Mmoja kati ya Washiriki wa Mashindano ya Harley-Davidson Kilimanjaro Expedition akianza safari ya kuelekea Ngorongoro, msafara ulioanzia katika Hotel ya New Arusha leo.
Washiriki wa Mashindano ya Harley-Davidson Kilimanjaro Expedition wakijidadiliana jambo kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ngorongoro Crater msafara ulioanzia katika Hotel ya New Arusha leo.
Na Tulizo Kilaga, Arusha
Jumla ya washiriki 70 waliowasili nchini mapema wiki hii kushiriki mbio za pikipiki zijulikanazo kama Harley-Davidson Kilimanjaro Expedition wameanza safari ya kuelekea Ngorongoro Crater.
Mbio hizo zilizoandaliwa na kampuni ya kutengeneza pikipiki za Harley Davidson ya nchini Marekani kwa ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuratibiwa na Kampuni ya Kibo Burea Travel linalengo la kutangaza vivutio mbalimbali vya kitalii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya New Arusha Hotel jijini Arusha leo, Mwandaaji wa Harley-Davidson Motorbikes Kilimanjaro Safari Expedition, Jean-Marc Chapel, alisema mbio hizo zilizoanza Februari 14 zitakuwa za kilomita 3,120, ambako kati ya hizo, 2,350 ni nchini Tanzania na 770 zitakuwa nchi jirani ya Kenya.
Chapel alisema mbio hizo zinashirikisha pikipiki 50 ambapo 43 kati yake zitaingizwa nchini kwa meli na 7 zitakuwa za hapa nchini.
“Siku saba zitakuwa nchini Tanzania na siku tatu kwa Kenya. Washiriki 70 wataingia mbuga ya Serengeti na Hifadhi ya Ngorongoro kuangalia wanyama na mapumziko kidogo kabla ya kuendelea na msafara. Mbio hizi si za kushindana sana ni za maonyesho ya kitalii,” alisema.
Hata hivyo, Chapel alisema tofauti na ilivyotarajiwa meli yenye mzigo wa pikipiki hizo umechelewa kuingia nchini na hivyo kufanya safari hiyo ianze na pikipiki saba zilizopo nchini.
Alisema msafara uliondoka jijini Dar es Salaam ukiwa na pikipiki 7 na magari ya matengenezo na kuongoza msafara kutoka vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na kuchelewa kuwasili kwa meli, lakini alisisitiza kuwa pikipiki hizo zitakapofika zitaletwa kwa gari Arusha tayari kuungana na pikipiki nyingine kwenye mashindano hayo.
Mbio hizo zitapitia Chalinze, Lushoto, Marangu, Arusha, Ngorongoro, Serengeti na kuvuka mpaka wa Namanga hadi Kenya na zitarejea kupitia mpaka wa Horohoro Tanga, Chalinze hadi Dar es Salaam kisha kuvuka maji Visiwani Zanzibar.
“Katika msafara wa mbio hizi waandishi kutoka nchi mbalimbali watachukua picha za video na kutengeneza filamu itakayorushwa na Liberty Tv ya Ufaransa mara mbili kwa mwezi kwa mwaka mzima,” alisema.
Mbio hizo zimedhaminiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Kibo Travel Bureau, Liberty Tv, Freeway, Atemi, Azam Marine, Bavaria, Hoteli za Sea Cliff, Arusha Hotel, Tsavo Inn, Ocean Paradise Resort, Tanga Beach Resorts, Lushoto Highland Park na Lawn’s.
0 comments:
Post a Comment