Social Icons

Friday, January 28, 2011

AIRTEL, KUKUTANISHA MAKAPUNI ZAIDI YA 40, KWENYE BONANZA LAO LA FEBRUARI 12 MWAKA HUU

Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino wa Kampuni ya Airtel Tanzania Beatrice Singano (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu tamasha la Wanahabari linalotarajiwa kufanywa na kampuni hiyo Februari 12 mwaka huu, Dar es Salaam.Kushoto ni Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo Mutta Muganyizi.
KAMPUNI ya Simu za mkononi ya Airtel Tanzania imeandaa Tamasha la waandishi wa vyombo mbalimbali vya Habari litakalofanyika Februari 12 mwaka huu katika viwanja vya Posta na Simu Kijitonyama, Dar es Salaam.
Hatua hii ya Airtel ni katika kutambua umuhimu wa tasnia ya habari nchini lakini pia ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kikazi baina ya pande hizi mbili zinazotegemeana katika utendaji wao wa kila siku.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Airtel Beatrice Singano alisema hatua hiyo ni ya kuimarisha ushirikiano baina ya pande mbili hizo na kwamba bonanza hilo litaziwezesha pande mbili husika kufahamiana zaidi.
Alisema wanahabari wamekuwa na mchango mkubwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kwamba Airtel wameona ni kitendo cha uungwana kwao kuonyesha thamani waliyonayo wanahabari kwa kukutana na kuburudika kwa pamoja kupitia michezo.
“Ni kawaida katika kila mwisho au mwanzoni wa mwaka kufanya tathimini ya jumla ya pale tulipo na wapi tunakwenda lakini pia huwa tunakitumia kipindi hiki kukaa na kufurahi kwa pamoja na watu wenye majukumu tofauti katika kulijenga taifa ambapo miongoni mwao ni nyinyi wanahabari,” alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na burudani tofauti pia kutakuwa na michezo mbalimbali ya kubahatisha ambapo wanahabari wataweza kujishindia zawadi tofauti kutoka Airtel.
Kampuni ya Capital- Plus International (CPI) ndio waratibu wa tamasha hili ambapo Mratibu Mawazo Waziri aliitaja michezo itakayohusika kuwa ni pamoja na mpira wa miguu ikihusisha timu ya watu saba kila upande, pete,kuvuta kamba na kuruka kwa magunia ambapo katika burudani kutakuwa na mashindano ya kuimba na kucheza dansi.
Alisema taratibu nyingine kuelekea katika tamasha hilo zitaendelea kutolewa kadri siku zitakavyosonga ambapo aliahidi wanahabari kupata burudani ya kipekee katika tamasha hili la aina yake katika medani ya Habari.
“Airtel chini ya uratibu wetu imedhamiria kuwapa wanahabari burudani ya kipekee kwani mchango wenu kwao pia umekuwa wa kipekee,” alisema Waziri.

0 comments: