Mwenyekiti wa wazee waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nathaniel Mlaki akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam baada ya kujisalimisha katika ofisi ya kamanda wa Kanda maalum, Suleiman Kova (kulia) Picha Na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi..
KIONGOZI wa wastaafu wa jumuiya ya zamani ya nchi za Afrika Mashariki( EAC), Nathael Mlaki amejisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi ambako anahojiwa dhidi ya tuhuma za kutoa taarifa za upotoshaji kuwa mmoja wa wastaafu hao alifariki dunia kutokana na kipigo cha polisi.Mzee anayedaiwa kufariki akiwa mikononi mwa polisi, Anderson Msuta (70) alipatikana mwishoni mwa wiki akiwa kwa mwanaye na aliwaeleza waandishi wa habari kuwa habari hizo za kuzushiwa kifo zilimshangaza na kumsababishia usumbufu. Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es salaam, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kutokana na uzito wa suala hilo, uchunguzi wa kina umefanyika na maamuzi yatapatikana baada ya kumfikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
“Mimi nilitangaza kifo cha mzee huyo bila kuthibitisha, lakini nilitoa taarifa hizo baada ya kupokea kutoka kwa wezangu kwa kuwa kazi yangu kama kiongozi ni kupokea taarifa na kutoa kwa umma ndivyo nilivyofanya nikiwa na lengo la kutaka kusaidiwa matatizo yetu wazee wale,’’ alisema Mlaki.
Kutokana na kauli hiyo kiongozi huyo aliliomba radhi Jeshi la polisi, familia ya mzee Msuta na wananchi kwa ujumla kwa kosa alilolifanya huku akidai kuwa kuna watu wanaowachonganisha wazee hao wastaafu na jeshi hilo. “Sisi hatuna matatizo na Jeshi la polisi kwa kuwa linatusaidia mara kwa mara, lakini tatizo lipo kwa wale wanaochelewesha mafao yetu ndiyo wanaotuchonganisha na jeshi hilo ili tuonekane watukutu;
“Nimekuja kujisalimisha kwa kuwa taarifa zilitolewa kwenye vyombo vya habari hivyo nikajisalimisha kama nilivyotakiwa.’’ aliongeza kiongozi huyo Wastaafu hao ambao wamekuwa wakifufua vita yao na serikali kila mara, walifunga barabara ya Kivukoni Front Jumatano iliyopita baada ya Jaji Njengafibili Mwaikugile kujitoa kwenye kesi yao kwa maelezo kuwa ana maslahi kwenye shauri hilo.
Siku hiyo, wastaafu hao walitarajia kuwa Jaji Mwaikugile angetoa hati ya kuiamuru serikali iwalipe haki zao, lakini wakakumbana na uamuzi wa kujitoa ambao uliwakera wakaamua kulala katikati ya barabara hiyo iliyo jirani na ofisi nyingi za serikali, ikiwemo Ikulu.
Kitendo chao kilisitishwa na polisi wa kutuliza ghasia ambao walifika na gari lenye maji ya kuwasha ili kuwatawanya wazee hao ambao wanadai stahili zao walizotakiwa kulipwa wakati jumuiya hiyo ikivunjwa mwaka 1977. Habari za vurugu za wazee hao zilikuwa mbaya zaidi baada ya kutokea taarifa kuwa mmoja wao aliuawa akiwa mikononi mwa polisi.
0 comments:
Post a Comment