
HATIMAYE Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesikia kilio cha mashabiki kuhusu viingilio kwa kupanga viwango vya chini zaidi katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN 2012) kati ya timu ya taifa, Taifa Stars itakayocheza dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Awali, mashabiki walikuwa wakilalamikia tabia ya mara kwa mara ya TFF kuweka viingilio vya juu kama vile vya Stars dhidi ya Brazil vilivyoanzia Sh.30,000 hadi Sh.300,000 na matokeo yake uwanja ukakosa mashabiki. Lakini sasa, viingilio vimewekwa vya chini ili Watanzania wengi zaidi wafike uwanjani na kuishangilia Stars.Akizungumza na waandishi wa habari jana, Afisa Habari wa TFF, Florian Kaijage, alisema kuwa kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 5,000 kwa jukwaa la kijani huku kiingilio cha juu zaidi kikiwa Sh. 30,000 kwa jukwaa la viti maalum (VIP A)."TFF imeweka viingilio hivi kwa kuamini kuwa Watanzania wengi watavimudu na kufanya uwanja ufulike na kuishangilia vyema timu yetu," alisema Kaijage.Aliongeza kuwa viingilio vingine ni Sh.7,000 kwa viti vya rangi ya bluu huku Sh.10,000 kwa viti vya rangi ya machungwa vilivyopo nyuma ya magoli pamoja na mkabala na jukwaa kuu.Alisema viti vya VIP C itakuwa Sh. 15,000 na viti vya jukwaa la VIP B litalipiwa Sh. 20,000.
0 comments:
Post a Comment