Spika wa Bunge, Anne Makinda.
MUNGU ndiye aliyenifanya niwe na uwezo wa kuandika haya nitakayoandika leo, hivyo sina budi kumshukuru na kumtukuza.
Baada ya kusema hayo nianze kwa kukumbusha tu kuwa Bunge la Bajeti ya mwaka 2011/2012 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeanza rasmi Jumanne iliyopita mjini Dodoma.
Ndugu zangu, huu ni mkutano wa kwanza wa bajeti kwa Bunge la 10 linaloongozwa na Spika Anne Makinda ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi za kulitoa taifa katika umasikini na kuimarisha umoja wa kitaifa ambao una dalili za kumomonyoka hasa baada ya kudaiwa kuwa kuna baadhi ya wananchi wanataka muungano ufe.
Watu wengi tunaelewa kuwa mkutano wa Bunge la Bajeti una kazi nzito kwa kuwa Wabunge tuliowachagua ndiyo wanaoamua kwa niaba yetu mustakabali wa taifa kwa kipindi cha mwaka mzima wa kifedha serikalini kwa kupitisha bajeti itakayoiwezesha dola kutekeleza mipango ya maendeleo katika sekta zote.
Hii ina maana kuwa, wabunge wana jukumu la kuchambua kwa kina bajeti ya serikali na kupitisha makadirio yanayolingana na hali halisi ya uchumi wa Tanzania, badala ya matarajio makubwa yasiyotekelezeka.
Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya wabunge wanapokuwa Bungeni hawawi makini kufuatilia na kujadili kwa kina hotuba hizo na mbaya zaidi huwa tunashuhudia wengine wakikwepa kuhudhuria vikao na wengine wakilala usingizi ndani ya Ukumbi wa Ubunge. Hakuna asiyejua kuwa hivi sasa Bunge letu linakabiliwa na tatizo la kiitikadi kwa kuingiza tofuati za kisiasa hata katika maamuzi muhimu ya kuliendeleza taifa letu, kitu ambacho ni kibaya.
Wapo baadhi ya wabunge kazi yao wakiwa ndani ya ukumbi bungeni ni kupinga au kuzomea hoja zinazotolewa na wenzao hata kama mambo yanayozungumzwa ni muhimu kwa masilahi ya taifa na wananchi.
Naamini hali hiyo inapotokea bunge linaweza kujikuta likipitisha maazimio yasiyo na tija kwa taifa kwani wabunge wengi huunga mkono hoja kwa lengo la kuimarisha kambi zao za kisiasa bila kujali athari zake.
Ndugu zangu, mifano ipo wazi, kwa mfano sheria inaweza kupitishwa bungeni ikifika mahakamani inaamriwa irejeshwe tena bungeni kujadiliwa.
Kutokana na hali hiyo, niwakumbushe waheshimiwa wabunge kutambua kuwa wapo bungeni kwa ajili ya kutetea masilahi ya wananchi na baadaye matakwa yao ya kisiasa ambayo kwa ujumla yanapimwa kutokana na kujitoa kwao kukabiliana na changamoto zinazokwamisha maendeleo ya wananchi na taifa letu.
Niwaombe waheshimiwa kuwa katika Bunge hili la Bajeti, wahudhurie vikao vyote pamoja na kufuatilia kwa kina bajeti ya Serikali iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo na zitakazosomwa na mawaziri mbalimbali.
Nasema hivyo nikiwa na maana kwamba wapitie kifungu kwa kifungu kugundua udhaifu uliomo na kufanya marekebisho sahihi kabla ya kuipitisha.
Sichoki kuwashauri kuwa, ule utamaduni wa wabunge kujifanya kupinga wakati wa kujadili na kuipitisha kwa asilimia mia moja kabla ya udhaifu uliobainishwa kurekebishwa, safari hii tunaomba usiwepo.
Wapiga kura tuna imani kuwa kama wabunge wataona udhaifu katika bajeti ya wizara fulani, asiwepo mbunge atakayesema naunga mkono kwa asilimia 100 kabla ya kurekebishwa kasoro iliyogundulika na kuthibitishwa.
Ndugu zangu, wapiga kura hatutegemei kuona kambi ya upinzani ikipinga kila kitu na kambi ya chama tawala kupitisha kila kitu kwa lengo la kuisaidia serikali hata kama kuna kasoro iliyogundulika.
Ni jukumu la Spika Makinda kutopendelea upande wowote katika suala hili la bajeti, haitafurahisha akilaumiwa katika suala hili.
Wengi tulishuhudia katika mikutano ya Bunge iliyopita spika alilaumiwa kwamba alikuwa na upande, wengine wakasema ni tofauti na mtangulizi wake, Samwel Sitta.
Ukweli ni kwamba, msimamo wa Spika ndiyo utakaoisaidia serikali kujipanga vizuri na kuleta bungeni hoja na bajeti inayotekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala kwa masilahi ya Watanzania wote.
Wabunge wanatakiwa kuichambua bajeti kwa lengo la kuwa na bajeti inayotekelezeka kwa kuzingatia mapato kutoka ndani ambayo yasimamiwe vizuri ili yapatikane na ili tusikwamishe malengo ya utekelezaji wa mipango iliyokusudiwa.
Wapiga kura wengi wanatarajia kuwa Bunge la sasa litakuwa jasiri kwa kupitisha makadario na matumizi yenye uhakia kwa asilimia100.
Wabunge wanaweza kutumia nafasi ya kuchangia bajeti hii kwa kuanza kushauri mikakati madhubuti itakayofanya serikali ijayo kuandaa mipango na bajeti inayotegemea pato la ndani kwa asilimia kubwa tofuati na sasa inapotegemea zaidi ya asilimia 40 kutoka kwa wafadhili ambao hakika tusitegemee kuwa watatufadhili milele.
Kitu muhimu ni kila mbunge alijione yupo pale kuwakilisha wananchi ambao wengine hawana vyama, hivyo basi wawapo bungeni itikadi za kisiasa ziwekwe pembeni.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
0 comments:
Post a Comment