Social Icons

Tuesday, July 13, 2010

Shigongo aongea na Watanzania Marekani

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, Eric Shigongo ameongea na Watanzania waishio nchini Marekani na kuwataka kuchangia maendeleo ya Tanzania na kuwa na mtizamo mwingine kuhusu nchi yao.

Akihutubia katika mkutano wa Diaspora 2010 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Marriot Hotel, Minneapolis nchini Marekani wiki iliyopita, Shigongo alisema mafanikio hayawezi kupatikana nchini Marekani peke yake kama ambavyo vijana wengi wanadhani, bali palipo na nia kila kitu kinawezekana mahali popote bila kujali historia ya mtu wala kiwango cha elimu alichonacho.

Aliwataka vijana walioko nje kubadilisha mtazamo wao kuhusu Tanzania kwani wengi wao wamekuwa na fikra hasi kuhusu nchi yetu na wamekata tamaa.

“Ni kweli inawezekana baadhi ya mambo yanayofanywa na watu wachache nchini yanavunja mioyo na kukatisha tamaa, lakini, je, ndiyo tuache mambo yaendelee yalivyo au tuyaweke yanapotakiwa kuwa? Ni kosa kubwa sana kuikatia tamaa nchi yetu wenyewe.

“Mungu alituweka pale (Tanzania) kwa makusudi, hivyo ni lazima kila mmoja wetu, mkubwa kwa mdogo kuhakikisha tunachangia maendeleo ya nchi yetu hata kama ni kwa kutonyamazia maovu yanayofanywa na wachache, lazima tuwe tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya vizazi vijavyo kama walivyofanya walioishi kabla yetu ambao hata majina yao hayatajwi katika historia,” alisema Shigongo.

Aidha, aliwataka vijana kufumbua macho na kuziona nafasi tele za kufanikiwa zilizopo nchini mwetu badala ya kupishana na Wachina pamoja na Wazungu uwanja wa ndege wakija kuchukua kila kitu ambacho kingewafaa Watanzania.

“Huu ndiyo wakati wa nyinyi kuja nyumbani kuchangamkia nafasi za mafanikio kabla hazijaisha, huko tunakokwenda, kama mambo hayatabadilika, itakuwa vigumu sana kwa Watanzania kufanikiwa, nafasi inazidi kuwa finyu kadri tunavyozidi kupanda juu,” alisema Shigongo huku akimtaka kila mmoja kuwa na mchango kwa maendeleo ya nchi yetu.

Alisema kufanya hivyo na huku serikali ikitimiza wajibu wake, Tanzania haitabaki ile ile miaka michache ijayo, na kwamba tufanye kazi kwa uzalendo huku tukiwafikiria watakaokuja baada yetu.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Baraza la Watanzania waishio nchini Marekani (DICOTA), wawekezaji wa makampuni makubwa nchini Marekani kama vile General Mills walikuwepo kukutana na Watanzania. Viongozi wengine kutoka Tanzania waliopata nafasi ya kuzungumza ni pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ambaye aliwahakikishia Diaspora kuwa serikali ya Tanzania iko tayari kuwasaidia pale watakaporejea nyumbani kuchangia maendeleo yetu.

Aidha, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Harry Kitilya naye aliongelea juu ya misamaha ya kodi inayotolewa kwa Watanzania walioko nje ya nchi pale wanaporejea nyumbani na alipongezwa kwa uamuzi wake wa kukifunga kitengo cha Long Room kilichodaiwa kuwa na usumbufu mkubwa na kuwa chanzo kikubwa cha rushwa na kushuka kwa mapato ya serikali.

Mwakilishi wa CRDB Bank katika mkutano huo, alifafanua kuhusu akaunti yao ya Tanzanite na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Emmanuel Ole Naiko aliongelea juu ya umuhimu wa kuwekeza nyumbani. Halikadhalika, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji, Dk. Hamis Kibola alihudhuria mkutano huo.

Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Ombeni Sefue na kamati nzima ya DICOTA, ikiongozwa na Dk. Lennard Tenende, ilipongezwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo kwa maandalizi mazuri ambapo Kampuni ya Global Publishers ilipewa tuzo kwa kazi nzuri inayoifanya katika jamii ikiwa ni pamoja na kuwa miongoni mwa wadhamini wa mkutano huo.

0 comments: