Social Icons

Friday, January 14, 2011

KINACHOTOKEA MBARALI TAFASILI YANGU!

Pichani ni Ubaruku, mwaka jana

Babu yangu alipata kutafsiri kwa watu wake kauli ya DC: " Idzi Ilogola umujetu si monga ukweli, si monga la" ( Kisangu) Maana yake:

- Anayoongea huyu mwenzetu mengine ya ukweli, na mengine ni uongo.

Msingi wa tafsiri hiyo ni kuwataka watu wake wafikiri kwa bidii na wapime wenyewe. Kuna vurugu zimeripotiwa kule kwetu Mbarali.

Kijana mmoja amepoteza uhai jana jioni: Justin, amepigwa risasi ya kichwa na ubongo kufumuka. Hassan, amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi ya kiuno. Kosa lao: Kuhoji mamlaka, polisi.

Mbarali ni kwetu. Nimefika Mbarali mara kwa mara. Nimewasikia WanaMbarali wanaonung'unika. Nimeandika makala kadhaa kuelezea kilio cha WanaMbarali. Kwangu mimi, kilichotokea jana ilikuwa ni suala la wakati tu. Na mamlaka husika zisipolifanyia kazi haraka hili la Mbarali, nahofia madhara zaidi kutokea.

Hivi sasa kule Mbarali kuna marufuku ya magari makubwa kufika Rujewa na Ubaruku kusomba mazao kwa vile yanaharibu barabara. Marufuku hiyo ina karibu mwezi mmoja sasa. Hali hiyo inamfanya mkulima wa mpunga Mbarali kuuza kilo yake ya mchele kwa shilingi 650 mpaka 700 badala ya elfu moja.

Wachuuzi wa mchele wanadai wanafidia gharama ya kukodi magari madogo kusomba magunia ya mchele mpaka barabara kuu pale Igawa. Mkulima huyu kwa kuuza kilo ya mchele kwa shilingi mia saba ina maana ya kupunjika zaidi. Faida yake ukitoa gharama zote inabaki kuwa shilingi mia au hata shilingi 80 kwa kilo. Mkulima huyu anahitaji kumsomesha mwanawe pia.

Wanambarali wanashangaa na kuhoji, iweje marufuku ya malori makubwa ipigwe na wakai huo huo wanaona malori makubwa ya mafuta yanapita barabara hiyo hiyo kupelekea mafuta kwa wenye biashara hiyo. Ndio sababu ya baadhi wenye hasira, jana wakafikia hatua ya kusimamisha lori hilo na kuhoji. Wenzao wakapigwa risasi.Ndipo wananchi kwa hasira wakachoma moto lori na kituo cha mafuta.

Ndio, kilichofuatia ni majonzi makubwa. Tunalaani tena mauaji yale yaliyofanywa na polisi wetu. Bomu la machozi lilitosha kuwatawanya waliokusanyika badala ya kutumia risasi za moto. Kulikoni jeshi la polisi?

Na sasa kuna taarifa zinatolewa. Kuna ya ukweli, kuna ya kupotosha. WanaMbarali wanaujua ukweli. Wana kilio. Ni kilio cha haki. Wanahitaji mtu wa kwenda kuwasikiliza. Autafute ukweli.

Kisha itafutw suluhu ya mgogoro unaofukuta kabla maafa makubwa zaidi hayajatokea. Inahusu ardhi. Mashamba yao, binafsi na ya umma yaliyouzwa kwa wawekezaji katika hali ya utata. Wawekezaji wanaowanyanyasa WanaMbarali ikiwamo kuwafungia wananchi maji ya mifereji kwa mashamba yao ya mpunga.

Ndio, inahusu hali za wakulima na wafugaji wa bonde la Usangu. Serikali iingilie kati sasa kuwasaidia watu wake wa Mbarali badala ya kuwalazimisha kuchukua hatua wenyewe. Hatujachelewa.

Maggid Mjengwa
Iringa

0 comments: