TUNAWAPITISHA watu wetu kwenye njia yenye giza. Kwenye njia yenye matope. Kwanini?
Socrates, mwanafalsafa wa Uyunani ya kale alipata kuonekana akimulika kurunzi mchana wa jua kali. Inaandikwa, kuwa Socrates yule alizunguka sokoni na kurunzi (tochi) yenye kumulika. Watu walimwuliza, kulikoni? Socrates akawajibu; ”Kwenye nuru hii , kuna walio gizani.”
Kwa Socrates lilikuwa ni tendo la kifalsafa lenye kuelezea hali halisi. Hata katika dunia hii ya kisasa, bado tuna miongoni mwetu, walio gizani mchana wa jua kali. Angalia ya kwa ’ Babu’ wa Loliondo. Ndio, kuna wanaohitaji kumulikiwa mwanga.
Na kuna tofauti ya ujinga na upumbavu. Marehemu Mzee Jongo alipata kutamka; ” Kusoma sio kuufuta ujinga, bali ni kuupunguza”. Kila mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja. Kuwa na ujinga wa jambo si kosa, hata Profesa anaweza asijue namna ya kuchochea kuni za kuchomea hindi bichi likachomeka. Kijana wa darasa la saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda Profesa.
Lakini upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa na uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu. Na ndio maana binadamu kuitwa mpumbavu ni tusi. Kuitwa mjinga si tusi, kila mmoja ana ujinga wake. Kuwa na ujinga wa jambo fulani ni kutoelewa jambo hilo. Ni nani anayeelewa kila jambo?
Na mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna niliyemwuliza swali hilo. Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!” Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani amgetamka, kuwa angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.
Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndio njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri? Haya ya kwa ’ Babu’ wa Loliondo ni kielelezo cha Watanzania kuamua kuacha kufikiri. Kuna umma uliojifunika vilemba vya ujinga. Umma uko gizani, unahitaji mwanga.
Yumkini wakatokea Watanzania wenzetu, wakaoteshwa na Mungu juu ya dawa za tiba kwa mwanadamu. Na hapo wakaingiza suala la imani. Lakini, jambo hilo halituzuii wanadamu kuhoji na kudadisi. Ndio, kuuliza maswali. Na kwa Serikali, jambo hilo haliizuii kufuata taratibu zake za kawaida ikiwamo kufanyia utafiti jambo hilo na kutoa msimamo wa Kiserikali. Hata kama Watanzania watakuwa na uhuru wa kwenda kwenye tiba za imani, lakini msimamo wa Serikali uwepo. Na kwa wengi utabaki kuwa ndio mwongozo, maana, watakuwa wameufanyia utafiti.
Si tumemsikia yule Nabii mwingine wa Tarakea, naye n i kijana wa miaka 28. Ikasemwa, kuwa naye kaoteshwa na Mungu dawa ya kutibu wagonjwa. Mpaka Serikali ilimpomzuia ili ifanye uchunguzi, tayari alikuwa na wagonjwa mia moja. Ndio, Watanzania tu wagonjwa tunaogombewa. Na viongozi wetu pia ni wagonjwa. Si tumewaona wakipanga foleni ya kikombe kwa ’ Babu’ wa Loliondo.
Katika dunia hii Serikali hupendwa na watu, lakini, si vema na busara, kwa Serikali za dunia kutaka kujipendekeza kwa watu. Kuna mambo yenye kupendwa na watu, na watu wakawa na haraka ya kutaka kuyafanya. Lakini, kama Serikali itahitaji kufuata taratibu ili kinachopendwa na watu kifanyike, basi, Serikali haina namna nyingine, bali kufuata taratibu. Si tuliona yale ya DECI. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisimamia taratibu, akasimamisha wimbi lile la DECI. Kuna wengi walishutumu, lakini , hao hao, leo wanaishukuru Serikali. Maana, DECI nayo ilikuwa ni Abrakadabra.
Na si juzi hapa tumemsikia Paroko wa Kigango cha Mt. Yohane wa Msalaba Parokoia ya Mbezi Luis.Padri Vivian. Niweke wazi, Paroko yule amesema kile ambacho kuna wengi hawataki kukisikia. Ameusema ukweli wake. Ameifanya kwa dhati, kazi ya utumishi wa Mungu wake.
Paroko yule wa Mbezi Luis alitamka; "Sina chuki wala tatizo lolote na tiba ya Loliondo, lakini kama unataka kwenda lazima ujiulize maswali manne yafuatayo;
Kwanza, tiba inayotokana na miujiza ya Mungu lazima iwe endelevu isiwepo kwa kipindi kifupi tu.
Pili, watu wajiulize kama miujiza kutoka kwa Mungu huwa na masharti?
Tatu, wajiulize kama tiba hiyo inafanya kazi ndani ya Loliondo, kwanini isifanye kazi Dar es Salaam na kwingineko?
Nne, wajiulize kuhusu tiba hiyo ya magonjwa sugu ukiwemo UKIMWI ni je, Mungu aliwaumba wanadamu na kisha kuamua kuwaangamiza? Au wanadamu wanaangamia kutokana na vitendo vyao vya ujanja ujanja?
Mwisho Paroko yule akasema; "Ukiishajiuliza maswali hayo na kujiridhisha kwa majibu utakayopata, basi, unaweza kufanya maamuzi ya kwenda Loliondo.
Ndio, tujiulize; katika mataizo yetu haya, tumechoka kufikiri? Tumechoka kuuliza maswali? Hapana. Tusichoke kuutafuta ukweli, hata kama umegubikwa na ukungu. Hivi ni Watanzania wangapi wamesikia au kusoma maelezo ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru Dr. Toure?
Nahofia si wengi, maana, maelezo yake yaliyopaswa kuwa habari kubwa ya ukurasa wa mbele yalipewa nafasi ndogo sana kwenye moja ya magazeti ya kila siku. Tena yaliwekwa katika ukurasa wa pili ndani ya habari nyingine. Si tunafahamu, kuwa baadhi ya wanahabari nao wanachagiza ’ Abrakadabra’ za ’ Babu’ wa Loliondo. Zinauza magazeti, na msimu ndio huu!
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Hospitali ya Mount Meru alisema, kuwa tangu tiba ya ’ Babu’ ianze, hajapata hata mgonjwa mmoja wa UKIMWI aliyepata kikombe cha ’ Babu’ na kurudi hospitalini hapo kupimwa tena. Hivyo, mpaka hii leo hatuna ushuhuda wa kimaabara kwa maana ya hospitalini. Ushuhuda tunaousikia ni wa mitaani. Ndio maana tiba ya ’ Babu’ itabaki kuwa ’ Abrakadabra’ mpaka hapo itakapothibitishwa vinginevyo kimaabara hospitalini na na si kwenye vijiwe vya barabarani.
Halafu tunaambiwa, kuwa tiba ya ’ Babu’ inatibu kansa pia. Hivi Kliniki ya Kansa ya pale Ocean Road mpaka hii leo imeshindwa kuwapeleka kwa ’ Babu’ wagonjwa watano tu walio kwenye matibabu ya kansa. Waende huko wakapate kikombe halafu wachukuliwe vipimo tena tuone nguvu ya tiba ya ’ Babu’ katika kuwasaidia wagonjwa wa kansa.
Ndugu zangu, Mfalme Suleiman alimwambia Mola wake; ” Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima”. Ndio, Mfalme Suleiman alipoambiwa na Mola kitu cha kuchagua, basi, aliichakua hekima ili aweze kuwaongoza watu wake.
Angalia leo, walio wagonjwa na kwenye hali ngumu za kiuchumi wanazidi kuwa wagonjwa na hali zao za kiuchumi zinazidi kuwa duni. Ndio, kuna wanaofunga safari zenye gharama kubwa kwenda Loliondo. Wanakwangua akiba zao. Kuna hata wanaokopa fedha za kwendea Loliondo.
Ndio, wanakwenda kupata tiba isiyo na hakika katika wakati huu tunaozungumza. Kuna wagonjwa walioacha kutumia dawa zao. Wamerudi na kuanza upya. Kuna waliopoteza maisha. Inasikitisha sana. Ni nani wa kuwasaidia kuwamulikia mwanga?
Naam. Kwenye nuru hii kuna walio gizani. Tuwasaidie.
Na Maggid Mjengwa.
0 comments:
Post a Comment