Social Icons

Monday, January 17, 2011

MADAI YA KATIBA MPYA YAZIDI KUPAMBA MOTO

Katiba inayotumika kwa sasa ambayo inahitaji kubadilishwa.

HATIMAYE Kanisa Katoliki nchini limejitosa rasmi katika mjadala wa katiba mpya likisema kuwa linaunga mkono mchakato huo, lakini likihadharisha kuwa mchakato huo unahitaji subira, weledi na ujasiri wa kisiasa kukubali mabadiliko.

Hayo yamo katika tamko maalumu lililotolewa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) katika mkutano usiokuwa wa kawaida uliofanyika jijini Mwanza kuanzia Januari 10-11, mwaka huu na kusainiwa na Rais wa baraza hilo Jude Thaddaus Ruwa’ichi.

Maaskofu wa kanisa hilo pamoja na mambo mengine walizungumzia suala la katiba mpya na tukio la kitaifa la maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uhuru wa nchi.

Kanisa hilo lilitoa wito kwa serikali na wadau wote kujadili mchakato huo wa kuandika katiba mpya likitaka busara itumike ili kufuata mchakato uliowazi wakati wa kuiandaa.

“Tunamshukuru, kwanza Rais amelitambua hilo na hivyo amekubali na kudhamiria kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na utaratibu mzuri wa kuratibu mambo yake kwa njia ya katiba inayoendana na wakati,” lilisema kanisa hilo kupitia tamko hilo maalumu na kuongeza.

“Ni matarajio yetu kwamba ili kufikia lengo na matamanio ya Watanzania walio wengi ya kuwa na katiba inayoendana na wakati, yenye misingi imara ya kidemokrasia na inayobeba matumaini ya Watanzania kuelekea miaka 50 ijayo, busara itatumika ili kufuata mchakato uliowazi.”

Kanisa lilifafanua kuwa katika kutumia busara huko kutafanya mchakato huo kuwa wazi wa haki na unaokubalika na wengi na kwamba utawezesha kupatikana kwa katiba inayolinda tunu za taifa ambazo ni amani umoja mshikamano na pia maslahi ya Watanzania wote.

Kanisa limeshauri uwapo wa jitihada za makusudi za kushirikisha watu wengi kutoka makundi mbalimbali yatakayochangia kupata mwafaka wa kitaifa juu ya katiba gani wanayoitaka Watanzania.

“Kwa kuwa bunge ni chombo cha wawakilishi wa nchini vema chombo hiki kikishirikishwa tangu mwanzo hasa katika kuweka taratibu za kufanikisha shughuli hiyo na mwisho kupata ridhaa kwa wananchi wote (referendum), mchakato huu utahitaji weledi, subira, uvumilivu wa kisiasa na ujasili wa kukubali mabadiliko,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika tarifa hiyo maaskofu waliweka bayana kuwa wao wanaunga mkono na kwamba wanatia moyo mchakato huo na na kuwaalika Watanzania wote kuungana pamoja kuliombea taifa liweze kudumu katika upendo uelewano umoja na amani.

Kuhusu maadhimisho ya Jubilie ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania bara kanisa limeelekeza waumini wake kushiriki kikamilifu katika sherehe hizo kwa kusali sala maalumu ya kuliombea taifa kuanzia ngazi ya Jumuiya, Parokia na Jimbo.

“Wazo ama lengo kuu la Kanisa Katoliki kusherehekea Jubilei ya Uhuru wa Tanzania ni kumshukuru Mungu na kuona kwamba uhuru tulioupata unaendelea kuwasaidia watu kuishi kama wana wa Mungu, maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania pia yamelenga kuongeza uelewa wa waumini na Watanzania wote juu ya umuhimu wa uhuru wa watu na taifa,” lilisema.

Sababu nyingine ni kutathmini mafanikio, matatizo, na changamoto muhimu za kitaifa za kanisa katoliki katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru katika kumwendeleza Mtanzania kiroho na kimwili na kuweka malengo ya jumla ya kudumisha uhuru wa Taifa la Tanzania.

Katika kuhakikisha kanisa linashiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, limeziagiza mamlaka zake za chini kuanzia ngazi ya jumuiya, kigango na Parokia kusali sala maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania bara kila zinapokutana na kuimba wimbo wa taifa pale inapobidi kufanya hivyo.

“Ili kufanikisha hilo, pamoja na mambo mengine , tunapendekeza kwamba kadiri ya nafasi na mazingira, wimbo wetu wa Taifa uimbwe mara kwa mara kadiri iwezekanavyo katika ibada zetu kama vile katika misa za Jumapili na katika shughuli zingine za kikanisa”, lilisema tamko.

Pia imeelezwa kuwa Parokia na Jimbo zitatakiwa kutenga siku maalum kwa ajili ya kuadhimisha misa maalumu kwa nia ya kumshukuru Mungu kwa kufikisha miaka 50 ya uhuru na kuliombea Taifa liweze kudumu katika upendo, amani umoja na mshikamano.

“Misa hizi ziadhimishwe kwa kufuata mtiririko kulingana na Kalenda ya litrujia, iteuliwe siku moja kwa ajili ya Misa ya Parokia, misa hii ifanyike Mei 31 na Agosti 15 , Misa ya Jimbo na ile ya kitaifa itafanyika karibu na kilele cha Sherehe za Uhuru (Desemba 9 mwaka huu,” lilisema kanisa hilo.

Kanisa hilo lilifafanua kuwa katika sherehe hizo kutakuwa na harakati za kuwahamasisha Wakristo na Watanzania kwa ujumla juu ya umuhimu wa uhuru katika kujipatia maendeleo ya kiroho na kimwili.

Aidha kanisa hilo limeitisha kongomano la kitaifa litakalofanyika Novemba 11 na 12 mwaka huu, lengo likiwa kutoa fursa kwa waumini na watu wote kutafakari juu ya wapi wametoka, walipo na wanakotaka kwenda kama taifa.

Moto wa kudai katiba mpya, uliwashwa na Chadema Novemba mwaka jana, baada ya kutangaza kutotambua kura zilizomweka madarakani Rais Jakaya Kikwete. Kutokana na hali hiyo, chama hicho kilianza mchakato wa kushikiza kuundwa kwa katiba mpya kwa kususia hotuba ya Rais Kikwete wakati wa akizindua Bunge la 10.

Pia wabunge pamoja na viongozi wa chama hicho walisusia sherehe za kuapishwa kwa Rais.

Katika kuendeleza madai hayo, hivi karibuni mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chadema, John Mnyika aliwasilisha hoja binafsi kwenye Ofisi za Bunge, hoja iliyokuwa na lengo la kudai katiba mpya.

Nao Wanachama wa CUF, hivi karibuni walifanya maandamano ya kuwasilisha rasimu ya katiba mpya kwa Waziri wa Katiba na Sheria. Pia viongozi mbalimbali wastaafu, walipo madarakani wamekuwa wakieleza umuhimu wa kuwa na Katiba mpya.

Miongoni mwa waliojitokeza adharani na kuunga mkono uwepo wa katiba mpya ni pamoja na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Mawaziri Wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Jaji Mkuu Mstaafu na Augustino Ramadhani, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Omar Makungu pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye aliahidi kumshauri Rais juu ya suala la kuundwa kwa Katiba mpya.

Madai ya Katiba mpya pia yamewahi kutolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa ambaye alisema bayana kuwa katiba mpya iandikwe mapema kabla ya mambo kuwa mabaya, akitoa mfano wa mapungufu ya katiba ya sasa kuwa ni rais kupewa madaraka makubwa.

Lakini akiwa Ikulu kwenye hafla ya kuapishwa Jaji Mkuu Mpya, Mohamed Othman Chande, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Frederick Werema, alisema kuwa haoni haja ya kuandikwa katiba mpya badala yake katiba iliyopo, iwekewe viraka.

“Kuandika Katiba mpya hapana, lakini kufanya marekebisho kwa kuondoa au kuongeza mambo fulani kwenye katiba, ruksa,” alisema Jaji Werema.



CHANZO: MWANANCHI

0 comments: