Social Icons

Tuesday, January 4, 2011

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA NCHINI AFANYA ZIARA INDIA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami (kushoto) akizungumza na waandishi wa Habari Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kusafiri kuelekea nchini India kwa ziara ya siku saba. Pembeni yake ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Lazaro Nyalandu.


TANZANIA inaweka mikakati ya kupata wawekezaji katika uzalishaji wa chuma na kilimo kutoka nchini India.
Akizungumza jijini Dar es salaam kabla ya kusafiri kwa ziara ya siku saba nchini India, Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami alisema kuwa safari yake na viongozi wengine nchini India itakuwa na manufaa makubwa kwa taifa.
“Tunakwenda kwa mwaliko wa Chamber of Commerce ya jimbo la Marakshi kwa ajili ya maonyesho ya biashara, lakini wao ni wawekezaji wakubwa katika chuma, kwa miradi yetu kama ya Mchuchuma na Liganga tunaweza kufanikiwa”.
Dk. Chami alisema mbali na uwekezaji katika uchimbaji wa chuma pia katika kilimo Tanzania imekuwa ikifanya bishara kubwa na India, lakini kwa sasa wanatazamia kupata wawekezaji wanaoweza kuboresha mazao yetu yakaongezewa thamani hapa nchini.



Waziri wa Viwanda na Biashara Dk.Cyril Chami akifurahia jambo na waandishi wa habari muda fupi kabla ya kuelekea nchini India kwa ziara ya siku saba.

“India ndio wateja wakubwa wa korosho zetu lakini kwa sasa sidhani kama tuna haja ya kuwauzia zikiwa bado ghafi, ni lazima tuongeze thamani na tuuze zikiwa zimetengenezwa ili kupata faida zaidi” alisema.
Ushirikiano wa kibiashara kati ya India na Tanzania umekuwa ukiongezeka kwa kasi na ni nchi pekee ambayo biashara baina yake na Tanzania inapanda mwaka hadi mwaka.
Dk. Chami alisema kuwa sasa hivi ni wakati muafaka wa kuweza kupata wawekezaji ili kufaidi keki hiyo ambapo Afrika ikiwa na watu zaidi ya asilimia 15 lakini ni asilimia moja tu ya uwekezaji duniani huja Afrika.
Pia alifafanua kuwa katika asilimia moja hizo ni nchi chache zinazonufaika zaidi zikiwemo Nigeria, Misri na Afrika Kusini na iliyobaki ndio hubakia kwa nchi kama za Tanzania na nyinginezo.
Alisema kikubwa kwa yeye na ujumbe wake ni kupata wawekezaji wakubwa ambao wataleta fedha nyingi na teknolojia nchini ili kuweze kukuza biashara na viwanda vya ndani.

0 comments: