Ugomvi wa aina yake umezuka msibani mwishoni mwa wiki iliyopita, Ilala jijini Dar es Salaam ambapo mtoto wa kike aliyetajwa kwa jina moja la Lailati (pichani) aligombewa na wanaume wawili waliojitokeza, kila mmoja akidai ni wake.
Chanzo chetu cha habari kilisema kuwa, hali hiyo ilijitokeza mara baada ya mama wa mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la Nasra Auth Omary Ngaugia kufariki dunia Aprili 26, mwaka huu na kuacha mtoto huyo akiwa na mmoja wa wanaume hao.
Marehemu Nasra Auth Omary Ngaugia enzi za uhai wake.
Habari zinasema siku ya msiba alijitokeza kijana mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Twaha na kuanza kumdai mtoto huyo kwenye msiba uliokuwepo karibu na Ofisi za Benki ya Damu maeneo ya Msimbazi Center, hali iliyowashangaza watu wengi kwani kulikuwa na baba anayedai kuwa ndiye mzazi.
Gazeti hili lilifanikiwa kumpata baba anayedai kuwa yeye ndiye alizaa na marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Mohamed Msumbwa na kudai kuwa, mtoto huyo ni wake na anashangaa kuona kuna mtu au watu wanadai ni wao.
“Historia kamili ya mwanangu ninaifahamu lakini hao wanaosema ni wao ushahidi huo hawana, najua hospitali aliyojifungulia lakini hao vielelezo vyote hivyo hawana,” alidai Msumbwa.
Naye Twaha alipohojiwa alidai kuwa, inawezekana marehemu hakuwa mkweli kwani aliwahi kumwambia kuwa, Lailati ni mtoto wake na wakati anaishi naye baada ya kutomuona alimwambia kuwa amempeleka kwa shangazi yake.
Hassan Mohamed Msumbwa akiwa na mtoto huyo.
Hata hivyo, dada wa marehemu ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, alipohojiwa na gazeti hili alisema kuwa, anavyofahamu yeye mtoto huyo ni wa Msumbwa.
“Mdogo wangu alikuwa akiniambia hivyo na hajawahi kumtaja mtu mwingine na hata cheti cha kliniki alimuandikisha mwanaume huyo, ukimuangalia mtoto wanafanana,” alisema. Kwa hivi sasa mtoto huyo yupo kwa kaka wa Msumbwa.
0 comments:
Post a Comment