Social Icons

Friday, January 14, 2011

MSUYA: SIJUI KWA NINI TUILIPE DOWANS


Waziri Mkuu wa zamani Cleopa Msuya.

WAZIRI Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya amezungumzia sakata la Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Dowans akieleza kuwa mpaka sasa hafahamu kwa nini Tanzania inapaswa kuilipa fidia kampuni hiyo ya kigeni inayodaiwa kuingia nchini kitapeli.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake
Upanga jijini Dar es Salaam, Msuya alisema anaamini hata Watanzania wengine, watakuwa wanajiuliza swali hilo.

"Wakati mwingine nashindwa hata kuzungumzia suala hili kwa sababu hadi sasa, sijui Dowans wanapaswa kulipwa kwanini. Naaamini si mimi tu ninayejiuliza swali hili, hata Watanzania wengine wengi hawajui kwanini Serikali inapaswa kuilipa Dowans," alisema Msuya.

Msuya alieleza kuwa kama suala la malipo hayo limefikiwa bila idhini ya Baraza la Mawaziri kama inavyodaiwa, hapa kuna tatizo kubwa linalopaswa kuangaliwa kwa makini zaidi.

"Kama ni kweli maana sina hakika, jambo hilo halijapita katika Baraza la Mawaziri, kutakuwa na tatizo kubwa. Kwa sababu jambo kubwa kama hilo lilipaswa lipitishwe huko liamuliwe na Serikali nzima si mtu mmoja kuamua," alisisitiza.

Msuya ameungana na mawazo ya Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliyetaka kampuni hiyo isilipwe kwa kile alichoeleza kuwa anamwamini Sitta kwa mambo mawili; ni mwanasheria makini na ni mtu aliyelishughulikia sakata la Richmond tangu akiwa Spika wa Bunge la Tisa.

"Inawezekana Samuel Sitta analijua vizuri sana jambo hili, kwanza kitaaluma ni mwanasheria, lakini pia, yeye ndiye alilishughulikia suala hilo akiwa spika bungeni. Hivyo nadhani kuna umuhimu wa jambo hilo kuangaliwa kwa makini sana," alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Msuya amezungumzia mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi nchini na kueleza kuwa siasa nchini, imevamiwa na watu wasiokuwa waadilifu na wito wa kutumikia taifa na kutoa wito kwa mamlaka husika kutowavumilia watu hao.

...Akemea maadili ya wanasiasa

Msuya mmoja wa viongozi wanaoheshimika nchini kutokana na kutumikia taifa kwa muda mrefu, ametoa mtizamo huo katika kipindi ambacho taifa limepigwa na wimbi la tuhuma nzito za ufisadi zinazohusisha baadhi ya wanasiasa wakiwemo makada maarufu wa chama tawala, CCM.

Alisema wakati wanasiasa hao wakikosa uadilifu, wengine wamekuwa wakipora mali za umma na kuonya kuwa hali hiyo inaitikisa nchi kwa sasa.

Msuya aliyeingia katika uwaziri wa fedha kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Nyerere kuwa mbunge mwaka 1972 hadi 1975, alisema ndiyo maana, hafikiri kushawishi watoto wake kujiunga na siasa kama wenyewe hawana wito wa kutumikia umma.

"Siasa inataka wito wa kusaidia watu, lazima uwe na moyo wa kutumikia nchi. Ndiyo maana, nilichofanya ni kusomesha wanangu waweze kupambana na dunia. Kama wakitaka siasa lazima wao wenyewe wajipime wana wito wa kutumikia wananchi?" alihoji Msuya ambaye alikuwa waziri mkuu kwa mara ya kwanza kuanzia Novemba 1980 hadi Februari 1983, chini ya uongozi wa Mwalimu.

.... tatizo kubwa lililopo sasa kuna baadhi ya watu wasiokuwa na wito wa kutumikia taifa wanaingia katika siasa. Hawana uchungu wala uzalendo na taifa bali wanataka kuingia kwa ajili ya kupata umaarufu na kupora nchi."

Alisisitiza , kutokana na tatizo hilo la baadhi ya waporaji kuvamiwa siasa ndiko kunakochangia matumizi mabaya ya fedha za umma katika safari na ununuaji wa magari ya kifahari maarufu kama mashangingi.

"Siku ya maadhimisho ya kuzaliwa kwangu niliwaambia watu wakati nikiwa waziri mkuu niliwahi kuwa napokea mshahara wa Sh3,000 wakashangaa. Wengi ambao wamekuwa wakifanya hivyo sasa hivi wameshakufa tumebaki wachache tu," alitia mkazo umuhimu wa taifa kupata viongozi waadilifu na wenye wito wa kutumikia taifa.

Mzee Msuya ambaye sasa ametimiza miaka 80, aliongeza, " Unafikiri haya magari ya kifahari ingekuwa ni mtu binafsi angenunua? Wananunua kwasababu gharama za kuendesha siyo za kwao. Kwasababu ukiacha gharama za kununua kuyaendesha haya ni kazi kubwa."

Alisema umefika wakati wa kutokuwepo uvumilivu katika kusimamia misingi ya maadili na miiko ya uongozi iliyokuwepo tangu wakati wa Mwalimu na kusisitiza, "Misingi ile ipo tatizo ni watu. Ni sawa na dini vitabu vinakataza dhambi, lakini binadamu wanatenda. Sasa lazima kuwe na zero tolerance."

...nasisitiza zero tolerance kwa wanaovunja sheria, lazima utawala wa sheria uheshimike kuhakikisha utekelezaji wa misingi ya maadili na miiko ya uongozi, Mwalimu alisema wapo wanyonyaji sasa kama tukiacha kuvumilia wanaokiuka misingi, wanyonyaji watashindwa."

Akisisitiza umuhimu wa kuzingatiwa kwa sheria, mzee Msuya alisema Bill Clinton alinusuruka kupoteza urais baada ya kukumbwa na kashfa ya ngono na kuongeza, "wenzetu hawana utani katika mambo ya kisheria hakuna mchezo, huku kwetu tatizo bado kuna uswahili."

Msuya alihoji mantiki ya kuendelea kuvumilia kuchezewa kwa utawala huku baadhi ya ya taasisi nyeti zikisafisha watuhumiwa wakiwemo wa rushwa kubwa kisha mamlaka nyingine zinakanusha.

Ingawa hakutaja jina la taasisi wala watuhumiwa, tukio la hivi karibuni ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoa taarifa ya kumsafisha mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na kashfa ya rada, lakini Uingereza ikakanusha jalada la sakata hilo kufungwa.

…Aunga mkono mabadiliko ya katiba

Akizungumzia suala hilo ambalo limeibua mjadala mzito nchini, alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuridhia mchakato huo huku akiweka bayana anakubaliana na uamuzi wa kuunda Tume maalumu itakayojumuisha watu wa makundi mbalimbali.

Mzee Msuya ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili na pia Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya uongozi wa Rais Alli Hassan Mwinyi kuanzia Desemba 1994 hadi Novemba 1995, alisema Rais Kikwete ni msikivu hivyo ni vema vyama vya mageuzi vikakubaliana na uamuzi wa tume ambayo pia itawashirikisha.

"Ni wakati muafaka kuwa na katiba mpya, naungana kabisa na Rais Kikwete katika msimamo wake wa kuunda tume ambayo naamini itawashirikisha hadi wapinzani. Ni uamuzi sahihi kabisa ambao sote tunapaswa kuukubali," alisisitiza msimamo wake wa kumuunga mkono Rais.

Hata hivyo, alitahadharisha watu wanaojaribu kudai katiba kwa njia zinazoashiria kuvunja amani, akiwakumbusha kwamba suala hilo ni la kitaifa linalopaswa kuweka dira ya nchi kuona baada ya miaka 50 ijayo mwelekeo wa nchi utakuaje.

Mzee Msuya ambaye aliamua kuacha kugombea ubunge wa Mwanga mnamo Oktoba 29 mwaka 2000, alisema taifa limetimiza miaka 50 baada ya uhuru hivyo, ni fursa kwa Watanzania kutathimini miaka 50 ijayo watakuwa wapi.

Kwa msisitizo, alisema dira hiyo ya taifa inapaswa kuwekwa pia katika katiba huku akisisitiza tume ya Rais itakayoundwa itapaswa kutumiwa vema na Watanzania kutoa maoni yao kuhusu wapi nchi itakwenda baada ya kipindi kingine cha miaka 50 na vipi itafika huko.

Alisema Watanzania wanapaswa kujiandaa vema kuitumia tume hiyo itakayoundwa na Rais Kikwete kwa ajili ya kutoa maoni yao yatakayokuwa na maana, ili kuwezesha kuwepo misingi imara ya maendeleo ya taifa.

Uchaguzi 2010 CCM ilipigwa kwenye ngome zake
Kuhusu matokeo ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, kada huyo aliyejiunga na TANU kuanzia mwaka 1964, alisema chama hicho kitapaswa kujitathimini upya kutokana na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana ambao umetikisa ngome zake za kisiasa katika maeneo muhimu ya kimkakati.

Akirejea historia ya CCM tangu TANU na ASP, alisema chama hicho kiliwahi kujitathimini katika matukio makuu matatu muhimu kuanzia uhuru, Azimio la Arusha na kisha baadaye mwaka 1977 kilipozaliwa rasmi upya kwa kuunganisha vyama hivyo viwili.

Mzee Msuya alifafanua kwamba, kupoteza majimbo muhimu kama Nyamagana ambalo lilikuwa likiongozwa na waziri Lawrence Masha, Arusha mjini na Mbeya mjini na Maswa ni pigo kubwa kutokana na maeneo hayo kuwa ya kimkakati zaidi kwa siasa zinazochangiwa na idadi ya watu.

"Mwanza ni jiji kubwa na la pili baada ya Dar es Salaam, kupoteza Jimbo la Nyamagana, Ilemela ni pigo kubwa. Maswa nako huko kanda ya Ziwa tumepoteza, tutapaswa kujiuliza kwa mfano, je, huyu (John) Shibuda alishindwa kweli kura za maoni au ni majungu tu, mbona alishinda alivyotoka chama? Arusha mjini nako baada ya kuondoka (Felex) Mrema, huyu waziri Batilda (Burian) naye alishindwa, " alitaja majimbo hayo nyeti na kuongeza,

"Tutapaswa kukaa na kutathimini upya mwelekeo wa chama. Naamini tutapata majibu ya msingi baada ya kukaa na mwenyekiti wetu, Jimbo kama Mbeya mjini ameenda kijana musician, hili ni jimbo nyeti. Lakini, chama chetu kimekwishajitathimini katika matukio makubwa matatu tangu tulivyopata uhuru," alifafanua.

"Kilimanjaro tumepoteza majimbo ya Hai, Rombo, Moshi mjini na Vunjo, Mrema pia ametushinda wakati amekwisha kisiasa? Siyo siyo siri hata ninyi mnajua kama amekwisha kwa hiyo tatizo ni jimbo kama Hai. Lakini, tutajitathimini."

Alitaja matukio hayo kwamba, ni baada ya uhuru ambako TANU iliamua utaratibu wa kupigiakura majina ya watu wenye rangi tatu, Mwafrika, Mzungu na Mhindi ndiyo maana kukawepo mawaziri machotara, pili ni mwaka 1967 lilipozaliwa Azimio la Arusha na kuweka miiko ya uongozi na mwaka 1977 TANU na ASP vilipoungana na kuzaliwa CCM.

Kwa tathimini yake ya awali, alisema ingawa chama kitakaa kuangalia ni vipi kilipoteleza, lakini mtazamo wake wa awali kuhusu matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana yanayonyesha yalitokana na sababu kuu tatu, ambazo ni chama kujisahau, wananchi kutorodhishwa na baadhi ya viongozi na mipango ya maendeleo na kuongezeka vuguvugu la vijana wanaotaoka maendeleo kwa kushiriki mchakato wa uchaguzi.

Alifafanua kwamba, ishara moja inayoonyesha chama kujisahau inapatikana hata kwenye salamu ambayo husema, "Kidumu chama cha mapinduzi na wengine huitikia...kidumu chama tawala. Huku ni kujisahau lazima tujitathimini upya," alifafanua.

Wananchi wanachukia ahadi hewa
Mzee Msuya akielezea sababu ya pili, alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikatishwa tamaa na baadhi ya viongozi ambao wanaonekaa kutokuwa na moyo wa kuleta maendeleo zaidi ya kile wanachoamini ni kula nchi wenyewe.

Kwa msisitizo, alisema hali hiyo inafanya baadhi ya wananchi kuamini CCM ni kundi la watu wanaolindana kula nchi huku akiweka bayana, "Sasa akitokea mtu mwenye kuweza kuongea vizuri na kushawishi watu wanageuka. Maana, watasema hao wanakula nchi wenyewe na kulindana."

"Tutapaswa kujitathimini kama chama kimekuwa ni dodoki ambalo limemeza hadi machafu au la, je tufanyeje li kuhakikisha maji hayo na uchafu wake unatokana ili kiwe safi ni jambo ambalo naamini tena, tutalipatia ufumbuzi," alisisitiza.

Sababu ya tatu, aliongeza kwamba kumekuwa na mwamko mkubwa wa vijana kushiriki katika mchakato wa uchaguzi hasa upigaji kura wakitegemea kuwepo maendeleo yatakayowapa maisha mazuri kitu alichokiita kuwa ni sahihi kuamini hivyo.

"Tatu, wapigakura wengi ni vijana, hawa ukiwaambia mkinichagua nitafanya hivi na wakikuamini basi, vijana wanataka kuendesha magari mazuri, wanataka kuishi katika nyumba nzuri na kusoma vizuri, vitu ambavyo ni sawa tu kuamini kwani wao wanataka maisha," alisisitiza.

Alisisitiza kwamba, chama kitapaswa kujitathimini kuona kama viongozi wa kuchaguliwa ni waadilifu na wenye moyo wa kutumikia wananchi, vinginevyo kitapaswa kuamua kama kipitishe fagio la chuma kwa wasiofaa au kitumie utaratibu upi utakaofaa kujinusuru.

…Anaamini CCM itapata mgombea mzuri 2015

Hata hivyo, kuhusu kuchomoza kwa kasi vuguvugu la vyama vya mageuzi na kama linaweza kutishia uhai wa chama hicho mwaka 2015, alisema, "ukuaji wa vyama vya upinzani ndiyo mantiki ya CCM kuamua kurejesha mfumo huo wa vyama vingi mwaka 1992."

Kada huyo wa CCM, alisema chama hicho tawala ndicho kiliamua kurejesha mfumo huo licha ya asilimia kubwa ya wananchi kukataa na kusisitiza, ni vema vyama hivyo vikue ili vilete changamoto kubwa ya kisiasa.

Alifafanua kwamba, chama tawala kikaa peke yake bila kupata upinzani hujisahau kabisa ndiyo maana, hata Urusi kuliibuka vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa kuelekea vyama vingi.

"Kwa hiyo uchaguzi wa mwaka 2015 haunipi wasiwasi sana, najua CCM ni chama makini, kitakaa na kujitathimini kilikosea wapi na vipi ijirekebishe.

Changamoto ni hii iliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambazo ndizo tunapaswa kuziangalia na kutoka na mikakati ya kwenda mbele," alirejea kipigo hicho cha 2010 ambacho kilipunguza hadi kura za urais za Kikwete kutoka asilimia 80 hadi 61.

Alitamba pia, chama hicho kina uhakika wa kupata mgombea bora wa urais kwa mwaka 2015 ambaye anatarajiwa kukubalika vema kwa wananchi wa Watanzania wakati uchaguzi ukiwadia.

Vurugu za Arusha zimetia doa nchi
Mzee Msuya aliweka bayana kwamba limeitia doa nchi ,lakini akasisitiza umuhimu wa kuheshimiwa utawala wa sheria, huku akitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutii na kuheshimu mamlaka za nchi.

"Ndiyo haya nazungumza umuhimu wa kuheshimiwa utawala wa sheria, mumeshaambiwa msiandamane bali fanyeni mkutano wenu bado mnaandamana, sasa wakiulizwa kwa nini waliandamana wanasema...oo! Haiwezekani kila mtu afanye maamuzi yake katika nchi," alisisitiza.

Alisema Chadema inachopaswa kufanya ni kwenda mahakamani kudai haki kwani kama uchaguzi ulikuwa na kasoro mahakama inaweza kutengua kama inavyofanyika mara kwa mara katika matokeo ya ubunge kwenye majimbo mbalimbali.

"Zipo chaguzi za ubunge ambazo matokeo yametenguliwa, wanachopaswa kufanya Chadema ni kwenda mahakamani kudai haki yao si kupingana na vyombo vya dola kwa kufanya maandamano ambayo yamepigwa marufuku. Lazima uwepo utawala wa sheria," alisisitiza Msuya ambaye ana historia ya kufanya maamuzi magumu.

Aliweka bayana kwamba, CCM haikujipa yenyewe ushindi bali kilichofanyika ni mamlaka ya uchaguzi kukipa ushindi chama hicho baada ya mchakato wa upigajikura hivyo kama ni kulalamikia taratibu, Chadema inapaswa kwenda mahakamani kudai haki.

"CCM haikujipa ushindi, ni mamlaka ya uchaguzi baada ya upigaji kura kufanyika, sasa kama ni ukiukwaji wa taratibu malalamiko hayo yanapaswa kupelekwa mahakamani, lakini si njia nyingine yoyote. Hii ni Law (sheria), kusema CCM wazungumze, wanataka wazungumze nini sasa?" alihoji kada huyo mkongwe.

Baraza jipya la mawaziri
Mzee Msuya ambaye anaonekana kuwa na imani kubwa na Rais Kikwete katika utendaji kazi, alimsifia akisema baraza alilounda amejaribu kuondoa watu aliowaita kuwa ni wenye madoa yasiyofutika katika jamii ya Watanzania.

"Ninachoona mimi, Rais Kikwete ameunda baraza la mawaziri zuri kwa kujaribu kuondoa watu wenye madoa, ameunda baraza ambalo limejaa watu wasiokuwa na madoa ambayo yanafahamika katika jamiii yetu," alifafanua.

Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kujifunza mambo ili kupata uzoefu wa utendaji kazi serikalini ili kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo iliyowekwa na Serikali.

Jumuiya ya Afrika Mashariki
Waziri huyo wa Viwanda kati ya mwaka wa 1975 hadi 1980, alisema ni vema Watanzania wakajiuliza watanufaikaje na Jumuiya ya Affrika Mashariki baada ya kuvunjika ile ya mwaka 1967 hadi 1977, ambayo tayari ilikuwa inakwenda vizuri.

Mzee Msuya alisema wakati ule tayari kulikuwa na mipango mingi ya maendeleo, lakini ghafla Kenya ikavunja jumuiya hiyo na kuzuia ndege katika Shirika la Ndege la Afrika Mashariki, na kuvuruga mfumo wa usafiri wa anga wa Tanzania mwaka ambao TANU na ASP viliungana na kuzaa CCM.

Alisema tayari Tanzania ilijenga makao makuu Arusha ambayo sasa ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) na Shirika la Bandari, huku Uganda ikiwa na Shirika la Posta na kuongeza kwamba, hana tatizo na muundo wa sasa, lakini kuna umuhimu wa nchi kfufua viwanda vyake ili kuepuka kuwa soko la bidhaa za Kenya.

Waziri huyo wa Fedha, Mipango na Uchumi kati ya Novemba 1985 hadi Machi 1989, alisema Kenya imekuwa ikijitanua kibiashara katika maeneo mbalimbali hadi Sudan Kusini na kuonya, kama Tanzania haitakuwa makini kufufua viwanda itageuzwa soko kuu la bidhaa za nchi hiyo.

Alisema vijana lazima wapatiwe elimu bora itakayowawezesha kushiriki vema katika soko la ushindani wa ajira, kuleta maendeleo ya taifa na kuongeza kwa hali ilivyo sasa Tanzania inapaswa kufanya kazi ya ziada kukabiliana na ushindani huo mkubwa.

Nchi iweke msukumo kwenye viwanda
Aliweka bayana kwamba, alipoteuliwa kushika wadhifa huo Mwalimu alimpa kazi kubwa kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali ili kujengea taifa uwezo wa kujiendesha kiuchumi.

Msuya anataja mikakati hiyo kwamba ilikuwa ni kujenga viwanda vya nguo 25, viwanda vya ngozi, zana za kilimo, mbolea, saruji, mahitaji ya nyumbani na kuongeza, bahati mbaya vitu hivyo vilikufa kabisa katika sera ya ubinafsishaji ingawa baadhi vilipigwa na mawimbi ya matatizo ya kiuchumi katika miaka ya 1970 hadi 80.

Alisema kuna changamoto kubwa kuhakikisha viwanda vyote muhimu vya nchi vinafufuliwa ili taifa liweze kujitosheleza na kusisitiza hilo linawezekana kwa kuwepo mipango ya kitafiti ambayo itatoa matokeo ya kufanikisha mipango.

Hata hivyo, alisifia uamuzi wa Rais Kikwete kurejesha upya Tume ya Mipango na kuongeza hiyo inapaswa kutoa dira ya wapi taifa linataka kwenda kiuchumi na inataka iwe kama nchi gani zilizopiga hatua harakaa kama Korea, Singapore au Malaysia.

Alisema Dubai ni nchi isiyokuwa na utajiri, lakini akaongeza, "Siku moja waziri wao akasema nataka kuondoa Dubai kutoka kisiwa cha uvuvi kuwa nchi ya kibiashara.

Kweli imewezekana, sasa Dubai imekuwa nchi yenye uchumi wa kisasa, kuna bandari kubwa, viwanja vya ndege ambazo ndege kubwa zinatua kila siku, watalii wanaingia kwa wingi na sisi lazima tuwe na mipango hiyo ya mbali, nampongeza sana Rais kwa kurejesha tume hiyo."

Haya ni mahojiano ya kwanza kati ya Mzee Msuya na vyombo vya habari katika kipindi cha mwaka huu ambao ametimiza miaka 80 ya kuzaliwa.

CHANZO: MWANANCHI

0 comments: