Social Icons

Tuesday, October 26, 2010

MBATIA ATISHIA KULIPWA MABILIONI

Mgombea ubunge wa jimbo la Kawe kupitia NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
KAULI majukwaani wakati huu wa kampeni zimekiponza Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huenda kitadaiwa Sh bilioni 4 kutokana na madai ya kashfa dhidi ya mgombea ubunge wa jimbo la Kawe kupitia NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Hali hiyo imetokana na kauli inayodaiwa kutolewa hivi karibuni na mgombea wa Chadema katika jimbo hilo, Halima Mdee, kwamba Mbatia ni kibaraka wa CCM ambayo inamlipa Sh milioni 80 kila wiki.
Mbatia mbali na Chadema, pia imekigeukia Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) na kukidai Sh bilioni moja, kutokana na kauli ya Mkurugenzi wake, Ananilea Nkya, dhidi ya Mbatia kuwa anamdhalilisha Mdee ambaye ni mgombea mwanamke.
Mwenyekiti huyo wa NCCR-MageuziAlisema, iwapo Chadema itashindwa kumuomba radhi kwa matamshi ya Mdee katika kampeni zake ndani ya siku tatu, atalifikisha suala hilo mahakamani ili iiamuru Chadema kumlipa kiasi hicho cha fedha.
Alitoa pia siku saba kwa Tamwa ilipe fidia hiyo na iwapo itashindwa kufanya hivyo; ataiburuta mahakamani bila kutoa taarifa nyingine kwa chama hicho.
Hata hivyo, hati ya madai iliyoandikwa na kampuni ya uwakili ya The South Law Chamber inayomtetea Mbatia, inaonesha kuwa mdaiwa ni Mdee na si Chadema, kama ilivyodaiwa na Mbatia.
Waraka huo umesainiwa na Wakili Kiongozi wa Kampuni hiyo, Dk Sengondo Mvungi, ambaye pia ni Mwanasheria wa chama hicho na unakwenda kwa Mdee mwenyewe, kupitia Chadema. Mbatia, ambaye ni mara yake ya kwanza kugombea ubunge katika mkoa wa Dar es Salaam, anachuana na Mdee na Angela Kizigha wa CCM.
Katika jimbo hilo, wagombea wanaolumbana zaidi ni wa NCCR-Mageuzi na Chadema na wachambuzi wmambo ya siasa wanabashiri kuwa hali hiyo inaweza kumpa ushindi kirahisi mgombea wa CCM.
Katika mchanganuo wa madai yake, Mbatia alisema kitendo cha Mdee kudai kuwa NCCR si chama cha siasa bali cha manunuzi, chama kinamdai Sh bilioni tatu wakati Mbatia kwa kuitwa kibaraka wa CCM anayepokea kiasi hicho cha fedha kila wiki, anadai Sh bilioni moja.
Mwanasiasa huyo alisema Mdee, amekuwa akitoa madai hayo katika kampeni zake kwa muda mrefu; lakini hakutaka kuyatilia maanani kutokana na uchanga wake (Mdee) kwenye siasa.
Aliongeza kuwa sasa imemlazimu kwenda mahakamani baada ya Mdee kurudia kashfa hiyo katika mkutano wa Jumapili ambao ulihudhuriwa na mgombea urais wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, lakini akashindwa kumkemea mgombea ubunge huyo.
“Dk Slaa hakukemea kashfa hiyo, badala yake aliposimama naye akanishambulia kuwa kama mimi nataka viti maalumu, niende nikagombee ukatibu wa Chadema … hivyo nachukulia kuwa huo ni msimamo wa Chadema,” alisema Mbatia.
“Kwa maneno hayo ya Mdee, Chadema wamenisababishia msongo mkubwa wa mawazo, na nataka wakaoneshe ushahidi wao mahakamani ukibaraka wangu kwa CCM na namna ninavyolipwa Sh milioni 80 na chama hicho tawala,” alisema Mbatia.
Kuhusu Tamwa, alisema taasisi hiyo imezusha kuwa anatoa lugha za matusi, hana hoja wala sera na anatumia mbinu chafu na kejeli na kwamba ana mtazamo potofu kwa wapinzani, hivyo hafai kuwa kiongozi. Alisema madai hayo ni uzushi na uongo na yamemsababishia mshituko mkubwa na kumshushia hadhi na heshima mbele ya jamii na familia yake.
"Madhara niliyosababishiwa na taasisi yako yanatibika au kuponyeka kwa kiasi cha fedha kilichotajwa hapo juu,” inasema taarifa ya Mbatia kwenda kwa Mkurugenzi wa Tamwa.
Mdee alipopigiwa simu kuulizwa madai hayo alisema: “Mwache akashitaki.” Mkurugenzi wa Tamwa alipotafutwa kuzungumzia madai hayo ya Mbatia, simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.
SOURCE HABARI LEO

0 comments: