Social Icons

Tuesday, April 12, 2011

TGNP YATAKA KATIBA YA UMMA, SI YA WATU BINAFSI

Mwenyekiti wa TGNP, Usu Mallya.

Na Walusanga Ndaki
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeorodhesha mapungufu kadhaa yaliyomo katika Muswada wa Katiba Mpya ambayo yatawanyima fursa watu wengi wa matabaka mbalimbali kuchangia matakwa yao katika katiba hiyo.

Mtandao huo, pia umelaani vurugu zinazopangwa na baadhi ya wanasiasa kwa lengo la kuvuruga majadiliano ya mchakato huo kwa kutumia watu wanaosababisha fujo, ikiwa ni pamoja na watoto wadogo ambao huwazomea wachangiaji.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Usu Mallya, TGNP ilisisitiza kwamba ili katiba iwe na uhalali wa kisiasa na mamlaka ya kisheria, ni lazima mchakato wake ushirikishe wananchi wote -- wanawake, wanaume, vijana, watu wanaoishi na ulemavu na watu wote walioko pembezoni ili kuleta mabadiliko chanya na pia kuleta haki na usawa kwa wote.

“Tunajua kuwa kama wananchi watanyamazia au watashindwa kutoa maoni yao juu ya muswada huu, katiba hiyo itakuwa si ya wananchi wote. Pia, tumesikitishwa na makundi ya wananchi wanaokubali kutumiwa vibaya kuzomea kwenye mikutano ya kujadili muswada huu na kuleta vurugu.

“Tunalaani kitendo cha wanasiasa kuwatumia watoto wadogo wasio na uelewa wa kuchangia muswada huu kwa kuwajaza katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam wiki iliyopita na kusababisha wananchi wenye mapenzi mema na taifa letu kukosa nafasi ya kuchangia kutokana na kukaa nje ya ukumbi,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia ililaani kitendo cha jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama kutumia silaha dhidi ya wananchi waliotaka kutoa maoni yao katika mjadala wa katiba uliofanyika mjini Dodoma wiki iliyopita na kusababisha wananchi wengi kuogopa kujitokeza kutoa maoni.

Kuhusu mapungufu, TGNP ilitaka tume ya kuongoza mchakato iwe na uwakilishi wa asilimia sawa kwa wanawake na wanaume na uteuzi wa wajumbe usifanywe na rais peke yake, badala yake bunge au vyombo vingine vyenye mamlaka vipewe jukumu hilo ambapo uteuzi uzingatie wajumbe toka kila jimbo zikiwemo asasi za kiraia, asasi za kidini na makundi ya watu wanaoishi na ulemavu, VVU na Ukimwi.

“Jina la muswada wenyewe liwakilishe mchakato wa wananchi walio wengi wanavyopendekeza kwa maana ya kutengeneza Katiba mpya, na sio muswada wa sheria ya marejeo ya Katiba iliyopo (Constitutional Review Act, 2011). Kwa mujibu wa kifungu cha 3 neno Katiba limetafsiriwa kumaanisha marekebisho katika Katiba ya sasa,” ilisema taarifa hiyo.

Matakwa mengine ya TGNP ni kwamba jina la muswada wenyewe liwakilishe mchakato wa wananchi walio wengi na si kumaanisha marekebisho katika katiba ya sasa, na hadidu za rejea zisiandaliwe na rais badala yake bunge liunde kamati maalum kwa ajili ya kutoa maamuzi.

“Lugha ya muswada iwe ya Kiswahili, kwa kuwa muswada huu wa kuandaa Katiba mpya si muswada kama miswada mingine ya sheria za kawaida, na kwa kuwa suala la Katiba ni nyeti na linaliwahusu na kuwagusa Watanzania wote, ushiriki wa kila aina katika mchakato wote ni muhimu sana. Tumeshangazwa sana na hatua ya serikali ya kuamua kutumia lugha ya Kiingereza ambayo Watanzania walio wengi hawaielewi kabisa,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Pamoja na kutaka rais asiwe na madaraka ya kuunda Baraza la Katiba, TGNP imetaka jukumu la kusimamia kura za maoni liwe mkononi mwa chombo huru, na imelitaka jeshi la polisi na vyombo vya usalama kuacha kuwatisha wananchi wanaotaka kushiriki mjadala huu ambao ni wa maslahi kwa wote.

“Jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama visiingilie utaratibu kwa kuwatisha wananchi na mabomu ya machozi na silaha kwani hali hii inawatisha wananchi walio wengi kushiriki ipasavyo katika mijadala hii pia vitendo hivi ni kinyume na haki za binadamu,” ilimalizia taarifa hiyo ya TGNP.

0 comments: