mishahara ya Januari kwa hiyo marekebisho yenu hayawezi kuwahi…wameniahidi mwezi ujao yatakamilika”, alisema huku akishangiliwa.
Amesema amemwita Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aje kukagua taarifa za mahesabu ya chuo hicho ili kubaini tuhuma zilizojitokeza za watu kulipwa hundi mbili za mishahara,walioacha kazi kuendelea kuwemo kwenye payroll ya mishahara, na wengine kukosekana kabisa kwenye payroll.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba CAG atakuwa hapa kesho… mpeni ushirikiano ili aifanye kazi kwa urahisi…, nia yetu ni kuangalia mfumo mzima wa fedha na utawala ukoje ili ikibidi uweze kurekebishwa,”alisema.
Kuhusu madai ya wanafunzi ya tatizo la maji, Waziri Mkuu alisema amemwagiza Naibu Katibu Mkuu (Fedha) Bw. John Haule ambaye alikuwepo katika ukumbi wa Chimwaga afuatilie uhamisho wa ndani wa fedha (reallocation) katika Wizara ya Maji ili zipatikane sh. bilioni 1.66 zinazohitajiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dodoma (DUWASA) kuchimba visima maeneo ya Ng’ong’ona na Ihumwa ikiwa ni pamoja na kutandaza mabomba hadi chuoni ili kupunguza shida ya maji haraka iwezekanavyo.
Pia alisema katika mipango ya muda mrefu, DUWASA pia wanataraji kupata dola za Marekani milioni 26 ambazo zitatumika kuchimba visima vingine na kujenga matanki yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 12 za maji na hivyo kuondoa kabisa tatizo la maji chuoni hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idris Kikula alimweleza Waziri Mkuu kwamba mahitaji halisi ya maji chuoni hapo ni lita milioni 3.5 kwa siku ambazo kati ya hizo, lita milioni 1.5 ni kwa matumizi ya wanafunzi peke yao na lita nyingine milioni mbili ni kwa matumizi ya ujenzi wa majengo unaoendelea chuoni hapo.
Mapema akizungumza na Kamati ya Makatibu Wakuu iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi, mara baada ya kuwasili mjini Dodoma jana asubuhi, Waziri Mkuu alielezwa kwamba kuna matatizo ya malipo ya posho na mishahara kwa watumishi na wahadhiri wa chuo hicho.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA), Bw. Idd Mwerange alimwahidi Waziri Mkuu kwamba watarudi madarasani wakati wakisubiri madai yao yakamilishwe bali aliomba kuwe na uwakilishi wa UDOMASA katika timu ya watu watakaonana na CAG.
Akifunga mkutano huo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idris Kikula alimwahidi Waziri Mkuu kwamba maagizo yake yatafuatiliwa na kwamba kesho (Jumatatu) menejimenti, idara ya Uhasibu na UDOMASA watakutana ili kuunda timu ya pamoja ambayo itakaa na kubainisha stahili za walimu wote ili orodha hiyo iwasilishwe kwa Waziri Mkuu mapema iwezekanavyo kwa ufuatiliaji.
Katika ziara yake ya jana, Mh. Waziri Mkuu alifanya vikao viwili, kimoja kikiwa cha uongozi wa Chuo Kikuu cha UDOM na kingine cha Serikali ya wanafunzi ambavyo vilidumu hadi saa 12.30 jioni na kumlazimu kuahirisha vikao viwili vilivyobaki hadi leo.
Kwa mujibu wa ratiba ya Chuo hicho,mara baada ya kukutana na serikali ya wanafunzi, Waziri Mkuu alipangiwa kukutana na jumuiya ya wanataaluma wa Chuo hicho (UDOMASA) na kisha kufanya majumuisho katika ukumbi wa Chimwaga kwa kuzihusisha pande zote tatu.
Katika vikao vyote viwili, Waziri Mkuu alielezwa matatizo yanayokibabili chuo hicho makubwa yakiwa ni uhaba wa maji, uhaba wa walimu, vifaa vya masomo na mlundikano katika mabweni.
Waziri Mkuu kabla ya kufanya mikutano hiyo miwili, alifanya ziara chuoni kukagua miundombinu ya maji safi, maji taka,vyumba vya kulala katika mabweni ya Chuo cha Sanaa na Sayansi za Jamii pamoja na mabweni ya skuli ya Tiba na Uuguzi pamoja na ujenzi wa visima vya maji.
IMETOLEWA NA:OFISI YA WAZIRI MKUU, DODOMA
0 comments:
Post a Comment