Social Icons

Thursday, October 28, 2010

KAZI ZETU, VIBURUDISHO VYETU, IMANI YETU

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wakiwa katika shughuli zao za kila siku.

KITAMBO kidogo, kabla utandawazi haujaingia nchini, maisha yalikuwa yanakwenda ‘kibubu-bubu’ kiasi kwamba mtu aliweza kufanya tukio la kushangaza mahali fulani lakini lisisikike popote.

Lakini kwa dunia ya leo, hilo haliwezekani, kwani kama utapigwa kofi kimyakimya na mkeo ndani ya nyumba, si ajabu kesho jambo hilo ukalikuta gazetini! Ndivyo maisha ya sasa yalivyo.

Kumekuwa na kawaida moja ya watu kupitia sehemu kadhaa za viburudisho baada ya kazi zao kwa ajili ya kupumzisha akili na kuchangamsha damu, lakini ndani ya hayo yote kuna jambo ambalo limekuwa likiwachanganya wengi na kuwaacha kwenye maswali lukuki yasiyo na majibu.

Hili ni lile linalohusu aina ya burudani wanayokutana nayo pindi wanapoamua kuwa ‘bize’ na kukonga nyoyo zao kwa vinywaji katika ‘viwanja’ mbalimbali vya starehe.

Siku hizi, si ajabu kuingia kwenye baa au sehemu fulani ya kinywaji na kukutana na sauti kubwa ya muziki wa Injili ukiporomoshwa eneo hilo ilihali si mahala pake sahihi.

Hii imekuwa ikiwachanganya watu wengi ambao wanaingia maeneo hayo kujiachia, lakini sasa cha ajabu watu hao wakiwa bado hawajakolea ‘ulabu’ huanza kuhoji kwa maswali mfululizo kuhusu hatua hiyo ya kupigiwa muziki wa Injili ambao kwa asilimia mia moja unamtukuza Mungu.

“Wewee! Mbona unatuwekea nyimbo za dini hapa kwani tuko kanisani? Acheni mambo hayo jamani la sivyo tutaondoka!” watu husikika wakisema maneno hayo kila mara.

Lakini dakika chache baadaye, pale kinywaji kinapokuwa kimeshakolea haohao waliokuwa wakiponda kwa kelele ndiyo wanakuwa mstari wa mbele kuziomba ama kuinuka kwenda kucheza hasa pale DJ anapoamua kuzipa nafasi nyimbo hizo. Hakika hii ni ajabu!

Haya, lakini hayo ni yao na starehe zao. Turudi kwenye mada ya msingi. Suala la upigwaji wa nyimbo za dini kwenye sehemu za starehe kama baa na kadhalika ni kutokuelewa maana halisi ya muziki huo. Au, je, hiyo ndiyo sehemu sahihi kwa ajili ya kuwakomboa waliopotea?

Hakuna hakika kamili. Hata hivyo, mnaojua maana mtatuambia, lakini kwetu sisi tunaona kama ni hali ya kutokuthaminiwa kwa muziki wenyewe. Mbona hatujawahi kusikia kaswida ikipigwa sehemu kama hizo?

Kumbukeni lengo si kurushiana kashfa na lugha chafu, tunachokitafuta ni maana halisi na ukweli juu ya uhalali wa kupigwa kwa nyimbo hizo sehemu ambazo lugha kutoka Maandiko Matakatifu inasisitiza kwamba ni haramu.

0 comments: