Dereva wa basi la Abood lililopata ajali.
Mmoja wa wauguzi wa wodi ya wagonjwa mahututi akimhudumia mmoja wa majeruhi Gosbert Kajalaba aliyevunjika miguu yote miwili na mkono.
Na Thompson Mpanji, Mbeya
WAKATI bado Watanzania wakiendelea na majonzi na kuomboleza vifo vya watu 16 waliofariki dunia katika ajali ya basi la abiria la kampuni ya Sumry iliyotokea wiki iliyopita maeneo ya Igawa, mpakani mwa Iringa na Mbeya, watu wengine 30 wamejeruhiwa katika ajali ya basi la Abood lenye namba za usajili T 297 ATH lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya jana katika eneo la Mlima Nyoka, Itewe, katika barabara ya Mbeya-Iringa.
Akiongea na mtandao huu ofisini kwake mkuu wa kitengo cha upasuaji, Dkt. Chrispin Masandika kwa niaba ya mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya amesema majeruhi hao walipokelewa jana (Juni Mosi) majira ya usiku ambapo mgonjwa mmoja Gosbert Kajalaba (45), mkazi wa Dar es Salaam mtaalam wa masuala ya hoteli aliyekuwa akifika kutoa semina katika hoteli ya Rift Valley yupo mahututi baada ya kupata jeraha kichwani, kuvunjika miguu yote miwili na mkono wa kushoto.
Dkt. Masandika amesema baada ya kumfanyia upasuaji usiku anaendelea vizuri ambapo dereva wa gari hilo George David (45), mkazi wa Dar es Salaam amelazwa katika wodi namba moja akiendelea na matibabu huku majeruhi wengine wanane wakiwa wamelazwa na kuendelea na matibabu na wengine 20 kuruhusiwa kurudi majumbani baada ya kupata matibabu.
Mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika wodi namba moja aliyejitambulisha kwa jina la Lucas Benedikto amesema chanzo cha ajali ni dereva wa basi hilo kutaka kulipita lori la mizigo katika mlima huo ambapo aliligonga lori hilo na kupinduka.
0 comments:
Post a Comment