Majonzi, huzuni na maombolezo makubwa yamegubika Jiji la Dar es Salaam eneo la Kibamba kufuatia vifo vya watu wanne wa familia moja vilivyotokea wiki iliyopita kwa ajali ya gari na kutajwa kuwa ni zaidi ya msiba.
Ajali hiyo ilihusisha basi lenye namba za usajili T612 BAM, mali ya Kampuni ya Moro Best liligonga gari dogo lenye namba T 666 BAP, Toyota Carina lililobeba familia ya baba, mke na watoto wawili ambao walifariki papo hapo.Watu hao walifariki katika eneo la Minarani Wilaya ya Kisarawe Juni 8, mwaka huu saa 9 alasiri.
Akizungumza na gazeti hili Kibamba nyumbani kwa marehemu Samson, mmoja wa wana ndugu Dk. Simon Mamuya alisema kwamba waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Samson Mamuya, Mkewe Rose Mamuya (44) ambaye alikuwa akifanya kazi Chuo Kikuu, Kitivo cha Sheria na watoto wawili Allen Mamuya (24) na Danny Bariki Mamuya (9).
Aidha, Dk. Mamuya aliendelea kusema kwamba siku hiyo ndiyo iliyopangwa na familia kumpeleka Danny shule ya kulala itwayo St. Doricas iliyopo Kisarawe, ndipo wakapata ajali ambapo walipoteza maisha.
“Taarifa tulizopata ni kwamba gari walilopanda marehemu hao lilikuwa likiendeshwa na Samson liliharibika vibaya likawa kama chapati kwani baada ya kugongana basi lililiparamia kwa juu na kuharibu sura ya gari ambalo walikuwemo wanafamilia hao.
“Kuondoa miili yao ndani ya gari hilo ilichukua saa tatu,” alisema Dk. Mamuya.
Aliongeza kuwa polisi walipofika waliichukua miili na walikuta kitambulisho cha Allen kikiwa na namba za simu ndipo ilipigwa kwa Joseph Mamuya na kuelezwa kwamba mtoto huyo amepata ajali na amezidiwa hivyo aende hospitali ya Kisarawe.
Aliendelea kueleza kwamba baada ya Joseph kupata taarifa hizo alimuita shemeji yake aitwaye Mnuo ili waongozane kwenda Kisarawe, walijishauri ni kitu gani cha kwenda nacho ambapo waliafikiana kuchukua chakula.
Hata hivyo, walipata hofu na kabla ya kuondoka walipiga simu polisi ili wapewe taarifa kamili ndipo waliambiwa kwamba ndugu zao wote wanne waliokuwa katika gari hilo wamefariki dunia.
Dk. Mamuya alieleza kwamba Joseph na Mnuo walikwenda hospitalini hapo na kuitambua miili ya wapendwa wao ndipo wakaanza kuwataarifu ndugu, jamaa na marafiki juu ya tukio hilo la kusikitisha.
Aliongeza kuwa, baadaye walichukua miili ya marehemu na kuipeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo taratibu za mazishi zilifanyika.
Dk. Mamuya alisema Samson na mkewe (Rose) walizikwa nyumbani kwao Ruguluni Kibamba siku ya Jumamosi iliyopita, Danny na Allen miili yao ilisafilishwa Jumapili kwa mazishi katika kijiji cha Marangu Arisi Wilaya ya Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Absalom Mwakyoma alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kwamba basi hilo lilikuwa likifanyiwa majaribio.
Gazeti hili linatoa pole kwa familia ya Mamuya kwa msiba huo mzito na kuwataka wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, AMINA.
Habari hii imeandaliwa na Makongoro Oging, Issa Mnally na Haruni Sanchawa.
2 comments:
Uandishi wa habari ni mgumu sana haswa inapofikia kuwapa watu taarifa zilizokamilika. Je, waliopata ajali nifamilia yote au kuna wengine walikuwa wamebaki nyumbani? Na kama kuna waliobaki ni watoto wa umri gani?
R.I.P
Post a Comment