Social Icons

Friday, January 14, 2011

JUKWAA LA SANAA BASATA NA SAFARI YA KUIKOMBOA SEKTA YA SANAA NCHINI

Mwanamitindo na mrembo maarufu nchini, Lisa Jensen akiwasilisha moja ya mada kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kuanzia saa 4 kwenye Ukumbi wa BASATA. Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego na wengine kutoka kushoto kwake ni Maratibu wa Jukwaa hilo Ruyembe Mulimba na Mkurugenzi wa Kundi la Parapanda, Mgunga Mwanyenyelwa.
Na Alistide Kwizela
Kwa kawaida hatuwezi kupata maendeleo katika sekta yoyote bila kuwepo kwa vyanzo mahsusi vya kupashana habari, kubadilishana uzoefu, kupata mafunzo, ujuzi na maelekezo mbalimbali katika kuhakisha uboreshaji wa yale tunayoyafanya na yale tunayopanga kufanya katika siku za usoni.

Mantiki hii ina ukweli mmoja kwamba, jamii yoyote inapokuwa haina ufahamu na elimu yoyote katika masuala mbalimbali basi inakuwa iko gizani na inayowayawaya. Daima watu wa jamii hii watakuwa wa kuonewa, kudhulumiwa na hatimaye kutawaliwa na watu wajanjawajanja ambao hapana shaka yoyote watakuwa wanatumia ugiza wa jamii husika katika kujinufaisha.

Jukwaa la Sanaa ni program ya wazi iliyoasisiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari za sanaa na utamaduni (CAJAtz) ili kuhakikisha inawatoa wasanii na wadau wa sekta ya sanaa hapa nchini katika hali hiyo ya ugiza.

Ni program ambayo imekuwa ikifanyika kila Jumatatu kuanzia saaa 4 kwenye Ukumbi wa BASATA kwa lengo la kuwa daraja la kupashana habari baina ya wadau wa sanaa.

Ingawa mwanzo wakati linaasisiwa lilikuwa limelenga kuwafikia wadau 1,000 katika kipindi cha mwaka mmoja kwa sasa limevuka lengo kwa kuhudhuriwa na zaidi ya wadau wapatao 2,700 huku mada zipatazo 47 kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo wasanii na harakati zao za kila siku zikiwa zimewasilishwa na wataalamu 52.

Hili ni moja ya mafanikio ya Jukwaa hili ambalo lilianza mapema Februari mwaka jana kwa kuzinduliwa rasmi na aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Vijana na Michezo,Mheshimiwa Joel Nkaya Bendera.

Baadhi ya mada zilizopata kuwasilishwa na kuvuta wadau wengi huku zikiacha mafunzo mapana kwa wasanii ni pamoja na Ujasiriamali katika shughuli za sanaa,muelekeo wa tunzo za muziki Tanzania na changamoto zake,Changamoto ya Sanaa ya unenguaji katika Muziki wa dansi,Mchango wa Vituo vya Sanaa vya nje katika kukuza Utamaduni wa mtanzania.

Mada zingine japo kwa kuzitaja chache ni pamoja na,Mchango wa vyombo vya habari katika kulinda maadili ya mtanzania,soko la sanaa ya ubunifu wa mavazi nchini na changamoto zinazowakabili,Mchango wa maprodyuza katika kujenga utambulisho wa muziki wa Tanzania na nyingine nyingi zinazofikisha idadi ya mada 52.

Kwa ujumla mahudhurio ya wadau katika Jukwaa hilo la Sanaa yamekuwa ni makubwa kiasi cha Baraza la Sanaa la Taifa mara kadhaa kuwa na changamoto ya kuongeza idadi ya viti ukumbini ikiwa ni pamoja na kulilia kukamilishwa kwa ujenzi wa ukumbi wa Baraza hilo unaofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao kwa sasa umesimama kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi hadi sasa.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego,Jukwaa la sanaa ni sehemu pekee ambapo wasanii na wadau wa sanaa wanapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu ikiwa ni pamoja na kukutanishwa na wadau tofautitofauti ambao mbali na kutoa elimu, mafunzo na changamoto anuai wamekuwa pia wakitoa fursa za kukuza vipato na vipaji vya wasanii.

Anaongeza kwamba,Jukwaa la Sanaa ni foramu ambayo hapana shaka pamoja na serikali kuitumia kama daraja la kuwafikia wadau kwa urahisi, wasanii na wadau wa sekta hii wanaitumia katika kuhakikisha wanaishauri serikali na kufikisha madai yao mbalimbali.

Kwa maneno mengine Materego analiona Jukwaa la Sanaa kama sehemu ya kutoa yaliyomo moyoni mwa wadau wa sanaa na kuachana na dhana ya ulalamishi miongoni mwa wasanii wetu pia upotoshwaji unaoweza kufanywa na waandishi wa habari katika masuala yahusuyo tasnia hii.

“Ninaamini kwamba,Jukwaa la Sanaa ni mahali tunapokutana na wadau wa kila aina, kuanzia na serikali yenyewe, wadhamini wa tasnia hii, waandaaji wa matamasha ya sanaa na burudani na wadau wengine wengi.Hapa ndipo tunakopatia elimu pia fursa mbalimbali katika kazi zetu.Kwa ujumla hapa ndipo tunapopashana habari sahihi kuhusu tasnia hii” anasisitiza Materego.

Ukiacha suala la mahudhurio, moja ya sehemu tata ambayo imekuwa ni kilio cha wasanii na wadau wengi ni suala la mikataba.Inaelezwa kwamba, wasanii wengi wamekuwa wakifanya kazi pasipo kuzingatia mikataba au kusaini mikataba pasipo kuing’amua barabara hali ambayo imekuwa ikiwafanya wapoteze haki zao.

Jukwaa la Sanaa kupitia mada za Mirabaha na Haki Za Wasanii Katika Kazi za Sanaa Andishi iliyowasilishwa na Shirika la KOPITAN na ile ya Haki miliki na Mikataba KAtika Kazi za Sanaa iliyowasilishwa na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) limeweza kuwafumbua wasanii.

Aidha,dhana ya kiutendaji kati ya BASATA na COSOTA iliyokuwa ikichanganywa na wadau wa sanaa hasa katika wajibu wa ulinzi wa haki za kazi za wasanii sasa imeeleweka.Awali wadau wengi na baadhi ya waandishi wa habari walikuwa wakiamini kwamba BASATA ndiyo yenye kulinda haki katika kazi za sanaa wakati hali ni tofauti.

Katika kuhakikisha BASATA inafanyia kazi maazimio na hoja zote zilizoibuka kwenye Jukwaa la Sanaa katika kipindi kizima cha mwaka uliopita,umeandaliwa Mpango mkakati wa mwaka 2011-2014 ambao kwa mujibu wa Bw.Materego umebeba mawazo mengi ya wadau wa Jukwaa la Sanaa.

Anayataja baadhi ya mawazo hayo kuwa ni pamoja na kuhimiza ufundishwaji wa stadi za sanaa toka elimu ya awali, kuhuisha sheria na kanuni za BASATA, kuimarisha mafunzo kwa wasanii na maafisa utamaduni.

Ama katika ulalo huohuo,mpango mkakati huo wa BASATA ambao kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya Jukwaa hilo la Sanaa unatajwa kubeba ukombozi mkubwa katika tasnia ya sanaa ambapo sasa nguvu inaelekezwa katika ukusanyaji takwimu za sekta ya sanaa, kuandaa tunzo za sanaa na zile za waandishi wa habari waliofanya vizuri katika kuandika makala na habari za sekta ya utamaduni hususan sanaa.

Aidha,Katika Jukwaa la Sanaa moja ya mada ambazo kamwe haziwezi kuwekwa kando ni pamoja na ile ya Mkurabita na Dhana ya Kuwawezesha Wanyonge iliyowasilishwa na Maafisa kutoka Mpango wa Kurasimisha Biashara za wanyonge (MKURABITA) ambayo ukiacha mipango iliyokuwepo toka mwanzo imeweka msukumo kwenye zoezi linaloendeshwa sasa hivi na BASATA la kurasimisha sekta ya sanaa nchi nzima ambapo kwa sasa limeanza kwa kutambua na kusajili kumbi zote za sanaa na burudani kabla baadaye halijahamia kwa wadau wapana wakiwemo wasanii.

Mnamo Septemba 21, 2010, Jukwaa la Sanaa kwa kushirikiana na Shirika la AMREF liliandaa program maalum ya kupima VVU/UKIMWI na utoaji ushauri nasaha kwa wadau wake.

Zoezi hili ambalo lilienda sambamba na mada ya Wasanii Katika mapambano Dhidi ya UKIMWI iliyowasilishwa na Bi.Sydney Msamba kutoka Programu ya Monitoring and Evaluation ilihusisha jumla ya wadau 79 ambapo wanawake walikuwa 40 na Wanaume 39.Katika zoezi hili ni wanaume wawili tu waliokutwa na VVU.

Kwa ujumla majumuisho ya mada mbalimbali zilizowasilishwa na kuchangiwa kwa kiwango kikubwa na wadau wa Jukwaa la Sanaa ikiwa ni pamoja na uwepo wa muda wa maswali na majibu yameanzisha zama mpya kabisa si tu katika kupanua uelewa wa wasanii na wadau wa sanaa katika masuala mbalilmbali ya tasnia hii bali pia yameifanya BASATA iwe maskani kamili ya wasanii na waandishi wa habari.

Katika kuonesha kwamba,Jukwaa la Sanaa lazima lipewe msukumo, katika mwaka huu wa 2011,Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Materego ameongeza vipengele kadhaa katika Jukwaa ambapo kila mwisho wa mwezi wasanii mbalimbali waliopata mafanikio katika tasnia watapata wasaa wa kuonesha kazi na wengine kuzisikilizisha kabla baadaye hawajaeleza siri ya mafanikio yao.Pia hili litaenda sambamba na Jukwaa kutumiwa na wasanii kutambulisha kazi zao.

Hata hivyo,pamoja na hatua iliyofikiwa na Jukwaa la Sanaa bado changamoto zinazolikabili ni nyingi lakini kubwa ni ukosefu wa wafadhili kwani gharama za kuliendesha zimekuwa kubwa.Changamoto zingine ni habari kutoka kwenye Jukwaa kutokuripotiwa kwa wingi kwenye vyombo vya habari,wasanii wazoefu kutojitokeza ingawa hili limekuwa likielezwa mara kadhaa kwamba, linatokana na kulewa umaarufu na wao kuamini wanajua kila kitu.



Mkurugenzi wa Bendi ya Muziki wa Dansi wa Extra Bongo, Ally Choki Mzee wa Farasi akichangia mada kwenye Jukwaa la Sanaa.


Mwandishi wa makala haya ni Afisa Habari wa BASATA na anapatikana kwa simu namba +255 715/767 082 889 au e-mail: alistide.kwizela@basata.or.tz

0 comments: