Mratibu wa Shindano la Miss Utalii kutoka BASATA, Rajab Zubwa akitoa ripoti ya shindano hilo lililopita mbele ya wajumbe wa kikao cha tathimini.
Afisa Kutoka Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Idara ya Utamaduni Bw.Michael Kagondela akitoa michango ya uboreshaji wa shindano la Miss Utalii kwenye kikao cha tathimini kilichofanyika wiki hii Ukumbi wa BASATA.
Baadhi ya waliokuwa washiriki wa shindano la Miss Utalii lililopita wakifuatilia kikao cha tathimini.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeendesha kikao maalum cha kutathimini shindano la urembo la utalii (miss utalii) linalofanyika kila mwaka ambapo wito umetolewa kwa waandaaji wa shindano hilo kufuata kanuni na taratibu zilizopo.Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika wiki hii kwenye Ukumbi wa BASATA,Mkurugenzi wa Idara ya ukuzaji Sanaa wa baraza hilo,Bi Vivian Shalua alisema kwamba,shindano la miss utalii limebeba utambulisho wa taifa hivyo waandaaji hawana budi kujipanga na kufanyia kazi mapungufu yote yanayokuwa yanajitokeza“Kumekuwa na mapungufu mengi katika mfumo mzima wa uendeshaji wa shindano hili,kamati haionekani, mambo mengi yamekuwa yakifanyika kinyume cha makubaliano na maandishi yaliyopo.
Hata mratibu wa shindano kutoka BASATA amekuwa hahusishwi katika masuala kadhaa” alisema Bi.Shalua wakati akitaja baadhi ya mapungufu yanayopaswa kufanyiwa kazi haraka.
Aliongeza kwamba,katika kutangaza vivutio vya utalii shindano hilo limekuwa likijikita katika maeneo ambayo tayari yanafahamika na ya eneo moja tu badala ya kwenda katika vivutio mbalimbali vilivyo katika kanda tofauti hapa nchini na kutumia mavazi na ngoma kutoka makabila mbalimbali.
Awali wakitoa michango yao, pamoja na kupongeza wazo na uwepo wa shindano lenyewe, wajumbe kutoka kada mbalimbali ndani ya jamii walishauri kuangaliwa upya kwa mfumo wa uendeshaji wa shindano hilo ambapo walitaka majukumu ya kamati ya uendeshaji shindano hilo yawekwe wazi.
“Shindano la Miss Utalii ni kubwa sana kuliko yote,ndilo limebeba nembo ya kitaifa ni lazima kwanza litangazwe na lifahamike pia washiriki wasiandaliwe kwa ajili ya kuwakilisha shindano tu bali pia kuliwakilisha taifa” alisema Michael Kagondela ambaye ni Afisa Kutoka Wizara ya Habari,Vijana,utamaduni na Michezo idara ya Utamaduni.
Aliongeza kwamba,kumekuwa na dhana mgando miongoni mwa waandaaji wa mashindano ya urembo nchini ya kuwaandaa washiriki katika kuyawakilisha mashindano yao badala ya taifa zima hali ambayo imekuwa ikisababisha wafanye vibaya kutokana na kukosa uungwaji mkono miongoni mwa watanzania walio wengi.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liko kwenye mchakato wa kuyapitia na kuyapa taswira mpya mashindano ya urembo nchini ili yawe na mfumo wa uwazi katika uendeshaji na zaidi kufuata sheria,kanuni na taratibu zilizopo.
0 comments:
Post a Comment