Social Icons

Saturday, October 23, 2010

FEMACT WALAA NI TISHIO


Muungano wa mashirika 50 yanayotetea Usawa wa Kijinsia, Haki za Binadamu, Maendeleo na Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi (FemAct) jana ulitoa kauli ya kulaani vikali tishio la serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Seth Kamuhanda kutishia kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mwanahalisi kwa madai kuwa yanaandika habari za uchochezi dhidi ya serikali iliyoko madarakani.
Tamko hilo la pamoja, lilitolewa katika mkutano wa wanachama wa FemAct na waandishi wa habari, uliofanyika katika Makao Makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Mabibo jijini Dar es Salaam na kusomwa na Francis Kiwanga, mwanaharakati kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
FemAct wamesema kuwa madai hayo ya serikali kwa magazeti ya Mwanahalisi, Mwananchi na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) hayana msingi, ni kinyume na katiba ya nchi, uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu na kuitaka serikali iache kutoa vitisho kwa wanaharakati na waandishi wa habari kwani wana kazi kubwa ya kuhakikisha Tanzania inapata viongozi bora na kuendelea kuongozwa kidemokrasia.
“Serikali iache kutishia waandishi wa habari, mashirika ya kijamii na mtu mmoja mmoja katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa madai kuwa wanaingilia masuala ya kisiasa. Wananchi wana haki ya kutoa maoni na mawazo mbadala kwa maslahi ya taifa,” alisema Kiwanga.
Pia walizidi kutanabaisha kuwa wananchi wanapaswa kuwa makini na viongozi wanaotaka kutumia nguvu nyingi kuziba midomo ya Watanzania kuelekea uchaguzi mkuu hapo Oktoba 30 mwaka huu. Katika tamko hilo, pia walilaani vikali kitendo cha serikali kuifungia redio SAUT FM inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, jijini Mwanza na kuongeza kuwa wao (FemAct) wanaangalia namna ya kukisaidia kituo hicho cha redio kupata haki yake.
Hivi karibuni, serikali ilitoa kauli ya vitisho kwa wanaharakati wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake ‘TAMWA’ ya kuwataka wasizungumzie masuala ya uchaguzi na kutishia kuyafungia magazeti ya Mwanahalisi na Mtanzania kwa madai kuwa yanaandika habari za uchochezi dhidi ya serikali iliyoko madarakani.

0 comments: