Social Icons

Tuesday, March 1, 2011

SERIKALI ICHUKUE HATUA ILI TUEPUKANE NA MAJANGA

Ndugu zangu, tuanze makala haya kwa kumshukuru Mungu ambaye ametuwezesha kuwa katika dunia hii leo tukiwa na afya njema.

Leo nitazungumzia majanga mbalimbali ambayo yanatokea nchini mwetu yanayohusisha magari, vyombo vya baharini, angani na hata nchi kavu na kuishauri serikali nini cha kufanya ili kuepukana nayo.

Nianze na hili la juzi la milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania zilizoko Mbagala na Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Nitajadili pia majanga mengine mbalimbali ambayo yametokea katika sehemu nyingi hapa nchini ambayo yamedhihirisha pasipo shaka kuwa serikali yetu haijawa na mikakati thabiti ya kuepusha majanga.

Nionavyo mimi ni kwamba serikali imekuwa inasubiri majanga yatokee ndipo ikurupuke na kujaribu kuyazima bila mafanikio, tena kwa gharama kubwa mno ya fedha za walipa kodi.

Ndugu zangu, hatuwezi kuorodhesha majanga yote yaliyotokea katika nchi yetu kama vile ya ajali za barabarani, moto, ajali za majini, reli, anga na nyinginezo.

Sitayaorodhesha majanga hayo kwa sababu yalikuwa mengi na wananchi wote walikuwa mashahidi wa ama kuyaona au kusikia kupitia vyombo vya habari.

Ndugu zangu, majanga hayo huacha majonzi makubwa kwa taifa na mfano hai ni hili tukio la milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto ambayo yameacha watoto yatima, wajane, walemavu wa viungo na familia zilizosambaratika.

Ndugu zangu, somo kubwa tulilojifunza kutokana na majanga haya ni kuwa, baadhi ya watendaji ndani ya serikali yetu hawawajibiki kwa kushindwa kusimamia vizuri sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika uendeshaji wa mambo mbalimbali katika sehemu zao za kazi.

Ni bahati mbaya kuwa badala ya kuendesha shughuli za kiserikali, kibiashara na kijamii kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka zinazotambuliwa kisheria na kikatiba, siasa ndiyo imekuwa dira ya kuongoza nchi.

Wanasiasa wamekuwa vinara wa kuhubiri yale wasiyoyatekeleza na kuwa chimbuko la kuporomoka kwa maadili katika serikali na sekta mbalimbali.

Ndugu zangu, tunaweza kusema kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa ni chanzo kikubwa cha majanga yanayotokea katika nchi yetu kwa kutanguliza siasa. Kwa mfano, angalia jinsi watendaji serikalini wanavyoangalia sheria za barabarani zikikiukwa mchana kweupe pasipo kuchukua hatua.

Angalia jinsi mabasi yanavyojaza mafuta kwenye vituo vya mafuta yakiwa na abiria licha ya kitendo hicho kukatazwa. Siku moja gari likilipuka (hatuombei itokee) utaona jinsi viongozi watakavyokuwa na maneno mengi matamu huku watu wakiwa wameshapoteza maisha au kujeruhiwa vibaya.

Ndugu zangu, angalieni jinsi watu wanavyovamia na kujenga katika hifadhi za barabara. Watendaji wa serikali wapo na wanaangalia tu bila kuchukua hatua yoyote. Angalia barabara jinsi zinavyoanza kuchimbika na kuweka mashimo makubwa. Mwanzo huanza shimo dogo lakini likiachwa huwa kubwa kama handaki na baadaye kusababisha ajali mbaya!

Tujiulize, katika manispaa au halmashauri, au Mamlaka ya barabara (Tanroads), hawana wakaguzi ambao kazi yao ni kubaini mashimo ya kuyaziba kabla ya madhara kutokea?

Mifano ya uzembe wa baadhi ya watendaji serikalini ni mingi na kwa sababu hiyo Tanzania limekuwa taifa la majanga kila mwaka.

Ndugu zangu, nitoe mfano tena, jijini Dar es Salaam pale Ubungo, tujitayarishe kushuhudia janga kubwa zaidi ya majanga ya mabomu ya Mbagala na Gongo la Mboto likitokea kwani maelfu ya watu wamevamia na wanafanya biashara eneo hilo hatari ambalo lipo karibu na mitambo mikubwa kabisa ya umeme kuliko yote nchini.

Ndugu zangu, hakuna kiongozi anayejali wale watu hawaoni hatari iliyo mbele yao kwa sababu ya kujitafutia riziki ambayo inahatarisha maisha yao na mali zao.

Wote tunajua kuwa pale maelfu ya watu wanaofanya biashara, juu yao kuna nyaya za umeme mkubwa zaidi ya 132 KV na kando kuna mitambo ya Kampuni ya Umeme ya Songas.

Ndugu zangu, hatuombei majanga lakini tujiulize kama matanki yale ya gesi yakilipuka au mitambo ile ya umeme ikilipuka na karibu yake kuna vituo vya mafuta na vitu hivyo ni vyanzo vya majanga, hali itakuwaje?

Hivi karibuni umezuka mtindo wa wananchi kufanya biashara kandokando ya barabara kama vile Mbagala Rangi tatu, Manzese, Tegeta, Tandika Sokoni, Buguruni, Banana, Soko la Ilala na Mbezi Mwisho.

Pia Mzunguko wa Mtaa wa Msimbazi, Mahakama ya Ndizi Mabibo, na kadhalika, magari yanapita wakati mwingine kwa mwendo kasi. Je, gari likikosa breki au kupata tatizo la kiufundi na kuparamia watu itakuwaje? Ni kwamba tutashuhudia au kusikia janga kubwa kama lile lililowahi kutokea Tukuyu au Tarime.

Si Dar es Salaam tu hata mikoani katika miji ya huko hali ni hiyo hiyo ya uvamizi wa wafanyabishara katika barabara kama vile hakuna halmashauri za miji au mamlaka za serikali Kuu, wote huko watendaji wanangoja janga litokee.

Kuna baadhi ya watendaji ambao hungoja amri ya Rais Jakaya Kikwete aseme ndipo huchukua hatua ya kutekeleza. Hata kama jambo hilo ni la kuzuia majanga, mkuu wa nchi atafanya kazi ngapi?

Ndugu zangu, ni wazi kuwa mamlaka husika zimetanguliza siasa badala ya kusimamia kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepusha majanga yanayowaangamiza Watanzania kila kukicha. Kila kiongozi aone aibu janga linapotokea sehemu yake kama lilikuwa linawezekana kulizuia.

Ndugu zangu, nishauri tu kuwa pengine Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, chini ya Mwenyekiti wake, Edward Lowassa iingilie kati haya mambo yanayosababisha majanga na kushughulikia kuzuia ili kunusuru taifa na huzuni na majonzi ambayo tungeweza kuyaepuka.

Ipo haja pia kwa kamati hiyo ya bunge kubuni mbinu za kuwafundisha wananchi jinsi ya kukabiliana na majanga pindi yanapotokea.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

0 comments: