MOTO unazidi kuwaka Cairo, unasambaa pia. Tumeona picha za askari wale vijana wakitabasamu na kupeana mikono na wananchi. Ni ukweli, wengi wa wanajeshi hao wamekuwa recruited ( kuingizwa jeshini) wakitokea kwenye familia za kimasikini.
Kwa wanajeshi hawa, wana uelewa mkubwa wa wanachokipigania watu wa Misri. Ni suala la wakati tu kabla wanajeshi kuchukua uamuzi wa jumla wa kusimama upande wa umma. Na hilo likitokea, basi, mwisho wa zama za Hosni Mubarak utakuwa umeharakishwa, kwa nguvu ya umma ukisaidiwa na jeshi.
Maana, hata Hosni Mubarak akifanikiwa kuning’inia madarakani, bado, siku zake zitakuwa zikihesabika. Hosni Mubarak hana support ya umma, hivyo basi, hana uhalali wa kuendelea kuongoza dola kubwa na kongwe ya Egypt.
Watawala Afrika wana cha kujifunza?
Katika Afrika, mtawala atakayepuuzia moto unaowaka katika Dunia ya Waarabu ama ni mgonjwa au ni mjinga tu . Ni ukweli, kuwa Dunia ya Waarabu i-karibu nasi sana. Ni mwendo wa saa tano tu kwa ndege kutoka Dar es Salaam, Nairobi au Kampala kabla ya kutua Egypt, Tunisia, Yemen au Algeria. Ndio, ni umbali mfupi sana kabla ya aliye kwenye ndege kuanza kuuona moshi wa moto unaotokana na moto uliowashwa na umma unaotaka mabadiliko.
Ni dhahiri, kuwa yanayotokea kwenye Dunia ya Waarabu yana athari kubwa kwa ‘ Dunia Ya Waafrika’. Kihistoria na Kiutamaduni, Waafrika tuna mengi yanayotufanya tuwe karibu na Waarabu. Yaliyokuwa yakitokea Ulaya Mashariki miaka ile ya 80, ingawa yalisaidia kuleta mabadiliko pia barani Afrika, lakini, bado, yalitokea mbali na Afrika.
Lakini, harakati za vijana wa Kiarabu kuleta mabadiliko na hata kufanikiwa katika harakati zao, yana kila uwezekano wa kuwatia hamasa vijana wa Kiafrika katika nchi zao. Ikumbukwe, mengi wanayopigania vijana wa Kiarabu yanafanana na ya wenzao wa Afrika. Inahusu ukandamizaji, mgawanyo wa rasilimali wa haki na kukua kwa demokrasia ili kuchangie ustawi wa mataifa yao. Kupelekee kupata ajira na kuongeza vipato vyao. Kwa vijana hawa, kukua kwa uchumi wa nchi zao hakuna maana kama hali za watu wa kawaida zinakuwa ngumu kila kukicha na huku pengo la walio na wasio nacho likikua kwa kasi ya kutisha.
Kwa viongozi Afrika busara ni mapema kupunguza nywele zao kabla ya kulazimishwa kutia maji na kunyolewa vipara! Inahusu mabadiliko makubwa ya Katiba za nchi zetu ambazo bado zina ukakasi wa enzi za ‘ Chama Kushika Hatamu Zote’. Dunia Imebadilika. Angalia picha za matukio
0 comments:
Post a Comment