JANUARI,12/ 2011
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal,
Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Seif Sharif Hamad,
Makamo wa Kwanza wa Rais, Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi,
Makamo wa Pili wa Rais, Zanzibar;
Mheshimiwa Alhaji Mzee Ali Hassan Mwinyi,
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Salmin Amour
Rais Mstaafu wa Zanzibar
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume,
Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Assalaam Alaykum,
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutuwezesha kukutana hapa leo, tukiwa wazima na wenye afya na tuko katika hali ya amani na utulivu.
Pili, kwa niaba yenu nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati viongozi wetu wa Kitaifa walioungana nasi katika maadhimisho haya.
Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete; Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal; Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi; Marais Wastaafu wa Zanzibar Mheshimwa Dkt. Salmin Amour na Dkt. Amani Abeid Karume na Waziri Mkuu, wa Tanzania Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Vile vile, napenda kuwashukuru sana viongozi wote wa vyama vya siasa, Mabalozi na Washirika wetu wa Maendeleo. Shukurani za pekee zije kwenu wananchi mliohudhuria maadhimisho haya pamoja na wale walioko majumbani, ambao wako pamoja nasi kupitia redio na televisheni. Kwenu nyote nasema ahsanteni sana.
Ndugu Wananchi,
Napenda kuchukua fursa hii adhimu kukushukuruni wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki kwenu kikamilifu katika kura ya maoni, ambayo imepelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa uliojenga msingi imara wa mashirikiano katika kuleta maendeleo ya Zanzibar, bila ya kujali itikadi za kisiasa.
Vile vile napenda kutoa shukurani zangu maalum kwenu pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na usalama na Tume ya Uchaguzi, kwa kuwezesha mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2010 kuwa wa amani, usalama na utulivu mkubwa. Nasema hongereni sana.
Shughuli zote mbili yaani kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu zimetuletea sifa kubwa ndani na nje ya nchi yetu na tunaamini kwamba huenda ikawa ni mfano wa kuigwa na nchi nyengine. Tunazishukuru Jumuiya za Kimataifa kwa namna walivyopokea na kufurahishwa na matokeo ya uchaguzi pamoja na kuundwa kwa Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Ndugu Wananchi,
Leo tunatimiza miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, kama zilivyofanya Serikali za Awamu Sita zilizopita, lengo lake kubwa ni kuyalinda na kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi hayo.
Tutahakikisha yale mambo ya msingi ya Mapinduzi yanaendelezwa kwa juhudi zote, likiwemo suala la ardhi kuendelea kuwa mali ya Serikali, pamoja na elimu na huduma za Afya kuendelea kutolewa bila ya ubaguzi. Sekta nyenginezo zikiwemo huduma za maji safi na salama, makazi bora na miundo mbinu zitaimarishwa. Aidha, umoja, mshikamano na utulivu ikiwa ndio nguzo kubwa ya maendeleo yetu, vitadumishwa.
Katika kutekeleza hayo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeunda Wizara kumi na sita (16) na Uteuzi wa Makamo wa Kwanza wa Rais na Makamo wa Pili wa Rais na Mawaziri wote umezingatia matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010.
Wizara hizo zimeundwa ili ziweze kutekeleza vyema Malengo ya Milenia, Dira ya mwaka 2020, MKUZA I na II pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010/2015. Kadhalika muundo wa Wizara hizo umekusudiwa kuleta ufanisi Serikalini na kuweza kuwahudumia wananchi kwa kuwapelekea huduma bora na kwa mujibu wa mipango iliyopangwa.
Ninatarajia kwamba wafanyakazi wa Wizara mbali mbali watajitahidi kufanyakazi kwa bidii na maarifa ili kuyafanikisha malengo ya Wizara zao katika kuwatumikia wananchi.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na awamu zote zilizopita za uongozi, tunajivunia kuwa nchi yetu imeweza kupiga hatua za maendeleo katika sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Katika kipindi hicho tumeweza kushuhudia ongezeko la pato la Taifa, kupanuka huduma za usafirishaji na mawasiliano, uimarishaji wa makazi ya wananchi, kuongezeka kwa kiwango na ubora wa elimu na afya pamoja na kuimarika kwa miundombinu na huduma za ustawi wa jamii pamoja na ukuaji wa demokrasia na utawala bora.
Zaidi ya hayo tumeshuhudia juhudi za kuleta umoja na mshikamano pamoja na amani na utulivu.
Ndugu Wananchi,
Ni fahari kwetu kuwa pato la Taifa limekua kwa kiasi cha asilimia 17 kutoka mwaka 2008 hadi 2009. Kiwango hiki kimeweza kuchangia kasi ya ukuaji wa hali ya uchumi katika nchi yetu. Uchumi wetu unakadiriwa kukua kwa asilimia 7 kwa mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 5.3 iliyofikiwa mwaka 2008.
Ni azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuziendeleza juhudi za ukuzaji wa uchumi, na hivyo kuimarisha ustawi wa jamii ifikapo mwaka 2015, sawa na matarajio ya Malengo ya Milenia, MKUZA, Dira ya Zanzibar ya 2020 na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya 2010/2015.
Ndugu Wananchi,
Tunatilia maanani mafanikio ya awamu zilizopita katika kustawisha huduma za fedha na ukuzaji rasilimali za Serikali na wawekezaji wa nje. Ukuzaji rasilimali umeongezeka kwa asilimia 21.2 kutoka T.Shs. 145,151 milioni mwaka 2008 kufikia T.Shs. 175,877 milioni mwaka 2009. Tunaimani kwamba uwekezaji huu utachochea zaidi ukuaji wa uchumi katika kipindi kijacho.
Serikali ya Awamu ya Saba imevutiwa sana na ustawi huu wa uchumi, hasa ikizingatiwa kuwa hali ya uchumi ya dunia ilikumbwa na msukosuko wa kifedha ambao uliathiri nchi nyingi duniani. Tumejipanga vyema kuendeleza ustawi huu wa uchumi kwa kuchochea kasi ya uwekezaji na ujenzi wa msingi wa uchumi endelevu. Tutaendeleza misingi ya mafanikio iliyowekwa na awamu zilizopita, hasa awamu ya sita. Sera na sheria za uwekezaji nazo zitaimarishwa.
Ndugu Wananchi,
Ni wajibu wetu kukumbuka na kuthamini mafanikio ya Wizara ya Fedha na Uchumi yaliyofikiwa katika Awamu ya Sita katika ukusanyaji wa fedha na usimamizi wake, uliotekelezwa na taasisi zetu zote, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) pamoja na watendaji wa Wizara ya Fedha.
Kutokana na kupanua wigo wa mapato na kuimarika kwa utendaji wa taasisi hizi, thamani ya mapato yaliyokusanywa yalikuwa kutoka T.Shs. 38,674 milioni mwaka 2001 hadi kufikia T.Shs. 146,200 milioni mwaka 2009/2010. Kwa maana nyengine, ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kwa takriban mara nne ya kile kiwango cha mwaka 2000.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, itaendeleza ustawi huu na katika mipango yake ya utekelezaji iliyonayo, ni pamoja na kuziba mianya yote ya uvujaji wa mapato ya Serikali.
Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010 imetuagiza kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa uwiano wa asilimia 22 ya pato la taifa. Jambo hili ni muhimu katika kukuza uchumi na kuimarisha uwezo wa Serikali wa kifedha ambalo ndilo moja ya lengo letu.
Ndugu Wananchi,
Ustawi wa uchumi uliofanywa hapo kabla umeiwezesha nchi yetu kupata maendeleo ya kuridhisha katika kugharamia mambo muhimu yaliyofanyika kwa mfano kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu. Aidha, umegharamia ustawi wa sekta za miundombinu ambazo zinachochea ukuaji wa uchumi ikiwemo ujenzi wa barabara, bandari, nishati na uwanja wa ndege wa Zanzibar. Jumla ya kilomita 1210 ya barabara za lami za kiwango cha juu zilizoipatia sifa Zanzibar zimejengwa Unguja na Pemba.
Serikali ya Awamu ya Saba itakamilisha miradi yote ya barabara iliyokwishanzishwa na kazi zinaendelea kwa kasi, kote Unguja na Pemba. Barabara zenye jumla ya kilomita 247.4 zimepangwa kujengwa katika miaka mitatu 2011/2013, zikiwa na urefu wa kilomita 152.9 kwa Unguja na kilomita 94.5 kwa upande wa Pemba. Kazi za kukamilisha ujenzi wa barabara za kilomita 108.9 huko Pemba zinaendelea.
Mkazo mkubwa utawekwa katika kuziimarisha barabara zinazounganisha maeneo ya kilimo na barabara kuu, ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo. Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaharakisha ujenzi wa barabara ndogo za vijijini na mijini Unguja na Pemba; sambamba na kuendelea kuzitunza na kuzifanyia matengenezo kila itapohitajika.
Ndugu Wananchi,
Ujenzi wa bandari kuu ya Malindi umekamilika, lakini licha ya kukamilika kwa ujenzi huo kulikofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Sita, kwa msaada uliotolewa na Umoja wa Ulaya, Serikali yenu sasa itajenga na kuziimarisha sehemu maalum za kuhudumia abiria pamoja na maeneo ya kuhifadhia makontena, Vile vile, Serikali itaendeleza mpango wa ujenzi wa bandari mpya ya mizigo katika eneo la Mpigaduri huko Maruhubi ikiwa ni miongoni mwa hatua za kuifanya Zanzibar kuwa na eneo la Bandari Huru ikiwa na lengo la kuifanya bandari hiyo kuwa ni kituo kikubwa cha biashara katika Afrika Mashariki.
Ndugu Wananchi,
Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kuongeza urefu wa barabara ya kurukia na kutulia ndege kutoka urefu wa mita 2462 hadi kufikia mita 3022 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga njia ya kupitia ndege (taxways) na eneo la maegesho (apron) ili kuziwezesha ndege kubwa kuweza kutua na kuruka bila ya msongamano.
Aidha, tutajenga jengo jipya la abiria katika uwanja huo kutokana na mkopo wa masharti nafuu uliotolewa na Exim Bank ya China. Kadhalika, tumepanga kuupanua Uwanja wa Ndege wa Pemba na kuuweka taa ili kuziwezesha ndege kutua na kuruka nyakati zote pamoja na kuweka uzio. Huduma za zimamoto na huduma zinazowahusu abiria, mizigo na ndege nazo zitaimarishwa.
Ndugu Wananchi,
Zanzibar imejipatia sifa katika Bara la Afrika kwa kuwa na mtandao wa simu wa kiwango cha juu, ukiwa na zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu wanaotumia simu ikilinganishwa na idadi ya watu wote wa Zanzibar (teledensity) kupitia kampuni tano za mawasiliano ya simu zinazotoa huduma hapa Zanzibar.
Mchango wa shughuli za mawasiliano na uchukuzi katika pato la taifa umeongezeka na kufikia asilimia 11 mwaka 2009, kutoka asilimia 8 mwaka 2008. Thamani ya huduma za shughuli hizi imefikia T.Shs. 96,800 milioni mwaka 2009, kutoka T.Shs. 59,600 milioni mwaka 2008.
Kutokana na umuhimu wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Serikali yenu itaendeleza ushirikishaji wa sekta binafsi katika kukuza na kustawisha mawasiliano ya simu na mtandao (Internet) kwa kupitia mkongo wa baharini wa mawasiliano ya haraka ‘Optic Fibre’.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika shughuli za kiuchumi, kama inavyofanywa sasa na Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na katika shughuli zote za Serikali; ili kujenga mfumo wa “E-government”; yaani uendeshaji kazi za kimawasiliano Serikalini kwa mtandao wa elektroniki. Aidha, teknolojia hiyo itatumiwa katika skuli zote za msingi na hatimae katika huduma za afya.
Ndugu Wananchi,
Mafanikio ambayo Zanzibar na watu wake hatutaweza kuyasahau ni yale ya sekta ya nishati. Zaidi ya asilimia 90 ya Shehia zote za Zanzibar zinapata huduma za umeme. Changamoto kubwa iliyopo ni uwezo mdogo walionao wananchi wengi kwa kuufikisha umeme huo majumbani mwao.
Tumeweza kuufikisha umeme Pemba kwa mashirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Norway. Waya uliolazwa chini ya bahari kutoka Pangani Tanga hadi Pemba umeikomboa Pemba kutokana na kutokuwa na umeme wa uhakika. Matarajio yetu ni kuifanya Pemba ipige hatua kubwa zaidi katika kuwaletea wananchi maendeleo na kuwa kivutio kikubwa cha watalii na wawekezaji wa ndani na nje.
Kwa upande wa Unguja tayari mradi mkubwa unaofadhiliwa na Marekani wenye lengo la kutandaza waya mpya chini ya bahari kutoka Ras Kilomoni, Dar es Salaam hadi Ras Fumba, Unguja umeanza. Mradi huu utakapokamilika, Unguja itapata Umeme wa uhakika kwa kipindi kisichopungua miaka 50 ijayo.
Aidha, tarehe 29 Julai 2010 itakumbukwa kuwa ni siku nyengine muhimu kwa historia ya Zanzibar kuhusu nishati na sekta ya umeme. Siku hiyo ulizinduliwa mradi wa majenereta ya umeme wa akiba huko Mtoni yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 25. Majenereta hayo yatatusaidia sana pale itakapotokezea hitilafu ya umeme.
Tunazishukuru Serikali za Nchi za Ulaya zikiwemo Norway, Uingereza na Sweden kwa msaada wao wa majenereta uliofanikishwa kwa kuchangiwa na fedha zetu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa niaba yenu namshukuru sana Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, kwa jitihada zake, katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la umeme Unguja na Pemba.
Ndugu Wananchi,
Kilimo ni sekta muhimu kwa ajili ya uchumi na maendeleo ya jamii. Kwanza inatoa ajira kwa asilimia 44 ya wananchi wa vijijini na asilimia 27 ya pato letu. Katika awamu hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya mapinduzi ya kilimo yakiwemo utekelezaji wa sera, mikakati na programu mbali mbali za kilimo na kuzifanyia mapitio kwa lengo la kuziimarisha na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo hadi kufikia asilimia sita (6) ifikapo mwaka 2015.
Pamoja na hayo tutaimarisha mafunzo ya kilimo kwa wakulima, tutawaendeleza wataalamu wetu pamoja na kukiendeleza Chuo cha Kilimo cha Kizimbani. Vile vile, shughuli za utafiti wa mbegu bora za mazao ya chakula, biashara na usindikaji matunda (agro-processing) zitaimarishwa.
Shamba la kilimo cha mboga mboga la pamoja baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, lilioko Bambi Wilaya ya Kati Unguja ambalo tarehe 7 Januari 2011 nililizindua rasmi ni mfano mzuri wa aina ya mashamba tunayotaka kuyaanzisha na kuyaendeleza.
Sambamba na hayo, mafunzo ya matumizi ya kanuni za kilimo bora, huduma za ugani, udhibiti wa maradhi ya mazao na wadudu waharibifu na matumizi ya zana za kisasa ikiwemo matrekta makubwa na madogo yataendelezwa. Serikali itashajiisha sekta binafsi ili ishiriki kutoa huduma za pembejeo, ugani na huduma za kifedha.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, itaimarisha uzalishaji wa mazao ya biashara hasa karafuu, nazi, matunda na mazao ya viungo. Serikali inalifahamu vizuri tatizo la wizi wa mazao kwenye mashamba na inaandaa mkakati madhubuti wa kupambana na vitendo vya wizi, ambavyo vinarudisha nyuma juhudi za wakulima.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, itaendeleza mafanikio ya kilimo cha mpunga na mazao mengine ya chakula yaliyofanywa katika Awamu ya Sita. Vile vile, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatilia mkazo kilimo hai (organic farming) na kilimo mseto kwa ajili ya kuongeza tija na kuhifadhi mazingira. Dhamira yetu ni kuwasaidia wakulima wetu walime kilimo chenye tija kwa ajili ya kuendesha maisha yao, kwa kutumia mbinu za kisasa na utaalamu.
Kilimo cha umwagiliaji maji kitatiliwa mkazo. Katika kufanikisha azma hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetayarisha Mpango Mkuu wa Umwagiliaji Maji na kuainisha mabonde 57 yenye hekta 8,521 ambazo zinaweza kutumika kwa kilimo hicho.
Hadi sasa jumla ya hekta 700 za eneo hili zimeshajengwa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na matayariso ya mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Korea. Jumla ya hekta 2000 tayari zimeshafanyiwa tathimini yakinifu.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kufanya mazungumzo na washirika wa maendeleo mbali mbali kwa lengo la kutusaidia kuendeleza sekta ya Kilimo, ili iweze kutoa mchango wake katika kukuza uchumi, kupunguza umaskini na kuwa na uhakika wa chakula.
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa uendelezaji maliasili zetu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia ulinzi na udhibiti wa misitu ya Zanzibar. Msitu wa Jozani uliopo Unguja na Msitu wa Ngezi uliopo Pemba na misitu yetu mingine ya asili kwa kushirikiana na wananchi.
Aidha, Wizara itashughulikia kudhibiti wimbi la ukataji miti ovyo unaoendelea. Halikadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na kazi za utunzaji na uhifadhi wa wanyama pori walio katika hatari ya kutoweka na kuendeleza uzalishaji wa asali kwa kushajiisha ufugaji wa kisasa wa nyuki.
Ndugu Wananchi,
Katika kuendeleza hali ya maisha na uchumi kwa wananchi, sekta za ufugaji na uvuvi zitaendelezwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao yatokanayo na bidhaa hizo.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaimarisha ufugaji wa kisasa unaozingatia ongezeko kubwa la tija kwa mifugo katika eneo dogo, hasa kutokana na uhaba uliopo wa maeneo ya malisho na haja ya kupunguza uharibifu wa mazingira.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba itawaendeleza wafugaji wadogo wadogo kwa kuwapatia mbegu bora za mifugo na mitamba kwa kupitia mpango wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe. Kadhalika, itaendeleza vituo vya huduma (farm service centres) na huduma za kinga na tiba ya mifugo ikiihusisha sekta binafsi.
Mapinduzi yetu ya uvuvi yataimarisha uvuvi wa kisasa unaozingatia uhifadhi wa mazingira ya bahari na kukuza kipato cha wavuvi, kuandaa sera mpya ya uvuvi na kusimamia utekelezaji wa sheria ya uvuvi.
Vile vile, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwahamasisha wavuvi, kuanzisha na kuendeleza vikundi vya ushirika na kutumia maarifa ya kisasa na zana bora za uvuvi kwa kuwapatia misaada na mikopo ya zana hizo na kuwawezesha kuvua kwa ufanisi na pia kufuga samaki na viumbe vyengine vya baharini kwa ajili ya biashara.
Lengo la Serikali ni kuhamasisha uvuvi kwa kulenga soko la viwanda. Wakati huo huo, Mpango Shirikishi wa Kuyaendeleza matumizi ya Bahari Kuu na kuendeleza Maeneo ya Hifadhi ya Bahari (MPAs) yakiwemo maeneo mapya ya Tumbatu, Chumbe-Bawe, Menai, MIMCA na PECCA utaendelezwa.
Ndugu Wananchi,
Msukumo mwengine wa uchumi wetu ni Biashara na Viwanda. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba imeiunda upya Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ili iweze kutoa mchango wake ipasavyo katika kuinua uchumi na ustawi wa wananchi wa Zanzibar kupitia sekta hizo.
Ili kuweza kuzalisha na kusafirisha bidhaa zaidi nchi za nje na hatimae kuondoa nakisi katika urari wa biashara, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatekeleza Mkakati wa Taifa wa Usafirishaji (Zanzibar National Export Strategy) na mpango kazi wa utekelezaji wa mkakati huo.
Vile vile, sheria ya Viwango ya Zanzibar ambayo itawasilishwa katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi hivi karibuni kwa lengo la kuinusuru Zanzibar kugeuzwa kuwa sehemu ya kuletwa bidhaa hafifu zisizokuwa na viwango vya kimataifa na kuhakikisha kuwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar zinatimiza viwango vya kimataifa. Hivi sasa Serikali inatazama uwezekano wa kuifanya Zanzibar kuwa eneo Tengefu la Kiuchumi (Special Economic Zone).
Sheria ya biashara ya mwaka 2006 itafanyiwa mapitio ili kuondoa upungufu na mfumo bora zaidi wa utoaji wa leseni za biashara utawekwa. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itawashajiisha wawekezaji ili waje kuwekeza. Wajasiriamali wadogo na wa kati watapatiwa fursa za mafunzo na nyenginezo ili waweze kuzalisha bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Kuhusu masoko, Wizara itawasaidia wafanyabiashara na wazalishaji wadogo wadogo ili waweze kushiriki katika maonesho mbali mbali ya biashara kwa kuzitangaza bidhaa zao na kuzitafutia masoko mapya. Uwanja wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa unatarajiwa kujengwa katika maeneo ya Dimani, Unguja katika eneo lililotengwa kwa ujenzi huo ambalo lina ukubwa wa hekta 60.
Ili kuimarisha zaidi Sekta ya Viwanda, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kutayarisha Mkakati wa Mpango wa Maendeleo ya Viwanda pamoja na kufanya tathmini ya Sera ya Viwanda sambamba na kujenga na kuimarisha sekta binafsi na kuweka mazingira mazuri zaidi ya ushirikiano na Sekta ya Umma (Public Private Partnership).
Tutasimamia utafiti utakaowezesha usarifu wa zao la karafuu kutengeneza dawa pamoja na aina nyengine za matumizi ya zao hilo kwa kutumia kiwanda cha makonyo kilichopo Chake Chake Pemba, ili kuzidisha thamani ya zao hilo.
Ndugu Wananchi,
Katika huduma za uchumi ipo sekta ya utalii ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya sita imeiendeleza vyema hasa katika miundombinu. Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba tutazidi kuimarisha na kujenga uwezo wa wazalishaji na watoa huduma ili kukidhi haja na viwango vya soko hilo. Sekta nyenginezo za uchumi ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, viwanda vidogo vidogo na vya kati zitapewa msukumo maalum ili ziweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya sekta hii.
Pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria na Mpango Mkuu wa Utalii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasisitiza kuwepo kwa utalii wenye kuheshimu mila, desturi, silka na utamaduni wa Mzanzibari.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo itaendeleza jitihada za kuitangaza Zanzibar katika masoko mapya hasa katika nchi za Asia, sambamba na kuimarisha maeneo ya kihistoria ili kuongeza mapato katika sekta hii.
Wakati huo huo, tumeandaa mpango wa kuwapa taaluma vijana ili wawe na uwezo wa kuajiriwa katika makampuni ya utalii ya nje na ndani ya nchi na pia uwezo wa kujiajiri wenyewe katika nyanja mbalimbali.
Ili kufikia azma hiyo, Chuo cha Maendeleo ya Utalii kitaimarishwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi na viwango vya masomo vitapandishwa kutoka cheti cha msingi na kati na kufikia cheti kamili na Stashahada ya Uendeshaji Utalii na Mahoteli, ambavyo vinatambuliwa na Shirika la Kimataifa la Elimu ya Hoteli na Utalii.
Mpango huu unatarajiwa kufanyika kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).
Tutaendelea kuchukua hatua za kutoa elimu ya utalii kwa wananchi ili kupunguza athari za utalii kwa jamii na mazingira pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa watalii na mali zao.
Ndugu Wananchi,
Katika utekelezaji wetu wa Ilani, MKUZA, DIRA na Malengo ya Milenia, imeundwa Wizara mpya ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, ili ikidhi mahitaji ya mipango ya kuwaendeleza wananchi kiuchumi.
Mbali na michango mingi iliyotolewa na Serikali ya awamu iliyopita kupitikia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imo mbioni kuandaa awamu ya tatu ya mradi huo kwa lengo la kuwaimarisha zaidi wananchi kiuchumi na kusambaza huduma za jamii kila pembe ya visiwa vyetu.
Vile vile, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kukuza uwezo wake wa kutoa mikopo kwa wananchi na kuwawezesha kutumia fursa zilizopo katika maeneo wanayoishi ili kujiendeleza kiuchumi.
Sambamba na kuimarisha mifuko hiyo, Wizara hii mpya itawashajiisha wananchi kuanzisha na kuviendeleza vikundi vya ushirika na SACCOS hasa kwa vijana na wanawake pamoja na kuendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali. Maeneo maalum ya kufanyia biashara ndogo ndogo, yatatayarishwa pamoja na kuimarisha mfumo na taratibu za utoaji leseni za biashara wenye kuzingatia usafi wa miji na hifadhi ya mazingira na kutambua rasilimali za biashara za wanyonge ambazo zipo katika sekta isiyo rasmi.
Ndugu Wananchi,
Baada ya kuzungumzia hali ya mafanikio ya uchumi na huduma za kiuchumi, sasa kwa ufupi nitazungumzia mafanikio katika sekta za huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu na maji safi na salama yaliofanyika pamoja na mipango ya sasa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba.
Kwa upande wa afya, mafanikio makubwa yamepatikana katika kuimarisha huduma za tiba na kinga. Mapambano dhidi ya malaria kupitia mpango wa “Kataa Malaria” uliotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani chini ya uongozi wa Mfuko wa Rais wa nchi hiyo na mashirika ya kimataifa kama WHO na UNICEF yamefanikiwa.
Takwimu za tafiti mbali mbali zilizofanyika kuanzia mwaka 2007 hadi 2010 zinaonesha kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa kwa ugonjwa huo katika maeneo yote ya Unguja na Pemba. Kiwango cha maambukizo ya malaria kwa sasa ni wastani wa mtu mmoja kwa kila mia moja ikilinganishwa na wastani wa watu arobaini kwa kila mia moja mwaka 2005.
Hatua ya sasa ni kumaliza kabisa malaria kwa kutumia njia mbali mbali za kitaalamu na hivi karibuni mzunguko wa sita unyunyizaji dawa za kuua mbu wa malaria zitaanza Unguja na Pemba. Natoa wito kwa wananchi washiriki kikamilifu katika kufanikisha mpango huu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia iliyokuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imefanikiwa kugawa vyandarua vyenye dawa kwa Wilaya saba kati ya kumi na mpango huo bado utaendelezwa.
Maendeleo mengine katika sekta hiyo ya afya ni pamoja na mradi wa afya ya uzazi wenye lengo la kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto wachanga, ambao tutauendeleza kwa lengo la kupata mafanikio zaidi. Hadi sasa, mafanikio yaliyopatikana ni kupungua kwa vifo vya watoto wachanga kutoka 61 kwa kila vizazi hai 1,000 (61/1,000) mwaka 2004/5 hadi 54/1,000 mwaka 2008.
Aidha, vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 101 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2004/5 (101/1,000) hadi 79/1,000 mwaka 2007/8. Sambamba na hayo, vifo vya akinamama vinavyotokana na uzazi vimepungua kutoka 377 kwa kila 100,000 mnamo mwaka 1998 (377/100,000) hadi 279/100,000 mwaka 2009. Lengo la MKUZA ni kufikia idadi ya 251/100,000 mwaka 2010.
Katika kuzuia maambukizo ya maradhi mbali mbali, mpango wa chanjo kwa watoto umeendelezwa kwa kuwapatia chanjo, asilimia 87, ya watoto wa umri wa miaka mitano. Jitihada hizi zitaendelezwa ili kuwawezesha watoto kujikinga na maradhi mbali mbali.
Serikali yetu imekusudia kuendeleza kwa nguvu mpango huo na mengine ya huduma za afya. Hii ni sababu moja ya kuiondolea Wizara ya Afya majukumu ya sekta ya ustawi wa jamii ili iweze kushughulikia sekta ya Afya kikamilifu. Afya bora kwetu sisi ni Maisha Bora na ni haki ya kila mwananchi.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, itahakikisha kwamba huduma za tiba na kinga zinaimarishwa kote Unguja na Pemba na inakamilisha utaratibu ulioandaliwa na Awamu ya Sita wa kuifanya Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja kuwa ya Rufaa.
Kadhalika Serikali itazipandisha daraja Hospitali za Abdulla Mzee na ya Wete huko Pemba kwa ajili ya kufikia hadhi za Hospitali za Mkoa, pamoja na kuzipa hadhi ya Wilaya Hospitali za Vitongoji na Micheweni kwa upande wa Pemba, Makunduchi na Kivunge kwa upande wa Unguja.
Aidha, Serikali ina lengo la kuanzisha kitengo cha kutoa huduma za utibabu wa maradhi ya saratani, huduma za utibabu wa maradhi ya figo na maradhi ya moyo. Vile vile, huduma za tiba asili zitapewa msukumo mkubwa katika sehemu zote za Unguja na Pemba.
Ndugu Wananchi,
Lengo letu katika sekta ya Afya ni kufikia Malengo ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM ya mwaka 2010/2015, Malengo ya Milenia, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 na MKUZA. Ili tuweze kufikia lengo hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, inatilia mkazo mkubwa elimu na mafunzo ya afya.
Tunakiendeleza Chuo cha Sayansi ya Afya cha Mbweni, kwa kukipanua Chuo hicho kwa kuongeza idadi ya wanafunzi, kuwaongeza walimu wa kufundisha masomo ya fani mbali mbali kwa kiwango cha Shahada. Kadhalika, chuo chetu cha madaktari kinachoendeshwa kwa mashirikiano ya Serikali ya Cuba nacho kitaendelezwa kwa lengo la kupata madaktari wengi katika kipindi kijacho. Wakati huo huo, tutaendeleza mafunzo kwa wafanyakazi wa sehemu mbali mbali za Wizara ya Afya ili waweze kutoa huduma bora.
Ndugu Wananchi,
Juhudi za kupambana na janga la UKIMWI zinaendelea Unguja na Pemba na ni vyema wananchi wakatambua na kukubali kuwa UKIMWI upo na ni tishio kwa maisha ya mwanadamu. Tathmini ya kasi ya maambukizo ya Wazanzibari kwa jumla inaonesha kwamba maambukizo yapo katika kiwango cha asilimia 0.6 ambayo ni wastani wa watu 7,200 tangu UKIMWI ulipobainika Zanzibar 1986.
Hadi sasa wagonjwa 4,908 wamesajiliwa katika kliniki 8 za huduma za tiba za Unguja na Pemba, sawa na asilimia 68.1 ya watu wanaokadiriwa kuishi na Virusi Vya UKIMWI (VVU). Jumla ya watu 2,498 wameshaanzishiwa tiba ya ART, hii ni sawa na asilimia 50.9, kati ya wagonjwa waliosajiliwa kwenye kliniki nane, wagonjwa 209 wamefariki dunia.
Miongoni mwa changamoto zinazopelekea utumiaji mdogo wa huduma za tiba dhidi ya maambukizo ya Virusi Vya UKIMWI ni kiwango kikubwa cha unyanyapaa, matumizi ya tiba mbadala, uhaba wa elimu na lishe isiyotosheleza kwa waathirika.
Natoa wito kwa wananchi Unguja na Pemba kuendelea kujitokeza kuchunguzwa katika vituo vya upimaji wa hiyari vya Serikali na vile vya binafsi. Aidha, kwa wale ambao wameambukizwa waende katika vituo vya ushauri nasaha vilivyopo Unguja na Pemba kwa ajili ya kupata huduma. Tutaendelea kushirikiana na taasisi za Kimataifa na jumuiya za kiraia katika kudhibiti kuenea kwa UKIMWI.
Maabara ya Mkemia Mkuu itaimarishwa kwa kupatiwa nyenzo, vifaa na wataalamu wenye ujuzi na kuifanya kuwa Idara kamili inayojitegemea, ili iweze kudhibiti na kupambana na uingizwaji na uuzaji wa bidhaa hafifu au zilizomalizika muda wake wa matumizi kwa madhumuni ya kuzilinda Afya za wananchi.
Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya awamu zilizopita, tokea Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ni ustawi wa elimu nchini; sekta hiyo imepiga hatua kubwa zaidi katika awamu ya chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Taasisi za elimu zikiwemo skuli za maandalizi, msingi, sekondari na vyuo zimeongezeka kutoka 325 mwaka 2000 na kufikia 624 (zikiwemo 272 za watu binafsi) mwaka 2009. Vyuo vya ualimu vimeongezeka kutoka viwili (2) mwaka 2000 na kufikia vitatu (3) mwaka 2009 na Vyuo Vikuu sasa vipo vitatu (3) baada ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar mwaka 2002.
Katika kukuza na kuimarisha mafunzo ya sayansi na teknolojia nchini, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia kuanzia mwezi wa Septemba 2009.
Pamoja na juhudi hizo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa itatekeleza uimarishaji na ubora wa elimu hasa katika skuli za sekondari, kufundisha walimu wengi wa kiwango cha Shahada, pamoja na upatikanaji wa vitabu vya kusomea, vifaa vya mafunzo na maabara kwa ushirikiano na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la USAID. Kwa sasa kila mmoja kati ya wanafunzi 82,802 waliopo skuli za sekondari ana kitabu chake mwenyewe cha masomo ya Hisabati na Sayansi.
Ndugu Wananchi,
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ni muhimu sana ili kuelimisha na kuhamasisha jamii katika masuala mbali mbali ya kiuchumi, maendeleo, demokrasia na utawala bora.
Kwa kutambua umuhimu wa wizara hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba, itasimamia utekelezaji wa Sera ya Habari, Sheria, Kanuni na miongozo ya Habari, ili tuweze kuongoza kwa ufanisi zaidi na kuleta mageuzi ya utangazaji nchini ikiwemo kuongeza uhuru wa vyombo vya habari. Pia, itashughulikia mradi wa mageuzi ya teknolojia kutoka “analogue” kwenda “digital” ifikapo mwaka 2012.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaviimarisha vyombo vyake vya habari ikiwemo kukifanyia matengenezo makubwa Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na kukipatia mitambo mipya ya uchapaji na vifaa vya kisasa.
Katika siku zijazo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelenga kuziunganisha Sauti ya Tanzania Zanzibar na Televisheni Zanzibar kuunda Shirika la Utangazaji la Zanzibar. Vile vile, studio mpya za kurushia matangazo ya televisheni Zanzibar zinatarajiwa kujengwa katika eneo la Tunguu kwa lengo la kuiwezesha televisheni Zanzibar kwenda sambamba na teknolojia mpya ya habari.
Kwa upande wa sekta ya Michezo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia sera na sheria za michezo na utamaduni pamoja na kuhimiza matumizi ya sanaa katika kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu masuala mbali mbali ya maendeleo.
Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Sita, ilifanya kazi kubwa ya kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa huduma wa maji safi na salama mijini na vijijini Unguja na Pemba. Awamu ya kwanza ya Mradi mkubwa wa maji uliosaidiwa na Serikali ya Japan umekamilika na sasa Serikali inashughulikia Awamu ya pili ya upatikanaji maji Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuweka mabomba mapya ili wananchi wapate maji vizuri na kwa uhakika.
Kwa hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo katika Manispaa ya Zanzibar kwa mashirikiano na Serikali ya Japan na utakapokamilika utaweza kuwanufaisha wananchi 460,000 katika Mkoa wote.
Kwa upande wa Pemba, mradi mkuba wa maji wenye kujumuisha uchimbaji wa visima, ujenzi wa matangi na ufungaji wa mabomba makubwa katika miji ya Wete, Chake Chake na Mkoani ulioanzishwa mwaka 2010, Serikali itasimamia utekelezaji wake. Mradi huu unatekelezwa kwa mashirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na utawanufaisha zaidi ya wakaazi 90,000 wa miji hiyo. Kwa upande wa Unguja Mradi wa ADB utawanufaisha wananchi wa Shehia mbali mbali za Wilaya ya Kati.
Ndugu Wananchi,
Baada ya hayo, leo napenda kuzungumzia kwa ufupi mambo mawili yanayoathiri ustawi wa jamii yetu, nayo ni uharibifu wa mazingira na dawa za kulevya, ambayo yanaratibiwa na Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais.
Uharibifu wa mazingira umefanyika baharini, mashamba na mijini. Tunaona jinsi miti inavyokatwa ovyo hata kuhatarisha vianzio vya maji kukauka na pia mchanga kuchimbwa kila pahala.
Vile vile, tunashuhudia kuzidi kwa uchafu wa taka mitaani ambao unahatarisha afya za wananchi. Haya ni mambo ambayo tunapaswa kushirikiana ili kuyadhibiti na kuyaondoa. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuimarisha ukaguzi wa maeneo ya makazi na sehemu za kazi. Lakini viongozi kama madiwani na masheha wachukue jukumu la kuwashirikisha wananchi katika kuyatunza mazingira. Serikali inalipa uzito suala hilo na haitovumilia uharibifu huo uwe unaoendelea.
Suala la matumizi ya dawa ya kulevya ni nyeti sana na limekuwa likishughulikiwa kwa nguvu zote na awamu zilizopita. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba itaendelea kulisimamia kwa kushirikiana na wahusika mbali mbali, ili tufanikiwe kupiga vita matumizi ya biashara ya dawa hizo zinazowaathiri zaidi vijana wetu kila kukicha.
Ndugu Wananchi,
Nakushukuruni sana kwa kunisikiliza katika maelezo yangu ya mafanikio ya awamu zilizopita na mipango ya awamu ya saba kuyaendeleza. Sasa napenda kuchukua nafasi hii kuzungumzia juu ya uwajibikaji wa Serikali yenu kwenu wananchi katika kuijenga Zanzibar mpya yenye neema.
Tunayo maeneo matatu makubwa katika kufanikisha hayo, nayo ni: amani, utulivu na mshikamano na umoja; utumishi wa umma na utawala bora; Muungano wetu.
Katika suala la amani na utulivu, nchi yetu katika kipindi cha hivi karibuni imejipatia sifa kubwa hasa baada ya kumaliza uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, 2010 kwa salama na amani, Uchaguzi uliokuwa huru na wa haki na uundwaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Napenda nielezee furaha yangu kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa imeanza kazi zake vizuri sana na inaendelea na majukumu yake kwa ufanisi na mafanikio yanayotarajiwa. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Makamo wangu wawili, ambao ndio Wasaidizi na Washauri wangu wakuu, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais.
Ninakushukuruni kwa ushauri wenu, jitihada zenu jinsi mnavyofanyakazi na mnavyonisaidia. Ahsanteni sana. Tutafanyakazi ya kujenga na kuitumikia Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kuwatumikia wananchi kwa pamoja, ushirikiano na masikilizano.
Wito wangu kwenu wananchi ni kufuata mwenendo wetu huu ili watu wawe na umoja, upendo na mshikamano na nchi iwe na amani, utulivu na maendeleo. Kadhalika, napenda niwashukuru Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu na Viongozi wote wa Serikali kwa kufanyakazi kwa bidii. Napenda nikuhakikishieni wote wameanza vizuri na kwa kasi kubwa.
Nchi yetu sasa ipo shwari na wananchi wote wanafurahia matunda ya amani na utulivu, ambayo yanatokana na umoja na mshikamano tulionao. Wajibu wa kila mmoja wetu ni kuendeleza na kukuza imani na moyo huo. Ni lazima tuheshimu na tudumishe amani na utulivu ndani ya nchi yetu na tusikubali kwa yoyote kutuvunjia hali hiyo, ambayo zipo nchi zinaitamani, lakini bado hazijabahatika kuwa nayo.
Maendeleo na mafanikio ya mipango niliyotaja itawezekana tu, ikiwa umoja na mshikamano wetu na tutaudumisha, amani na utulivu itaendelea kushamiri siku zote.
Ndugu Wananchi,
Jambo jengine ninalopenda kusisitiza ni suala la Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali yetu yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa imelenga katika kustawisha hayo mawili na kwa umuhimu huo ndio maana ikaanzishwa Afisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Utawala Bora unafungamana na wananchi kupatiwa haki zao bila ya upendeleo au ubaguzi na kupata huduma bora kutoka idara na taasisi za Serikali. Katika utekelezaji wa utawala bora, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeamua kulishughulikia suala la maadili ipasavyo.
Suala hili linamhusu kila mmoja wetu, kuanzia viongozi waliochaguliwa, walioteuliwa pamoja na watumishi. Huduma bora yenye kutolewa kwa misingi ya uadilifu ni haki ya wananchi wote. Ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma nzuri na kwa uadilifu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, itatekeleza mpango mkubwa wa mabadiliko katika utendaji wa utumishi wa umma, kwa kuziimarisha huduma zinazopaswa kutolewa na kuleta ufanisi mkubwa makazini.
Katika mabadiliko haya Serikali imeandaa Sheria mpya ya Utumishi wa Umma yenye lengo la kuleta ufanisi kazini, kuwatumikia wananchi bila ya upendeleo au bugdha na kuzitatua kero zao kwa wakati na huku wafanyakazi nao wakipata haki zao kutokana na kutimiza wajibu wao. Sheria hio mpya inatarajiwa kupelekwa Baraza la Wawakilishi hivi karibuni.
Kuanzia wiki ya mwanzo hadi wiki ya mwisho wa Disemba,2010, Mimi na Viongozi wenzangu Serikalini tulifanya mazungumzo na viongozi na watendaji wakuu wa Wizara mbali mbali, ili kusikiliza mipango yao ya kazi na jinsi wanavyoendesha shughuli zao.
Zoezi hilo limekuwa na mafanikio na sasa ni jambo la kutia moyo kwamba watendaji wamepata ari mpya kazini baada ya kupewa maelekezo na maagizo ya kutekeleza mipango ya kazi zao. Matumaini yangu ni kuwa wafanyakazi watafaidika na matunda ya zoezi hilo na kuona mabadiliko katika utoaji huduma.
Serikali itaendelea kuheshimu haki za binadamu, uhuru na haki za raia na kutekeleza misingi ya demokrasia. Kadhalika wananchi nao wataendelea kuzingatia haki zao na kuendelea kuwa na utamaduni wa utiifu kwa kufuata sheria za Serikali yao ili jamii idumu katika amani na utulivu.
Ndugu Wananchi,
Jambo la tatu ni kuhusu Muungano wetu. Juhudi kubwa zimeendelea kuchukuliwa katika kuuimarisha Muungano wetu na kuzishughulikia kero zilizojitokeza, ingawa bado zipo changamoto chache zilizotukabili lakini zinashughulikiwa.
Kamati ya pamoja ya Serikali zetu mbili inayoshughulikia kero za Muungano inayoongozwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kukutana na kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi mkubwa.
Napenda kumshukuru na kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kusimama kidete katika kuutetea na kuuendeleza Muungano wetu na kwamba siku zote yuko tayari kuzizungumzia changamoto zinazoukabili Muungano wetu na kutafuta njia za kuzipatia ufumbuzi kila zinapotokea.Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuudumisha Muungano kwa manufaa ya nchi zetu mbili.
Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia nachukuwa fursa hii kuzipongeza nchi marafiki, washirika wetu wa maendeleo ambao wamekuwa wakifanyakazi pamoja na Zanzibar na kutusaidia katika harakati mbalimbali za kuleta maendeleo ya nchi yetu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaimarisha uhusiano huu kwa madhumuni ya kuendeleza ushirikiano wa wahusika mbali mbali wa maendeleo katika juhudi zetu za kuijenga nchi yetu na kuwaletea wananchi maendeleo ambayo ni endelevu.
Kwa mara nyengine tena napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwenu wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010 kwa amani, utulivu na usalama mkubwa. Nakushukuruni kwa kuhudhuria sherehe hizi kwa wingi sana.
Vile vile, naishukuru Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya kutimiza miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kwa juhudi kubwa walizofanya hadi kufanikiwa kwa sherehe hizi.
Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie mafanikio makubwa katika azma yetu ya kuijenga na kuiendeleza Zanzibar.
Nakutakieni Maadhimisho mema na Kheri ya Mwaka Mpya wa 2011.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
MAPINDUZI DAIMA
Mungu Ibariki Zanzibar
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika

0 comments:
Post a Comment