National Arts Council BASATA
26/08/2011
PRESS RELEASE
PONGEZI KWA WASANII WA TANZANIA WALIOSHINDA TUZO ZA MUZIKI ZA AFRIKA MASHARIKI (EMAS)
Baraza la Sanaa la Taifa linatoa pongezi za dhati kwa wasanii wa Tanzania walioshinda Tuzo za muziki za Afrika Mashariki (EMAS) zilizofanyika Jijini Nairobi,Kenya Agosti 20,2011 na kushirikisha wasanii mbalimbali wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Ushindi huo wa wasanii wa Tanzania ambao ni Bendi ya Muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Ambwene Yesaya (AY), Khamis Mwinjuma (Mwana FA) na Christian Shusho ni heshima kubwa kwa taifa letu na ni ishara kwamba,kazi zao zinakubalika na zina ubora unaoziwezesha kushindana na kazi za wasanii wa mataifa mengine.
Aidha,Baraza linawapongeza kwa dhati wasanii Judith Wambura (Lady Jay Dee), Vumilia Abraham, Upendo Nkone, Mwanza Gospel Choir, Christian Bella, Mabeste, Beatrice Mathew na Tina Mdulule kwa kuwa miongoni mwa wasanii walioingia kwenye kuwania tuzo hizo.
Ingawa hawakushinda,kuwemo kwao kwenye tuzo hizo ni ishara kwamba,kazi zao ni bora na zinakubalika.Cha msingi ni kutokata tamaa na kuendelea kufanya kazi zenye ubora na zinazokubalika.
Ni wito wa Baraza kwamba,wasanii wetu wataendela kuongeza ubunifu na ubora katika kazi ili kuhakikisha wanaendelea kuwa bora katika ukanda huu.
Baraza linawakumbusha wasanii wote kuwa,ubunifu, kujituma, kuzingatia maadili na kusimamia misingi ya sanaa ndiyo njia pekee itakayowapa heshima na mafanikio katika kazi zao.
Sanaa ni Kazi Kwa Pamoja Tuikuze na Kuithamini.
Ghonche Materego
KATIBU MTENDAJI, BASATA
0 comments:
Post a Comment