Viongozi wa CHADEMA wakiwa kwenye maandamano huko Arusha jana.
*Mbowe na wabunge watano wa Chadema watiwa mbaroni
*Yumo Slaa, Mrema wa Arusha Mjini, Ndesamburo na Owenya
*Maandamano yavunjwa kwa mabomu na risasi
Jiji la Arusha limeendelea kuwa kitovu cha matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa vyombo vya dola, baada ya polisi kuwakamata wabunge watano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuvunja maandamano na kukamata raia wengine kadhaa.
Tukio hilo lililotawala Jiji la Arusha kwa siku nzima jana, linaibuka ikiwa ni wiki chache tu, baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, mwishoni mwa mwaka jana kupigwa na polisi na kumsababishia kupoteza fahamu.
Tukio la jana linaibuka wakati joto la kisiasa katika Jiji la Arusha likiwa juu kutokana na rafu zinazodaiwa kuchezwa kumpata Meya wa Jiji hilo maarufu kwa utalii nchini.
Katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita, Chadema ililalamikia hatua ya CCM kumtumia Mbunge wa Viti Maalum ambaye ni Katibu wa Chama hicho, Mkoa wa Tanga kupiga kura wakati hakuwa na sifa na kusababisha Diwani wa CCM, Gaudence Lyimo, kutangazwa kuwa Meya na nafasi ya Makamu Meya kuchukuliwa na Michael Kivuyo (TLP).
Waliokamatwa ni Kiongozi wa upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe; Mbunge wa Arusha Mjini, Lema, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Owenya na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibroad Slaa. Aidha, mke wa Katibu Mkuu wa Chadema, Josephine Mushumbusi, alijeruhiwa na kutiwa mbaroni.
Jiji hilo lilikuwa tete baada ya kugeuka uwanja wa mapigano baina ya polisi na wananchi, kufuatia polisi kuzuia maandamano ya Chadema yaliopangwa kufanyika jana kwa lengo la kushinikiza kurudiwa kwa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya pamoja na uandikaji wa katiba mpya ya nchi.
Wananchi wengi na baadhi ya polisi walijeruhiwa vibaya, baada ya polisi kutumia risasi za moto na mabomu, yalioambatana na maji ya kuwasha, na kuwalazimisha wananchi nao kutumia mawe na kuvunja baadhi ya majengo.
Wakati vurugu hizo zikitokea, wananchi walilazimika kulishambulia kwa mawe jengo la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha na kulivunja vioo, huku polisi zaidi ya watatu wakidaiwa kujeruhiwa vibaya.
Hayo yalitokea baada ya Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Dk. Willibrod Slaa, kuhutubia maelfu ya watu, kwenye viwanja vya NMC na kueleza unyama wa polisi wa kuwajeruhi watu waliokuwa wakiandamana kwa amani wakiwa wamefunga vitambaa vyeupe mikononi.
Baada ya Dk. Slaa kuhutubia, aliwataka wananchi kwa kutumia nguvu ya umma kuandamana kwenda kituo kikuu cha Polisi kwenda kuwatoa wabunge waliokamatwa.
Kufuatia ghasia hizo baina ya waandamaji hao na askari polisi pamoja na mgambo ambao walitumika kuongeza nguvu, hali hiyo ilipelekea watu kadhaa kujeruhiwa na risasi za moto baadhi yao katika maeneo ya miguuni na mikononi.
Ghasia hizo zilianzia eneo la tenki la maji wakati waandamaji hao wakiongozwa na Mbowe, Lema pamoja na viongozi wengine wa Chadema wakiendelea na maandamano hayo ndipo walipokuta kizuizi cha askari polisi na kuamriwa kutawanyika.
Baada yakukaidi amri hiyo, ndipo risasi za moto, mabomu ya machozi na gari la pilipili lilipoanza kuwatawanya waandamanaji hao.
Mbali na Mbowe, Lema na Mke wa Slaa kujeruhiwa vibaya wengine waliojeruhiwa ni waandishi wa habari Mosses Mashala, Omar Ashraf wa Channel Ten, Edward Selasini wa Arusha Times pamoja na mwandishi wa kujitegemea Mosses Kilinga.
Baada ya Mbowe, Lema na Mushumbusi kujeruhiwa, vibaya walikwenda kituo cha polisi cha Arusha kwa ajili ya kupatiwa fomu ya matibabu (PF3), lakini waliingizwa mahabusu.
Kufuatia viongozi hao kuingizwa mahabusu, Dk. Slaa alilazimika kufuatana na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, kuhutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya NMC.
Maandamano yakiwa yamezuiliwa na Polisi.
Hata hivyo, umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo ulishinikiza kwenda mpaka zilipo ofisi za jeshi la polisi kwa ajili ya kuwatoa wote waliokamatwa, hatua ambayo ilizua upya vurugu katika uwanja huo.
Hatua ya kuanza tena maandamano, iliyosababisha watu wengine zaidi kujeruhiwa na polisi waliokuwa wakifyatua mabomu na risasi.
Katika maandamano hayo, polisi walionekana kuzidiwa nguvu na kundi kubwa la waandamanaji, hatua iliyowalazimisha kuomba msaada kutoka kwa mgambo, ingawa pia bado walishindwa kuwadhibiti.
Kufuatia ghasia hizo, shughuli zote za kimaendeleo jijini Arusha zilisitishwa, maduka yalifungwa, biashara sokoni zilisimama na hata safari kutoka ndani na nje ya Jiji zilisimama.
Dk. Slaa akihutubia maelefu ya wananchi katika viwanja vya NMC, kabla ya kuanza kuandamana kuelekea polisi, alisema tayari ana ushahidi wa picha zinazoonyesha polisi walivyowajeruhi wananchi pamoja na viongozi wa kitaifa wa Chadema.
Alisema picha hizo atazipeleka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyoko mjini The Hague, Uholanzi ili wajionee jinsi Tanzania isivyo na amani na kutawaliwa na nguvu ya mabomu.
Pia Dk. Slaa alisema kuwa anaishangaa serikali badala ya kutumia fedha kuwaletea wananchi maendeleo, inazitumia kununulia magari ya maji ya kuwasha kuwadhuru wananchi.
DIWANI WA CCM AJIUNGA CHADEMA
Katika tukio lingine, Diwani wa CCM wa Kata ya Sombetini, Alphonce Mawazo, alijitokeza katika umati wa watu katika viwanja vya NMC na kutangaza kujiuzulu na kujiunga na Chadema kwa madai ya nguvu ya umma.
Naye Ndesamburo akizungumza katika mkutano huo, alisema Chadema hawaitaki katiba mpya ambayo Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuanzisha mchakato wa kuifanyia marekebishao, bali katiba itakayoundwa na wananchi wenyewe.
Alisema wananchi wanahitaji katiba mpya, lakini kauli ya Rais Kikwete kuwa ataunda tume ya kukusanya maoni, hawatakubaliana nayo kwani tume ambayo itaundwa itakuwa ni ya CCM na sio ya wananchi.
Ndesamburo alilaani vikali kitendo cha jeshi la polisi kuwapiga mabomu viongozi wa Chadema na wananchi.
Kwa upande wake Dk. Wilbord Slaa alisema wao walifuata sheria na walipewa kibali cha kuandamana, lakini wakashangaa kuwa maandamano yao yamefutwa na kujikuta wakipigwa mabomu na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andendenya, jana alikataa kuzungumzia vurugu hizo na waandishi wa habari walipokwenda kituo kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha, waliamriwa kuondoka haraka. Kwa siku nzima, kamanda huyo alikuwa amezima simu yake ya kiganjani.
POLISI MAKAO MAKUU YATOA TAMKO
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limesema litawafikisha mahakamani wakati wowote watu ambao walikamatwa wakishiriki katika maandamano hayo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana jioni, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Paul Chagonja, alisema watu hao watachukuliwa hatua hiyo kwa kuwa wamevunja sheria zilizowekwa na serikali.
Alifafanua kuwa viongozi wa Chadema, pamoja na wananchi wa kawaida watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kukiuka agizo la serikali la kuwakataza kuandamana.
“Watu wote wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi watafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu mashitaka ya kuvunja sheria na kukiuka agizo lililotolewa na serikali la kukataza maandamano,” alisema Chagonja.
Alisema Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua za kisheria watu ambao wanaonekana kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kuongeza kuwa uhuru na amani iliyopo nchini inapaswa kulindwa na kuheshimiwa.
Chagonja alisema kama kuna mambo ambayo wananchi hawaridhiki nayo, kuna njia mwafaka za kufanya ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo badala ya kufanya maandamano.
Hadi tunakwenda mitamboni, Polisi walikuwa wameizingira Hoteli ya Mount Meru walipofikia Dk. Slaa na Ndesamburo huku ikidaiwa kuwa walikuwa wakitaka kuwakamata.
Aidha, polisi walikuwa wameimarisha ulinzi kwa kuweka doria katika barabara kadhaa na kuyazuia mabasi ya mikoani kuingia stendi kuu ya mabasi.
Mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.Wilbroad Slaa, Josephine Mshumbusi akiwa ametapakaa damu baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kipigo na polisi wakati wakivunja maandamano ya viongozi na wanachama wa chama hicho.
Wakati hayo yakitokea, habari zaidi zilidai kuwa watu kadhaa walikufa katika vurugu hizo, ingawa Jeshi la Polisi halikuwa tayari kuthibitisha.
Jitihada za waandishi wetu kwenda katika hospitali ya Mkoa Mount Meru kufuatilia kama kuna majeruhi au maiti hazikufanikiwa kutokana na barabara kufungwa na polisi.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment