MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Kisutu imepokea pingu, miwani na hati ya upekuzi katika kesi ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) Jerry Muro kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.Vielelezo hivyo viliwasilishwa jana mahakamani hapo na Ofisa wa Polisi dwani Nyanda ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Gabriel Mirumbe.Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa Januari 29, mwaka 2010 akiwa ofisini kwake alipokea maagizo kutoka kwa mkuu wake wa kazi Kamishina wa Upelelezi Charles Mkumbo akimtaka kufanya upekuzi katika gari yenye namba za usajili T 545 BEH mali ya Jerry Muro.Alidai alishuka kwenda kulifuata gari hilo lililokuwa limepaki kwenye maegesho ya magari ya kituo kikuu cha polisi kati akiwa na mlalamikaji Michael Wage pamoja na mashahidi wengine ili kushuhudia zoezi la upekuzi huo.“Wage aliyekuwa analalamika kutishiwa kuuawa na Muro alikuwepo makusudi ili kuitambua miwani yake aliyodai kuisahau katika gari ya Muro siku aliyokamatwa na pingu aliyodai kutishiwa kufungwa nayo.“Baada ya upekuzi huo vitu vyote vilirekodiwa na kusainiwa na mimi na Muro mwenyewe kama uthibitisho kwamba kweli vitu hivyo vilikutwa garini kwake,” alidai shahidi huyo.Katika kesi hiyo Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mgasa wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 10, kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Michael Wage, Januari 29 mwaka jana.Mwendesha mashitaka wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus alidai kwa jana upande wa mashitaka ulikuwa na shahidi mmoja ambapo wengine watatu waliobaki watatoa ushahidi wao pindi kesi hiyo itakapopangiwa tarehe nyingine. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7 na 8, mwaka huu itakaposikilizwa tena.
1 comments:
hivi kweli Muro atakuwa alitaka kupokea rushwa? siamini lakini yaweza kuwa kweli lakini tunajua viongozi wa hapa wanavyoweza kuyapoteza majina ya watu maarufu na kuwaharibia kabisa maisha yao hasa unapoingia kwenye anga zao ngoja tuone itakavyokuwa
Post a Comment