Social Icons

Wednesday, June 8, 2011

BAJETI YA TANZANIA 2011/2012 IDHIBITI MFUMUKO WA BEI


Askofu Beatus Kinyaiya, Mwenyekiti wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Tanzania, Caritas Tanzania, anasema, bajeti ya maendeleo ya Tanzania kwa Mwaka 2011-2012 inapaswa kujikita zaidi katika kudhibiti mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma, ili kuwawezesha watanzania wengi kupambana na makali ya maisha yanayoendelea kuwatumbukiza katika baa la umaskini.


Udhbiti wa nishati ya mafuta ni jambo la msingi kwani bei ya mafuta imekuwa daima ni chanzo cha kupanda kwa bidhaa na huduma nyingine zote zinazotolewa.

Bajeti hii iyaangalie pia maeneo nyeti kama vile, elimu, afya, kilimo na miundo mbinu. Askofu Kinayaiya anasema, elimu ni mkombozi wa watu wanyonge ndani ya jamii, Serikali na wadau wa maendeleo wakiwekeza katika elimu, mbele ya safari, inalipa! Nchi nyingi zinazoendelea zimeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na kuwekeza katika sekta ya elimu, sayansi na teknolojia.

Kilimo kimekuwa kikipewa msukumo wa pekee katika mikakati ya kukuza na kuinua uchumi wa Tanzania kwa kutambua kwamba, kilimo ni uti wa mgongo wa Tanzania. Lakini, hali ya maisha na kipato cha wakulima bado ni cha chini sana, changamoto ambayo Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu wanapaswa kuifanyia kazi, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Askofu Beatus Kinyaiya ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Mbulu anasema, Serikali na wadau mbali mbali wameonesha nia ya dhati katika maboresho ya sekta ya afya, tangu katika bajeti ya mwaka 2010-2011.

Ni vyema kuendeleza mikakati, juhudi na mafanikio yaliyokwishakufikiwa, daima wakipania kuboresha huduma kwa watanzania, kwani maisha ni haki msingi ya binadamu.

0 comments: