TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU BABU HUKO SAMUNGE LOLIONDO.
TAARIFA YA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII KUPITIA TAASISI ZAKE ZA UTAFITI KUHUSU DAWA YA MCHUNGAJI MSTAAFU AMBILIKILE MASAPILA WA SAMUNGE- LOLIONDO, AMBAZO NI: MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA), TAASISI YA UTAFITI WA DAWA ASILI YA CHUO KIKUU CHA AFYA YA SAYANSI SHIRIKISHI MUHIMBILI, (MUHAS) MKEMI MKUU WA SERIKALI (CGC), TAASISI YA TAIFA YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMU (NIMR)
Taarifa ziliifikia serikali kuwa, Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila, anatibu magonjwa sugu kwa kutumia dawa aliyooteshwa na Mwenyezi Mungu. Inasemekana kuwa, mchungaji alianza tiba hii tangu mwezi Agosti 2010, lakini watu wengi walianza kumiminika kwenda huko Samunge, kuanzia mwishoni mwa mwezi wa pili, mwaka huu wa 2011.
Kufuatia taarifa hii, serikali iliielekeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa, ufanyike haraka uchunguzi kuhusu dawa hii na itoe ushauri Serikalini ipasavyo. Baada ya kupokea maagizo hayo, wizara iliteua wataalamu kutoka taasisi zake tukiwemo sisi, TFDA, NIMR, Muhimbili kwa maana ya MUHAS, Mkemia Mkuu na tulijumuisha wataalamu wa hapa wizarani, ili kuifanya kazi hiyo muhimu, akiwemo Msajili wa Tiba Asili na Mbadala.
Hapo Machi 7 mwaka huu, sisi TFDA na wenzetu wanasayansi tulifanya safari kwenda Samunge kuonana na kufanya mazungumzo na Mchungaji mstaafu AmbilikileMasapila. Sisi TFDA na wataalam wenzangu wote, tunamshukuru sana mchungaji mstaafu, kwa ushirikiano na msaada mkubwa aliotupa sisi watafiti wote. kwa kuwa, tulifanya mazungumzo kwa masaa kadhaa kuhusu dawa hiyo jinsi alivyoanza, pia, alituonyesha mti unaotumika na alitupa sehemu mbali mbali za mti huo, kwa uchunguzi zaidi. Kadhalika, alituonyesha jinsi anavyotayarisha dawa hiyo na kutupatia sampuli yake iliyokwishategenezwa, tayari kwa matumizi. Sisi TFDA na wataalamu wenzetu tuliondoka nayo, kwa ajili ya uchunguzi zaidi, kwenye maabara zetu.
Baada ya kurejea kituoni Dar es Salaam, kazi ya utafiti wa dawa hiyo ilianza:
Jambo la kwanza kama watafiti, ilikuwa ni kuangalia na kuhakikisha usalama wa dawa ya Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila kwa watu. Uchunguzi uliofanyika, umetoa matokeo ambayo tumeridhika kuwa, dawa kwa kipimo anachotumia Mchungaji mstaafu AmbilikileMasapila, haina madhara yoyote yanayotambulika kwa sasa, kwa matumizi ya binaadamu.
Kazi inayofuata kwetu sisi watafiti baada ya matokeo haya, ni kuchunguza na kubaini, kama kweli dawa hii inatibu magonjwa hayo matano (5), kama anavyoeielezea yeye Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila. Uchunguzi huu utakapo kamilika, matokeo yake yatatolewa mara moja kwa wananchi wote!.
Hata hivyo, ninaomba kuwatahadharisha kuwa, hatua hii ya uchunguzi, si ya muda mfupi. Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kisayansi duniani, tafiti za namna hii zina mchakato unaohitaji muda wa kutosha kukamilisha hatua zake mbali mbali, na pia, kufikia viwango na vigezo vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa. Tunafanya hivyo kwa kuzingatia kuwa, dawa hii ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu, na inafuatiliwa na wananchi wetu na mataifa mbalimbali.
Sambamba na utafiti katika hatua hii, pia tunafanya uchambuzi wa kisayansi, katika maabara zetu, kwa sampuli tuliyoichukua kwa Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila, kwa kuangalia mambo mengine mawili muhimu kama ifuatavyo:
1. Kwa hatua tuliyofikia na taarifa tulizo nazo za dawa hii mpaka sasa, tumeandaa na tunakamilisha taratibu, ili tuweze kufuatilia maendeleo ya kiafya ya wagonjwa 200, ambao wamekubali kwa ridhaa yao wenyewe, kushiriki katika utafiti huu, ili kuona maendeleo yao kiafya, baada ya kunywa dawa ya Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila, kwa maradhi walionayo. Hatua hii, inafuata vigezo vyote vya Kitaifa na Kimataifa.
2. Pia tumeweka utaratibu madhubuti, wa kufuatilia matumizi ya mti huu, kama “mmea tiba”, katika sehemu nyingine za nchi yetu, kwani tuna taarifa kuwa, makabila mbali mbali yamekuwa yakitumia mti huu kama tiba. Makabila hayo ni pamoja na; Wagogo, Wamasai, Wabarbaig na Wasonjo kule Samunge.
Kwa niaba ya watafiti na wataalam wenzangu, ninaomba nimalize kwa kusema kwa muhtasari kuwa;:
1. Sisi sote tumeridhishwa kuwa, dawa anayotoa Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila, haina madhara yeyote yanayotambulika kwa sasa kwa matumizi ya binadamu. jambo hili mwazoni lilitia wasiwasi Serikali, Wataalam mbalimbali na wananchi kwa ujumla.
2. Kazi hiyo ya utafiti inaendelea ili kubaini magonjwa inayotibu,
3. Katika hatua hii, ninapenda kuwashukuru wataalamu wenzangu wote wa kikosi kazi cha wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya mkuu wa wilaya, Ngorongoro na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha na wananchi wote kwa kufanikisha zoezi hili mpaka sasa.
4. Pia sisi tunamshukuru sana Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila, kwa ushirikiano alioutoa, kwa timu ya watafiti waliofika kumuona, kuanzia siku ya kwanza mpaka leo hii..
Mwisho ninachukua fursa hii, kuwaomba wananchi wawe na subira katika kipindi hiki ili watupe nafasi tuweze kufanya kazi hii ya utafiti na uchambuzi zaidi, kwa utulivu na umakini wa juu kwani duniani kote, tafiti za aina hii, hazina njia ya mkato, nasi tunaahidi kwamba, tutatoa taarifa ya kina mara utafiti utakapo kamilika.
Asanteni na Ninawashukuru kwa kunisikiliza!
0 comments:
Post a Comment