Social Icons

Thursday, November 25, 2010

BARAZA LA MAWAZIRI MABADLIKO SURA 24 MPYA



RAIS Jakaya Kikwete jana alitangaza Baraza lake jipya la Mawaziri, huku akiwatema mawaziri tisa wa zamani, akiwemo Profesa Juma Kapuya na Mohameid Seif Khatib ambao wamekuwa mawaziri kwenye awamu tatu tofauti.
Baraza hilo jipya pia halina sura za wabunge ambao wamekuwa wakitajwa sana na vyombo vya habari kuwa wamepewa uwaziri, akiwemo Januari Makamba ambaye ni mtoto wa katibu mkuu wa CCM, mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango na waziri wa zamani wa fedha, Zakhia Meghji.
Pia kwenye orodha hiyo, hakuna jina la mweka hazina wa CCM, Amos Makalla ambaye pia alikuwa akitajwa sana kuwa ameteuliwa kuwa waziri mdogo wa fedha baada ya kushinda ubunge kwenye Jimbo la Mvomero.
Hata hivyo, majina mengine yaliyotajwa sana kama spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe na Lazaro Nyalandu yamo kwenye baraza jipya ambalo lina kazi kubwa ya kuhakikisha ilani ya CCM, ambayo inajumuisha ahadi nyingi kubwa alizozitoa Rais Kikwete kwenye kampeni, zinatimizwa ili nguvu ya chama hicho iliyotikiswa kwenye uchaguzi wa mwaka huu iweze kurejea.
Katika uteuzi huo mpya Kikwete amemuacha Profesa Kapuya ambaye katika serikali iliyopita alikuwa Waziri wa Kazi Ajira na Maendeleo ya Vijana, nafasi ambayo aliishikilia kuanzia mwaka 2008. Katika baraza la kwanza la JK, Kapuya alipewa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Nafasi ya Kapuya sasa imechukuliwa na Gaudensia Kabaka
na imebadilishwa na kuwa Wizara ya Kazi na Ajira, huku Dk Makongoro Mahanga akiendelea kuwa naibu wa wizara hiyo.
Kikwete pia amemtema Mohammad Seif Khatib, ambaye alikuwa waziri tangu enzi za serikali ya awamu ya pili. Katika baraza lililopita, Seif Khatib alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ambaye alishughulikia masuala ya Muungano, nafasi ambayo sasa imekwenda kwa Samia Suluhu.
Rais Kikwete pia amemtema Profesa Peter Msolla aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia pamoja na naibu wake Dk Maua Daftari.
Badala yake Rais Kikwete amemteua Profesa Makame Mnyaa Mbarawa aliyempa ubunge wa kuteuliwa wiki iliyopita, Charles Kitwanga akiteuliwa kuwa naibu waziri.
Kikwete pia amemuacha Prof David Mwakyusa, ambaye alikuwa daktari wa Mwalimu Julius Nyerere. Prof Mwakyusa aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kwenye serikali iliyopita na nafasi yake imekwenda kwa Dk Haji Hussein Mpanda huku naibu wake akiwa ni Dk Lucy Nkya ambaye serikali iliyopita alikuwa naibu wa Wizara wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto.
Aliyekuwa naibu waziri katika wizara hiyo Dk Aisha Kigoda alishindwa kupenya katika mchakato wa awali wa kuwania ubunge ndani ya CCM.
Margareth Sitta, aliyeshika Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na kuongoza kwa mafanikio kuundwa kwa Sheria ya Mtoto, hayumo kwenye baraza jipya na badala yake nafasi yake imekwenda kwa mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wa CCM, Sophia Simba, ambaye atasaidiwa na Umi Ali Mwalimu.
Rais pia hakumteua katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati kuingia kwenye baraza jipya baada ya kuiongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kipindi cha miaka mitatu. Naibu wake, Hezekiah Chibulunje pia ametemwa.
Nafasi ya waziri imekwenda kwa mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), Anna Tibaijuka, ambaye atatakiwa kupunguza migogoro mingi ya ardhi inayoendelea kukua. Mama Tibaijuka atasaidiwa na Goodluck Ole Madeye.
Mwanasiasa mkongwe Philip Marmo, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) hakuwa na nafasi ya kuteuliwa kurejea kwenye nafasi yake baada ya kupigwa kikumbo katika uchaguzi mkuu alipojaribu kutetea kiti cha ubunge Jimbo la Mbulu.
Wizara hiyo sasa itaongozwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, William Lukuvi ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) katika serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa.
Marmo amefuata njia inayofanana na ile ya Lawrence Marsha ambaye pia aliangushwa kwenye uchaguzi wa Jimbo la Ilemela na hivyo kukosa nafasi ya kurejea kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani.
Nafasi yake imechukuliwa na Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha ambaye alianguka kwenye kinyang'anyiro cha urais wa visiwa hivyo, lakini akateuliwa na rais kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.Naibu wake atakuwa Khamis Kagasheki.
Wengine walioanguka kwenye uchaguzi ni Shamsa Mwangunga na Dk Batilda Buriani, ambao kila mmoja alianguka kwenye hatua tofauti.
Wakati Mwangunga, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii alianguka katika kura za maoni ndani ya CCM, Dk Buriani aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), alipigwa mwereka katika uchaguzi mkuu Oktoba 31 alipoangushwa na mgombea wa Chadema kwenye Jimbo la Arusha Mjini.
Kuanguka kwa Mwangunga kumempandisha aliyekuwa naibu wake, Ezekiel Maige ambaye sasa anakuwa waziri kamili wakati nafasi ya unaibu imeondolewa.
Nafasi iliyoshikiliwa na Dk Buriani katika serikali iliyopita, safari hii itashikiliwa na Dk Terezya Luoga Hovisa aliyeteuliwa kuwa miongoni mwa mawaziri wataokamilisha malengo ya mpango wa maendeleo wa milenia wa 2015.
Katika baraza hilo jipya la mawaziri Kikwete pia amemtema, Dk James Wanyancha, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Mawaziri wengine walioanguka kwenye uchaguzi mkuu ni Mwantumu Mahiza, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Joel Bendera, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Chanzo Mwananchi.

0 comments: