Social Icons

Friday, January 7, 2011

POLISI ARUSHA WAWEKA WAZI SUALA LA VURUGU ZILIZOTOKEA HIVIKARIBUNI

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha Thobias Andengenye akiongea leo. Shoto ni Naibu DCI Kamishna wa Polisi Peter Kivuyo .


JESHI la polisi mkoani hapa limesema kuwa halijafanya kosa kuvuruga maandamano na mkutano CHADEMA majuzi likidai kuwa yangeachwa yaendelee yangeleta madhara makubwa zaidi ya yaliyotokea.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha Thobias Andengenye amesema mchana huu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake kwamba jeshi hilo limetenda haki kabisa kuvuruga maandamano hayo na mkutano huo kwani iwapo vingefanyika kungeweza kutokea madhara makubwa zaidi ambayo yangewapata wananchi na mali zao.
Alisema kuwa mpaka sasa vurugu hizo zimesababisha vifo vya watu watatu baada ya leo kuongezeka ameongezeka mtu mmoja ambaye alijeruhiwa siku hiyo na kusababisha idadi ya watu waliokufa katika vurugu hizo kufikia watatu.
Kamanda Andengenye alimtaja mtu huyo kuwa ni Ismail Omari (37) mkazi wa Unga limited ambaye yeye alijeruhiwa kwa risasi tumboni katika fujo hizo. Amesema marehemu alifariki leo asubuhi katika hospitali ya mkoa ya Mounti Meru na mwili wake umeifadhiwa katika chumba cha kuifadhia maiti cha hospitali hiyo.
Naye Kamishna wa Operesheni na mafunzo ya jeshi la polisi Afande Paul Changonja amesema katika mkutano huo kwamba viongozi wa CHADEMA walikuwa wameachwa kwa dhamana baada ya kusomewa mashitaka kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria na sio kwa kufuata shinikizo la mtu yeyote.
Afande Chagonja kasema jeshi la polisi linamshangaa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mh. Zitto Kabwe kwa kujifanya kutoa amri viongozi wa chadema watolewe na kutopewa mashariti yeyote, akisisitiza kuwa hicho ni kitu ambacho hakutegemea kabisa mtu kama yeye angeweza kuongea.
"Namshangaa sana Zitto kuzungumza maneno kama haya. Anazungumza maneno bila ya kufikiria kweli, na wakati CHADEMA ndio wamesababisha haya yote. Wasilikwepe hili na wala wasitafute njia ya kulikwepa kabisa "alisema Chagonja.
Alimalizia kwa kuwapa pole wale wote waliopata mazara na kusema kuwa kwa sasa wasiwe na wasiwasi kwani hali ya mji wa arusha imerudi sehemu yake na kutakuwa na fujo tena.

0 comments: