Social Icons

Tuesday, December 13, 2011

"CUF KIMENUKA MABIBO"Hamad Rashid Mohamed.

Maalim Seif Hamad.


MSUGUANO kati ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Hamad, sasa umefika pabaya baada ya wafuasi wao kushambuliana kwa mapanga, mawe na fimbo na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa.

Tukio hilo lilitokea jana katika tawi la CUF la Chechnya, lililoko Mabibo, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, baada ya makundi ya wafuasi hao kupambana.

Tukio hilo lilisababisha kuvuruga moja ya vikao vilivyoanza kuendeshwa juzi na Hamad Rashid.

Baadhi ya wafuasi wa CUF wakishirikiana na wale kutoka makao makuu wakiongozwa na kikosi cha ulinzi cha chama, maarufu kama ‘Blue Guard’, wanadai kuwa vikao hivyo vina nia ya kukivuruga chama hicho.

Mapigano hayo yalizua tafrani na hofu kubwa miongoni mwa wapita njia, wafanyabiashara na wakazi wanaozunguka tawi hilo.

Hata hivyo, wafuasi ambao waliandaa kikao hicho, walilazimika kutumia mbinu mbalimbali za kupigana na kufanikiwa kukikimbiza kikosi hicho, baada ya kutaka kutumia nguvu kuvunja kikao hicho.

Kikosi hicho cha Blue Guard, kilifika katika eneo la kikao hicho na kuamuru mkutano huo uvunjwe kwa madai kwamba haukuwa unaendeshwa kihalali kwa vile haukutambuliwa na makao makuu ya chama.

Baada ya kikosi hicho kutaka kuvunja kikao hicho, wanachama wa tawi la Chechnya waligoma kukivunja.

Walidai kwamba ni haki yao kikatiba kufanya mkutano kwa sababu lengo lao si kubomoa bali ni kutaka kujenga chama.

Hata hivyo, pande mbili hizo zilishindwa kufikia mwafaka, ndipo zilipoibuka vurugu.

Wafuasi hao walianza kupigana huku upande mmoja ukitaka kuvunja mkutano na mwingine ukizuia mkutano huo kuvunjwa.

Katika tafrani hiyo, Blue Guard mmoja alitumia panga na kumjeruhi kijana mmoja kutoka katika kundi la Chechnya katika kiganja cha mkono.

Kijana huyo alikimbizwa katika kituo cha afya kwa matibabu.

Mbali na panga, silaha nyingine zilizotumika katika vurugu hizo, ni mawe, fimbo na ngumi.

Hata hivyo, Blue Guard walishindwa kuvumilia na kuamua kuingia katika gari lao na kuondoka.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa la CUF, Doyo Hassan, alisema mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano inayofanywa na tawi hilo ambayo inalenga kuhuisha na kuimarisha chama.

“Lengo la mkutano huu ni kujadili na kuangalia namna ya kuhuisha chama kirudishe mwelekeo na si vinginevyo, lakini cha kushangaza watu wanakuja kutuamrisha eti tuvunje mkutano,” alisema Doyo.

Akizungumza katika mkutano huo baada ya hali kutulia, Hamad Rashid, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alilaani vurugu zilizotokea na kuziita kuwa uhuni.

“Nimeghadhibika sana. Nilipoambiwa kwamba kuna watu wamekuja kufanya fujo hapa na kuwakata baadhi yenu mapanga, hiki kitendo kinasikitisha na kinapaswa kulaaniwa,” alisema Hamad.

Aliongeza: “Inasikitisha sana kuona chama hakina fedha, na hiyo fedha kidogo iliyopo wanayotoa wanachama ndiyo inatumika katika kujazia mafuta kwenye gari na kwenda kuwakata mapanga watu wanaochanga.”

Hata hivyo, Hamad aliwataka wanachama wa chama hicho, kutokukata tamaa bali waendelee kudai mabadiliko ya katiba ya chama chao.

“Ninaomba msikate tamaa, bali muendelee kudai mabadiliko ya katiba ambayo yatasaidia kuimarisha chama,” alisema Hamad.

Aliongeza: “Hatutakubali kuona Katibu Mkuu Maalim Seif akiendelea kukalia nafasi hiyo, tunataka nafasi hiyo ishikiliwe na mtu mwingine ambaye atakiendeleza chama, hawezi kufanya kazi zote kwa wakati mmoja, na mtu hawezi kupanda farasi na punda kwa wakati mmoja.”

Alisema hatishiki na vitisho wala jambo lolote bali ataendelea kupambana mpaka kuhakikisha chama hicho kinashika dola mwaka 2015.

Alipoulizwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema alikuwa hajapata taarifa hizo rasmi lakini anafanya juhudi za kuzitafuta.

Chimbuko la hali hii linadaiwa ni vuguvugu za ndani kwa ndani za uchaguzi wa viongozi wa chama hicho akidaiwa kutamani kiti cha Katibu Mkuu kitakaachoachwa wazi na Maalim Seif kama ataamua kustaafu.

Hamad Rashid analalamika kuwa Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ana mwanachama anayemuandaa kwa ajili ya kiti hicho.

Harakati hizo pia zimesababisha viongozi hao wawili kulaumiana juu ya utendaji na ujenzi wa chama Tanzania Bara, huku Hamad Rashid akimlaumu Maalim Seif kwa kutokufanya kazi kubwa ya kisiasa Tanzania Bara.

Miongoni mwa lawama anazobebeshwa Maalim Seif ni kufanya vibaya kwa CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ambao chama hicho kilishika nafasi ya tatu huku kikipata idadi ndogo ya wabunge Bara kiasi cha kupoteza nafasi ya kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni nafasi ambayo wameishikilia tangu mwaka 1995.

CHANZO: NIPASHE


0 comments: